Sunday, January 5

Vyombo vya habari vyajikita kutunza amani, maridhiano PPC, Internews wakusanya nguvu kuwajengea uwezo waandishi

 

NA HAJI NASSOR, PEMBA

DISEMBA 8 mwaka huu wa 2020, Zanzibar ikiingia kwenye historia nyingine mpya ya kisiasa, baada ya kupatikana kwa serikali ya Umoja wa Kataifa ‘SUK’, ambayo ipo kikatiba.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 2010 na hasa baada ya marakebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ilifuta nafasi ya Waziri Kiongozi, kuwa kama mtendaji mkuu wa serikali.

Na hapo sasa, ikamtambua Makamu wa Pili wa rais kuwa ndie atakaekuwa mtendaji mkuu wa serikali, ingawa imeongeza kiongozi mwengine anaitwaye Makamu wa Kwanza wa rais.

Huyu mwenyewe, hutokana na kile chama kilichoshika nafasi ya pili, kwenye chaguzi mkuu wa vyama vingi nchini, na Katiba ikimtaja kuwa atateuliwa na rais.

Kumbe wa Zanzibar suala la kuwa na serikali ya Umoja wa Kitaifa sio geni, wala huu mwaka 2020 sio mara ya kwanza, maana ilianza mwaka 2010.

Ingawa mwaka 2015, ilisita kidogo kwa sababu za hapa na pale, lakini mwaka huu tena, chini ya rais wa Zanzibar wa awamu ya nane Dk. Hussein Ali Mwinyi akitokea chama cha Mapinduzi ‘CCM’ imerudi tena.

Na kwasasa, Makamu huyo wa Kwanza wa rais ni yule yule aliyeanza mwaka 2010, ingawa kwa sasa akihudumu ndani ya chama cha siasa cha ACT-Wazalendo.

Zanzibar imekuwa ikitofautisha na mataifa kadhaa ya Afrika kama vile Burundi, kwamba zinapotokezea hitilafu za ndani yenyewe, hukaa chini na kutatua jambo hilo.

Na ndio maana, kwa sasa ndani ya serikali ya Umoja wa Kitaifa ‘SUK’ na hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, viongozi wetu wapendwa Maalim Seif Sharif Hamad na Dk. Hussein Ali Mwinyi sasa wanafanya kazi pamoja.

Wote wakati wa kunadi sera zao, walishaawahidi wananchi wa Zanzibar kuwa, watahakikisha wanawaunganisha wazanzibari wote, kwa kuwaweka pamoja kwa upendo, ili kuchapuza maendeleo.

Nakumbuka sana mwezi Oktoba mwaka 2020, wakati alipokuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi, uwanja wa Gando Wete, aliahidi kuwaunganisha wazanzibari.

“Kama mkinichagua kuwa rais wa Zanzibar, pamoja na mambo kadhaa, pia nawaahidi kuwaunganisha wazazibari, ili kuona tunakuwa kitu kimoja na neema tuitumie wote,’’alisema Dk. Mwinyi.

Akaenda mabali zaidi, akisema mshikamano wa wazanzibari ndio jambo la mwanzo, maana wanapotengana inakuwa vigumu hata kuwatumikia, kwa kuwaletea maendeleo.

Maneno kama haya, pia yalitamkwa na aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, wakati akiwa kwenye uwanja wa mkutano Ditia Wawi Chake chake.

“Kwanza, mkinichagua nitahakikisha umoja, mshikamano, maridhiano ya wazanzibari ndio jambo la kwanza, na ndio kipaumbele changu kama mkinichagua,’’alisema Maalim.

Akafafanua kuwa, wazanzibari ni watu wastaarabu, wapenda umoja, mshikamano na hawapendi kugawanywa, wala kuishi kwa chuki hivyo nae azma yake ni kuwaleta pamoja.

Haya ya viongozi wetu wapendwa, yamedhihirika Disemba 8, mwaka huu, kwenye hafla ya kuapishwa kwa Makamu wa Kwanza wa rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Ambae aliweka mbele maslahi ya taifa na kuwaangalia wazanzibari wote waliopo nje na ndani, na kukubali kwa moyo mkunjufu, kuwa sehemu ya serikali ya Umoja wa wa Kitaifa Zanzibar ‘SUK’.

