IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA
NDIZI ni tunda maarufu na muhimu duniani kote.
Ingawa hasa eneo la Afrika ya Mashariki na kati, na hasa kati nchi za joto.
Mmea unaotoa ndizi, unaitwa Mgomba, ambapo kibiolojia ndizi moja ni fuu ‘mkungu’ au pigi inakua pamoja na nyingine kwenye mshikano au shazi.
Ndizi hupatikana kwa aina nyingi, na wataalamu huhesabu takriban ziko aina 100 duniani kote.
Tunda hili ambalo ni chakula kizuri kwa wanyama na hasa mwanadamu, anaweza kukisarifu katika mitindo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuila baada ya kuiva yenyewe.
Mtindo mwengine ni ule maarufu wakupika iwe kwa kuchemsha, kuweka nazi, kuzikaanga na hata mfumo wa kuchoma kwa moto.
Makabila mengi katika eneo la Afrika Mashariki, yanaitegemea ndizi kama chakula kikuu, huku wapo wanaoitumia kama lishe ya mifugo, au mti kwa ajili ya kivuli kwa wakulima wa kahawa.
Utafiti unaonesha kuwa, asili ya mti wa Mgomba unao zaa ndizi ni eneo la nchi ya Papua New Guinea.
Mmea wa Mgomba kitaalamu ‘pseudo stem’, huweza hata kufikia urefu wa mita kati ya 2 hadi 8, na majani yake hata mpaka urefu wa mita 3.5 na ikikomaa, migomba hutoa mikungu ya ndizi zenye rangi ya kijani, ambazo zikiiva hubadilika na kuwa na rangi ya manjano.
Mkungu wa ndizi unaweza kufkia kati ya uzito wa kilo 30 hadi 50, ambapo ndizi moja ‘dole’ huwa na uzito wa gramu 125, ambayo kwa makadirio huwa na maji kwa asilimia 75.
Sayansi inakuba kuwa, ndizi ni chanzo kizuri cha kujipatia vitamini B6, vitamini C na potassium, hadi miaka 30 nyuma, ndizi imegundulika kulimwa katika zaidi ya nchi 107 duniani kote.
AINA ZA NDIZI
Katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na kati, zipo aina zaidi ya 15 za ndizi ikiwa ni pamoja na kipukusa, mzuzu, mashale, matoke, bokoba, kusukari, kimalindi, mtwike, na mkono mmoja.
Asha Mohamed Hilali miaka 65 wa Kengeja Mkoani ambae ni mkulimwa wa ndizi miaka 25 sasa, anasema analima ndizi karibu aina 7, lakini aina ya bokoboko ameacha kulima.
Anasema, thamani ya ndizi hiyo iko chini na wala kwa ukanda wa kusini mwa kisiwa cha Pemba, wateja wake ni nadra mno, hivyo hakupendelea kujitia kazi isio na tija.
“Mkungu mmoja wa ndizi ya Mtikwe nimeshauuza kati ya shilingi 30,000 hadi shilingi 60, 000 lakini kwa ndizi ya aina ya boko boko tena iliyoongoka haivuuki shilingi 10,000,’’anasema.
Hata Khamis Ali Khamis wa kijiji cha Furaha Chake Chake, anasema kilimo cha ndizi ya boko boko, hakina thamani ikilinganishwa na ndizi kama za mzuzu, kipukusa na mtwike.
UBUNIFU WA KUIPANDISHI HADHI NDIZI YA BOKO BOKO
Meiye Hamad Juma ni mjasiriamali wa mbunifu wa bidhaa kama vile mafuta ya mti wa mkaratusi, chai dawa iliyotengenezwa kwa miti 10, manukato ya mwani na majani ya Mkunazi.
Mjasiriamali huyo, anasema sasa ndizi ya bokoboko imekuwa na hadhi kuliko ndizi ya aina yoyote, baada ya kubuni namna kuzalisha unga wa lishe, anaouchanganya na kokwa za boga ‘tango’.
UTAYARISHAJI WA UNGA WA LISHE YA NDIZI YA BOKOBOKO NA KOKWA ZA BOGA
Hatua ya kwanza ni kutayarisha lishe ya ndizi ya bokoboko, ambapo huchanganywa na kokwa za ‘boga’ na kisha baada ya yafuatayo huchanganywa pamoja.
Hatua ya kwanza, hutanguliwa na kumenywa kwa ndizi hizo, ingawa sharti lake kubwa, hazitakiwi kuparwa parwa kama vile mtu anaetaka kuzipika kwa ajili ya chakula.
