RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewakumbusha Viongozi wa chama cha Mapinduzi (CCM) wajibu wa kurudi kwa wananchi kuwatumikia pamoja na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili, baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.
Dk. Mwinyi amesema hayo katika Ufunguzi wa Kongamano la Jumuiya za CCM za UWT, Wazazi pamoja UVCCM lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil Kikwajuni Jijini Zanzibar, likiwa na lengo la kuwapongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli pamoja an Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa ushindi mkubwa waliopata katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2020.
Amesema wananchi wana shida mbali mbali zinazohitaji misaada kutoka kwa viongozi wao, hivyo akawataka kutokuwasahau wale waliowachagua na kubainisha kuwa huo ndio mwelekeo sahihi wa Viongozi wanaotoka CCM.
Alisema uchaguzi umemalizika, hivyo kazi kubwa ilioko mbele ya viongozi wa chama hicho ni kuwatumikia wananchi kwa kuyatekeleza mambo mbali mbali waliyoyaahidi katika kampeni pamoja na kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya 2020,- 2025.
Aidha, aliwakumbusha wanachama wa chama hicho wajibu walionao katika kujiandaa na uchaguzi ndani ya chama hicho ifikapo mwaka 2022, hivyo akawataka kujiandaa kwa msingi kuwa hatua hiyo itatoa fursa ya kupanga safu za uongozi katika chama hicho.
“Nasaha zangu kwenu wakati utakapofika, wachagueni viongozi wenye mapenzi ya dhati na CCM na sio wanaotafuta maslahi yao wenyewe kupitia CCM”, alisema.
Alieleza kuwa ni muhimu kupata viongozi wenye uwezo wa kukitumikia Chama hicho ili waweze kukivusha katika uchaguzi mkuu ujao, akiamini Chama hicho kina hazina kubwa ya viongozi bora.
Aidha, Dk. Mwinyi alisema hatua zilizoanza kuchukuliwa katika kupambana na vitendo vya ubadhirifu wa mali ya umma, uzembe na ukiukwaji wa sheria pamoja na rushwa zinalenga kuleta nidhamu katika matumzi ya fedha za Serikali.
Alisema serikali imeanza kuchukua hatua za kupambana na vitendo vya ubadhirifu wa mali ya Umma, uzembe, ukiukwaji wa sheria, pamoja na rushwa miongoni mwa watendaji wake kwa dhamira njema ya kuleta nidhamu katika matumizi ya fedha za Serikali kwa manufaa ya wananchi.
Aliwahakikishia wana CCM kuwa wale wote watakaohusika na matukio ya vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kisheria bila kumuonea mtu, hivyo akawataka wananchi kuunga mkono hatua hiyo.
“Nafahamu kuwa hatua hizi tunazozichukua kuna wengi wanazifurahia, ingawa wapo wachache zinawaumiza lakini ni vyema watuvumilie”, alisema.
Akigusia maudhui ya kufanyika kwa Kongamano hilo, Dk. Mwinyi alisema ushindi mkubwa iliopata chama hicho katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba 2020 katika pande mbili za Muungano na katika ngazi zote, ni kielelezo cha imani na matumaini waliyonayo Watazania kwa chama chao.
Alisema Watanzania wanaridhishwa na utendaji wa chama hicho na ndio maana wakafanya maamuzi ya kuendelea kukichagua kwa kura nyingi.
Alisema CCM kinajipambanua na vyama vyengine vya siasa kwa kuwa na ukweli katika utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi pamoja na ahadi zake kwa asilimia kubwa katika kila awamu ya Uongozi.
“CCM ina Ilani na sera zinazotekelezeka kulingana hali halisi ya wananchi hasa walio wanyonge, zikiwa na lengo la kuwaletea maendeleo na Ustawi wa maisha yao.
Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa Viongozi na wanachama wa Jumuiya hizo kwa uamuzi wa kuandaa Kongamano hilo lenye lengo la kumpongeza kutokana na ushindi mkubwa wa asilimia 76.27 aliopata katika Uchaguzi mkuu pamoja na kuipongeza CCM kwa kuwa na utaratibu mzuri wa Kidemokrasia wa kupata viongozi katika ngazi mbali mbali.
Aidha, aliwapongeza wanachama wa CCM kwa namna wanavyojitokeza kwa wingi katika hafla mbali mbali za ufunguzi wa miradi ya maendeleo na Uwekaji wa Mawe ya msingi katika kipindi hiki cha shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Abdalla Juma Sadalla ‘Mabodi’alisema Chama hicho kinaunga mkono hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi katika kuimarisha ustawi wa jamii pamoja na mapambano dhidi ya Udhalilishaji, sambamba na hatua ya kuunda serikali ya umoja wa Kitaifa (GNU).
Alisema hatua ya kuunda GNU itaendeleza umoja na mshikamano wa Wazanzibari na kudumisha Utawala bora.
Alitoa pongezi kwa kusimamia na kuweka kipaumbele katika uimarishaji wa uchumi wa nchi kupitia uchumi wa Buluu, akibainisha Bahari kuwa ni rasilimali muhimu hapa nchini.
Alisema CCM itaendelea kusimamia kikamilifu uibuaji wa matukio mbali mbali ya ubadhirifu na uwajibikaji.
Adha, alisema miongozo ya utekelezaji wa Jumuiya hizo inafanyakazi kwa pamoja na ndio iliosababisha kushuka hadi chini na kukipatia chama hicho ushindi.
Nae, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Othman Ali Maulid alisema Kongamano hilo linalenga kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi kwa ushindi mkubwa wa asilimia 76.27 aliopata katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba, 2020.
Alisema kwa pamoja Jumuiya hizo zinampongeza Dk. Mwinyi kutokana na hotuba mbali mbali alizozitoa kwa nyakati tofauti na hivyo kuwapa matumaini makubwa wananchi katika utumishi wake.
Katika kongamano hilo Mada tatu ziliwasilishwa , ikiwemo ya ‘Uchumi wa Buluu’ ; Utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025 pamoja na Historia ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.
Kaika Kongamano hilo lililoandaliwa na Jumuiya za CCM za UWT, Wazazi pamoja na UVCCM, Viongozi mbali mbali wa chama hicho na Serikali walishiriki, wakiwemo Wake wa Viongozi wakuu wa Kitaifa wakiongozwa na mama Mariamu Mwinyi pamoja na Wake wa Viongozi wakuu wastaafu, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Abdalla Juma Sadalla, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma, Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Mawaziri pamoja na Wabunge na Wawakilishi .