
WAJUMBE wa Baraza kuu UWT Wilaya ya chake Chake, wametakiwa kushikamana kusaidiana na kutokurudi nyuma katika kugombani nafasi za uongozi hususan ngazi za juu.
Hayo yameelezwa na aliyekuwa afisa Mdhamini Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Pemba, Fatma Hamad Rajab wakati alipokua akifungua kikao cha baraza kuu UWT wilaya ya Chake Chake.
Alisema mshikamano upondo na Umoja ndio kitu muhimu, hadi kupelekea Pemba kushinda majimbo ya uchaguzi kwa kishindo kikubwa, jambo ambalo halijawahi kutokea tokea mfumo wa vyama vingi kuanzishwa.
“Tokea kuanza kwa vyama vingi ushindi uliopatikana katika uchaguzi mkuu uliomalizika haujawahi kutokea, hili ni jambo la kupongeza ni dhahiri inaonesha ushindi huu umekuja kutokana na mshikamano na umoja wetu uliopo sisi wanawake”alisema.
Aidha Fatma alisikitishwa na tabia za kutokupendana, kupigiana majungu pamoja na kufanyiana fitana katika nafasi zauongozi jambo lililopelekea wagombea wengi wanawake kushindwa kupata nafasi katika uchaguzi mkuu.
Alisema majungu na fitna hazi msaidi mtu yoyote katika kufikia maendeleo bora, zaidi ya kumrudisha nyuma na mwisho wake kubakia omba omba.
Aidha aliwataka wajumbe wa baraza kuu UWT Wilaya hiyo, kuhakikisha wanashikamana na kuwa kitu kimoja ili kutokuwapa nasafi watu wenye tabia ya ufitinishaji.
Alisema wanawake wanapaswa kushirikiana, kuwa waaminifu wanawake ni jeshi kubwa lazima kupambana katika kuleta maendeleo kuliko wanaume.
Aidha aliwataka viongozi hao kumsaidia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, katika kuleta mabadiliko makubwa kwenye uongozi wake.
Aliwataka akinamama hao kujipanga na kujikwamua na umasikini kwa kubuni miradi mbali mbali ambayo itawasaidia wao katika jamii pamoja na jumuiya yao.
Akizungumzia suala la udhalilishaji na ubakaji, aliwataka wajumbe hao kutokuwafumbia macho watu wanaofanya matendo hayo na badala yake kuisaidia serikali katika kupiga vita vitendo hivyo.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa kusini Pemba Bimkubwa Mohamed Khamis, alisema katika Mkoa huo hakuna jimbo ambalo mwanamke hakugombea, kutokana na kazi kubwa walioifanya ya kuhamasishana.
Aliahidi 2025 kuwa wanawake wengi watajitokeza katika kuwania nafasi mbali mbali za uongozi, huku akiwataka wanawake wenzake kuwaunga mkono pale watakapogombania.
Katibu wa UWT Wilaya ya Chake Chake Riziki Sadra Hassan, alisema kikao hicho kinafanyika kila baada ya miezi sita, huku kikuwa na ajenda mbili moja shukurani wa wajumbe baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu na ajenda ya pili kupiga vita udhalilishaji.
Akitoa neon la shukurani kwa niaba ya wajumbe wenzake, Lela Nassor Khamia alisema kipindi cha uchaguzi kilikuwa kigumu sana lakini sasa maisha yanaendelea kila na watu wakokitu kimoja.