Meiye anasema, kwenye ndizi baada ya kuondosha gamba la juu, hubakia maji maji kitaalamu yanaoitwa ‘zinc’ ambayo nayo ni muhimu kwa afya ya mwanadamu.
Hatua nyingine ni kuzianika katika jua kwa muda wa siku tatu, sawa na saa 72, ambapo baada ya kukauka kwake, hatua inayofuata ni kuziingiza kwenye mashine.
Anasema mashine hiyo lengo ni kuzisaga hadi upatikane unga wake na uwe laini, mithili ya unga wa nganu, ambapo kisha zile kokwa za tango nazo husagwa.
“Baada ya kupatikana kwa unga wa ndizi za boko boko, nao unga wa kokowa za tango, huchanganywa pamoja na hapo lishe kwa ajili ya watu wa rika zote, huwa umeshakalika,’’ anasema mbunifu.
Anasema katika uchanganyaji unga wa ndizi wa boko boko, lazima uzidi kidogo, ambapo kwa mfano hutia unga huo kilo 4, na kilo 2 kwa unga wa kokwa za boga.
“Hii naifanya kwa sababu tu kokwa za tango ni ghali mno, ndio maana natia kilo 2, kila kwenye kilo 4 za unga wa ndizi ya boko boko,’’anafafanua mbunifu huyo.
ALIUPATIA WAPI UBUNIFU HUU ?
Alianza kusikia taarifa kwa wazee (watu wenye umri mkubwa) kua, ndizi ya boko boko ni tiba tosha ya magonjwa kadhaa, ikiwa ni pamoja na kutibu miguu kama ilivyo kwa kokowa za tango.
Baada ya hapo, anasema alianza kuumiza kichwa nini afanye, ili kutengeneza lishe hiyo ambayo inaweza kuwa tiba kwa kila mmoja.
Ndipo alipoamua kununua ndizi chache katika eneo analoishi la Mavungwa shehia ya Mbuzini wilaya ya Chake chake, na kuagizishia kokwa za tango kutoka Tanzania bara.
“Nilianza kuzikausha ndizi na kuzisaga na kisha kusaga kokwa za tango na kuchanganya pamoja, niliaza kutumia mwenyewe na kisha kupata mabadiliko makubwa,’’anafafanua.
MWATEJA WAKE WANASEMA?
Khadija Muhidini Ali anasema, alishamaliza dawa na hospitali kwa tatizo la pumzi kupanda juu na kushuka bila ya mpangilio wake, na alishakata tamaa.
“Mimi nimeshaugua maradhi ya pumzi kwa muda wa miaka mitatu mfululizo, na nimeshatumia dawa nyingi, lakini nimepata ahuweni wakati naendelea na dozi, ikimalizika narejea kwenye ugonjwa,’’anasema.
Baada ya kuwasikia watu kuwa waliopona magonjwa mbali mbali kwa kutumia lishe ya ndizi ya boko boko na kokwa za tango, hakusita na alianza kutumia.
“Hadi sasa naendelea kutumia kama chakula changu cha kawaida asubuhi na jioni, na ndani ya wiki mbili baada ya kutumia, sasa pumzi zimeshakaa kwenye hali yake ya kawaida,’’anasema.
Anasema hata unyumba wake na mume wake, anaona ana nguvu za kutosha za kumuendesha mume wake, jambo ambalo hapo kabla hakuwa akimudu vyema.
“Hata unyumba sasa umekaa vyema, maana zile pumzi wakati wa tendo zimeshaondoka, kutokana na kutumia unga huu wa liseha unaotokana na ndizi ya boko boko na kokwa za tango,’’anafafanua.
Hata Amour Abdalla ‘Meja’ anasema, alikuwa anaugua ungonjwa wa sukari na kukosa nguvu za miguu wakati anapotembea.
Anasema, alitumia unga huo wa siku 14 tu na sasa yuko ‘fit’ na anauwezo wa kubeba vitu vyenye ujazo wa kilo hadi 50, jambo ambalo hapo kabla hakuwa nalo.
Asha Mussa Khamis wa wa Unguja Kiponda, anasema alitumia dawa zaidi ya aina tano za kinyeji, ili kutibu tatizo la miguu yake kukosa nguvu bila ya mafanikio, lakini lishe hiyo ilimfaa.
“Mimi nilishakata tamaa kuwa hakuna tena tiba ya miguu yangu kukosa ‘balance’ lakini nilitumia lishe hiyo baada ya kumkuta nao jirani yangu, na sasa ndio chakula changu cha asubuhi na niko vizuri,’’anafafanua.
SOKO LA UNGA WA LISHE
Mbunifu huyo anasema miongoni mwa wateja wake ni pamoja na madaktari, wafanyabiashara, wenye watoto wenye ukuaji hafifu, watoto wanaochelewa kupata ufahamu.