Wazee wa zamani wana msemo wao kuwa, waungwana wawili daima hawapoteani, na wengine wakasema chanda chema huvishwa pete, hapa utaona Dk. Mwinyi na Maalim Seif ni waungwana wawili waliopoteana na kisha kuonana.

Sasa Zanzibar kuanzia Disemba 8 ya mwaka 2020, inaendeshwa kwa mfumo wa serikali ya pamoja, kwa lengo la kuchapuza maendeleo ya wazanzibari wenyewe.

Na ndio maana Maalim Seif amesema dhamira ya yeye na Rais wa Zanzibar, Dk. Husein Ali Mwinyi kufanya kazi kwa pamoja ni kuondoa yale madhaifu yote, ambayo hupelekea wazanzibari kutofautiana na kuleta chuki miongoni mwao.

Anasema, kuwepo kwa Serikali yenye muundo wa umoja wa kitaifa, ni njia moja ya kubaini sababu ya kupata dawa kulinda tena Zanzibar isirejee katika migogoro isio ya lazima.

VYOMBO VYA HABARI VINAFANYAJE KULINDA AMANI NA MARIDHIANO HAYO?

Kwa Pemba, waandishi wa habari kuanzia mwaka 2002 waliamua kuanzisha Klabu yao, inayojulikana kwa jina la Klabu ya waandishi wa Habari Pemba PPC.

Ambapo pamoja na mambo mengine ni kutaka kuwajengea uwezo waandishi wa habari, waandaji wa makala ili kuripoti habari zilizoshiba.

Ndio maana hata hivi karibuni PPC katika kufanikisha hilo, ilishirikiana na Shirika la Internews na kuandaa mkutano wa kuwajengea uwezo waandishi namna bora ya kuandika habari za amani na maridhiano.

Mkutano huo wa siku moja, ambao ulifunguliwa na Mwenyekiti wake Bakari Mussa Juma, na kufanyika Chake Chake, aliwaambia waandishi kuwa unalengo la kuwajengea uwezo.

“Mkutano kama huu sio wa mwanzo wa kuwajengea uwezo nyinyi waandishi na lazima nilishukuru Shirika la Internews kwa kukubali kushirikian na sisi,’’anasema.

Mwandishi mkongwe Khatib Juma Mjaja, ndie aliwakumbusha mbinu waandishi hao, namna bora ya kuandika habari za maridhiano na amani.

“Tusitumie maneno ya kejeli, dharau, kukebehi tunapoandia habari, makala na utengenezaji vipindi kwani maridhiano yaliofikiwa Zanzibar yameangalia maslahi mapana ya nchi,’’alisema.

Moja kati ya eneo linalotegemewa mno na kila ili kufikisha ujumbe wa kwa haraka ni kwenye vyombo vya habari, kwa kule sauti na upeo wao kufika mbali tena kwa haraka.

Wapo wanaoamini kuwa chombo cha habari ni kama kisu au panga, kikitumika vibaya kinaweza kuwa janga na kusababisha taharuki, ingawa kikiwa kizuri huwa furaha na upendo kwa wote.

Hapa Meneja wa redio Jamii Micheweni Ali Massoud Kombo, anasema katika kuhakikisha wanayaenzi, kuyalinda maridhaino sambamba na kutunza amani na utulivu, wanaandaa vipindi mbali mbali.

Anasema, wao kama redio ya kijamii wamevutiwa na kupendezewa mno, na namna ya uwepo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, akiamini ndio suluhisho kwa maendeleo ya kweli.

Anasema, wameanzisha kipindi chao ambacho huwa kizungumzia umuhimu na faida za maraidhiano kwa wazanzibari, sambamba na utunzaji wa amani kama chachu ya kufikia maendeleo hapa Zanzibar.

Kipindic hao huruka hewani kila wiki mara mbili, (Ijumaa na Jumatatu), ambapo jina la kipindi hicho ni ’itunze amani yako’ ambapo huwa baina ya dakika 30 hadi 45.

Anasema hutegemeana na aina ya wasemaji, ambapo kwa mfano kama wiki iliyopita, walikwenda hewani hadi dakika 55, walipoweka mada ya ‘umuhimuwa maridhiano’.

“Sisi tunazungumzia amani na maridhiano kwenye kipindi hicho, maana kilichofanywa na viongozi wetu ni jambo jema na hasa kwa maslahi ya wazanzibari,’’anasema.

