NA ABDI SULEIMAN.
WANANCHI wa shehia kiuyu kigongoni Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, wamempongeza mbunge wa jimbo la Kojani kwa kuendelea kuwatatulia matatizo mbali mbali yanayowakabili katika shehia yao.
Wananchi hao walisema kuwa kwa mda mrefu walikuwa na tatizo la maji katika kijiji cha fimbo, ambapo tataizo hilo kwa sasa limetatuliwa baada ya mbunge huyo kuwapatia mpira mpya wamaji na kuufukia.
“Hapa maji ilikuwa yanamwagika kwa wingi sana, hata majumbani hayafiki yanaishia hapa barabarani kutokana na kupasuaka kwa hili boba, tulishalitengeneza zaidi ya mara mbili lakini bado, sasa mbunge ametusaidia na maji yanafika”walisema.
Yussuf Faki Hamad kutoka kijiji cha Chwakani shehia ya Kiuyu Kigongoni, alimshukuru mbunge huyo kwa kupatia fedha za kuezekea nyumba yake baada ya kuungua moto hivi karibuni.
Alisema kasi ambayo mbunge huyo ameanza nayo inavutia na yakutia moyo, licha ya kumsaidia fedha lakini tayari juhudi njema zimeanza kuonekana mapema, ikiwemo kushiriki katika uchimbaji wa mtaro wa maji.
“Hatua hii nzuri ameanza kutuonyesha kama bado yuko na sisi katika shuhuli mbali mbali, tafauti na huyu mwakilishi aliyepita mwisho alitaka kutuchagisha fedha kwa ajili ya kuziba maji yanayomwagika hapa barabarani”alifahamisha.
Kwa upande wake Tamimu Ali Omar kutoka shehia hiyo, alimshukuru Mbunge huyo kwa kumapatia bati, pamoja na kufika kufariji kutokana na matatizo aliyokumbana nayo katika nyumba yake.
Alisema kazi ya kiongozi sio kukaa ofisini bali ni kupita katika shehia kusikiliza kero za wananchi pamoja na kuzitatua kero hizo moja kwa moja au kuzitengenea muda wa kuzitatua.
Alifahamisha kwamba wananchi ni watu wenye imani kubwa na viongozi wao wa majimbo, hivyo viongozi hao wanapopita katika shehia wananchi huendelea kujenga imani na viongozi hao.
“Umefika wakati na sisi kuendelea kujenga imani na kiongozi wetu, wamepita viongozi wengi katika shehia hii lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kujitolea mwisho wengine walitaka hata kutuchagisha fedha ili kuziba mpira wa maji”alisema.
Naye Mariyam Hassan Kombo aliwataka akinamama wenzake kumuunga mkono Mbunge huyo, kwani tayari ameshaonesha nia ya kuwa pamoja na akinamama wa shehia hiyo.
Alisema tayari wameshaanzsiaha vikundi vya ushirika baada ya kupatiwa elimu, huku kiongozi huyo akiwahidi kuwaunga mkono kwa kuwasaidia.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kojani Hamadi Hassan Chande, aliwataka wananchi wa jimbo hilo kutarajia mabadiliko makubwa katika jimbo lao.
Aliahidi kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zilizomo ndani ya jimbo hilo, pamoja na kuwataka wananchi kushirikiana katika kutatua changamoto hizo.
“Leo tumechimba mtaro na kuzika bomba mpya ya mfereji kazi tumeifanya kwa pamoja na wananchi, haya ndio maendeleo tunayoyataka kwenye kazi tushirikiane”alisema.
Hata hivyo alisikitishwa na baadhi ya Viongozi waliopita, kuahidi kuwasaidia wananchi na mwisho wake kushindwa kutekeleza ahadi walizozitoa, huku akiwataka wananchi kuwa wastahamilivu ili kunufaika na neema.