Anasema, sasa anatimiza mwaka tokea kubuni unga huo wa lishe, na bei yake kwa paketi moja la gramu 500 sawa na nusu kilo, huuza shilingi 3,000 hadi shilingi 4,000.
“Inabidi sasa wateja niwakimbie, maana wanakuja kwa wingi hadi wananizidi, na sasa nanunua ndizi kwa gari kutoka ununuaji wa ndizi moja moja kwa jirani,’’anasema.
Anakusudia kusema kuwa, sasa ndizi aina ya boko boko imeshapanda hadhi, maana sasa anaifuata zaidi ya kilomita 20 katika miji ya Mtambwe na Pembeni kisiwani Pemba.
UTAMBULISHO WA UNGA LISHE
Anasema anachocheti cha kutambuliwa na kukubaliwa kuzalisha bidhaa hiyo kutoka Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar ‘ZFDA’, ambao umempa uhakika wa ubora wa lishe hiyo.
Anasema changamoto kubwa kwa sasa ni kutopewa ushirikiano wa karibu na Taasisi ya Viwango Zanzibar ‘ZBS’ kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya maabara na kisha kupewa ithibati.
Athari ambayo ameshaipata ni kukosa wateja walioko nje ya Tanzania bara, ambao walifika dukani kwake, ingawa waliacha kununua bidhaa hizo, kwa kukosa nemba ya ZBS.
“Hivi karibuni walikuja tena ZBS na sasa nimeshapata matumaini ya kupewa nembo yao, maana wameshachukua bidhaa zangu zote ukiwemo unga huu wa lishe,’’anasema.
JE UNGA HUU NI LISHE TOSHA KWA AFYA?
Utafiti umeonyesha kuwa ndizi, zinatosha kukupa nishati ambayo utaitumia kwa mazoezi ya nguvu ya dakika 90, ambazo ni sawa na saa moja na nusu.
Hii ndio sababu wanamichezo wengi hutumia ndizi kabla na baada mazoezi mazito, na wakati mwingine kabla na baada ya mashindano katika mchezo husika.
Nishati si faida pekee inayopatikana kwenye ndizi, tunda hili lina faida nyingine ambayo ni kuusaidia mwili wako kupambana na kuulinda na maradhi kadhaa.
Msongo wa mawazo au mfadhaiko wa akili (stress and depression), kwa mujibu wa tafiti kadhaa, watu wengi wanaopata mfadhaiko au msongo wa mawazo hujisikia nafuu pale wanapokula ndizi.
Ndizi zina madini ya potassium na una madini chumvi kwa kiwango cha chini, jambo ambalo linafanya tunda hili kuwa dawa ya kupambana na matatizo ya presha.
Mamlaka ya chakula na dawa nchini Marekani imetambua uwezo wa ndizi, katika hili kiasi cha kuingiza wazalishaji na viwanda vya ndizi kufanya tunda hili kuwa rasmi katika mapambano ya kupunguza vifo vitokanavyo na presha na kiharusi (stroke).
Katika utafiti uliofanywa huko nchini England wanafunzi 200 walifaidika kwa kufaulu kwa mitihani ya mwaka, kwa kula mlo wa ndizi asubuhi na mchana.
COSTECH
Tume ya taifa ya sayansi na teknologia ‘COSTECH’ imekuwa ikipiga ya mgambo kuwataka wabunifu wa bidhaa, kujitokeza kwenye tume hiyo ili kuangalia wapi wanaweza kusaidiliwa.
Ndio maana hivi karubuni wakati akizungumza na waadishi wa habari na watafiti kwenye mkuatano uliofanyika Chae Chake, Afisa Mtendaji kutoka COSTECH Bunini Manyilizu, alisema waandishi wa habari wawaibue wabinifu.
Alisema COSTECH imekuwa mstari wa mbele kuwawezesha kitaaluma, fedha na hata mashine wabunifu hasa wadogo wadogo, ili kukwamua changamoto zinazowakwamisha kufikia ndoto zao.
“Waandishi wa habari hivi karibuni tuliwawezesha, kusudi wawaibue na kisha wawatangaaze wabunifu na watatifi wanaofanya mambo makubwa, lakini hawajulikani ndani ya jamii,’’anasema.
Hili lilikaziwa kamba na Afua Khalfan Mohamed, ambae ni Kamishna wa Idara ya Utafiti kutoka Tume ya Mipango Zanzibar, akisema hata serikali ya Mapinduzi imeweka mazingira rafiki ndio maana wajasiriamali wanazitia thamani bidhaa zao.