Hapa anawakaribisha wanaharakati, wanasiasa, wanasheria na jamii yote kuzitumia dakika 45, bila ya malipo kuzungumza na jamii ya Micheweni, juu ya umuhimu wa kutunza na kuyaenzi maridhiano.

Pamoja na vipindi hivyo maalum, Meneja huyo wa redio Jamii Micheweni, anasema wamekua wakiandika habari za umuhimuwa maridhiano na nafasi jamii katika kuendeleza hilo na amani kwa ujumla.

Lakini sio redio Jamii Micheweni pekee, wanaoendesha vipindi vya aina hiyo, lakini kwa mujibu wa mtengenezaji vipindi wa kituo cha redio cha Istqama Othman Ali Juma, nao wanaendesha vipindi vya aina hiyo.

Anabainisha kuwa, kila siku wanamkusanyiko wa matukio kupitia jina la kipindi baraza ya ‘V.I.P’ ambapo ndani yake huelezea faida za kutunza amani na utulivu.

Wameamua pia kuelezea maridhiano kwa mfumo wa kuwaacha wasikilizaji wakipiga simu ‘live’, ili kuhakikisha wanatoa maoni yao, ingawa wote wanaonesha kuridhishwa na maridhiano hayo.

“Inaonekana wananchi kwa kule kuzingatia maslahi mapana ya Zanzibar, wanaunga mkono serikali ya Umoja wa Kitaifa wakiamini ndio msingi mkuu wa maendeleo,’’anasema.

Kaimu Meneja wa Redio Jamii Mkoani, Said Omar Said, anasema kwa muda mrefu ndani ya kituo chake, wanaendesha kipindi cha utawala bora, ambapo hukusanya mambo kadhaa yakiwemo amani na utulivu.

“Sasa baada ya kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa Zanzibar, na sisi tumebadilisha mwelekeo, hivyo kila Jumanne huwa tunadakika kati ya dakika 30 hadi 45 tukigusia maridhiano,’’anasema.

Akiongeza kuwa, mfumo wa kipindi hicho huwa kwa mfumo wa kurikodi na wakati mwengine kwenda mubashara ‘live’ ili kuwapa nafasi wasikilizaji kutoa maoni yao.

“Wengi wa wasikilizaji wetu wanaonesha wamevutiwa mno na Malim Seif, kukubali kuingia kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa, ingawa wakiomba mamlaka husika kusimamia hilo,’’anasema.

Amesema wataendelea kutengeneza vipindi vya kuhamasisha jamii maridhiano hayo, kwa vile ndio mwarubaini wa kuwa na siasa za ustaarabu na kuvumiliana.

Juma Mussa Juma, anatengeneza kipindi cha sauti ya amani kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar ‘ZBC’, ambapo anasema hukusanya makundi mbali mbali.

Kwa mfano wiki iliyopita, aliendesha kipindi na vijana juu ya kujadili nafasi yao, katika kuitunza, kuiendeleza na kuiheshimu amani iliyopo Zanzibar.

Changamoto ambayo ipo masikioni kwa vijana, awali walidhani kua suala la amani na utulivu kwa ajili ya kipindi cha siasa, na mwanzo walikuwa woga kuzungumza baadae walielewe.

“Kwa sasa, najitayarisha kuongeza suala la maridhiano ndani ya kipindi hiki, ili kuzungumza na makundi mbali mbali juu ya umuhimu na faida za maridhiano yaliopo Zanzibar,’’anasema.

NINI KIFANYIKE KUENDELEZA MARIDHIANO

Wapo wanaoona kuwa, elimu kwa jamii inahitaji kwani, bado wapo wanaodhani kuwa, suala la kuendeleza maridhiano ni jambo la kisiasa na sio utamaduni.

Haji Khamis Mussa wa Wawi, anasema elimu ya kuitambua vyema serikali ya Umoja wa Kitaifa, isambaazwe hasa kwao vijana, ili iwe rahisi kuwafahamisha wengine.

Ingawa hivi karibuni, Mufti Mkuu wa Zanzibar sheikh Saleh Omar Kaabi, wakati akifungua kongamano la viongozi wa dini ukumbi wa kiwanda cha Makonyo Wawi, alisema utamaduni wa maridhiano, upo wa asili.

Alibainisha kuwa, utamaduni wa wazanzibari tokea asili, walijengeka kwa kuvumiliana, kusameheana, kupendana, kukosoana na kuridhiana, ili jambo fulani liende mbele.