Thursday, January 9

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi atoa msamaha kwa wanafunzi (wafungwa) Arobaini na Tisa (49) waliokuwa Vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba

 

 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa msamaha kwa wanafunzi (wafungwa) Arobaini na Tisa (49) waliokuwa wakitumikia Vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za Sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Dk. Mwinyi ametoa msamaha huo kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachompa mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa waliofungwa gerezani.
Kutokana na msamaha huo, Dk. Mwinyi ameamuru kuwa kifungo kilichobaki cha wanafunzi (wafungwa) hao walionufaika na msamaha katika vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba kuwa kipindi hicho chote kinafutwa na waachiwe huru kuanzia Januari 11.2021.
Kwa vile,  Zanzibar itakuwa inasherehekea miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 Dk. Mwinyi ameona kuwa kuna sababu za kutosha za kutoa msamaha kwa walengwa walionufaika na msamaha huo kwa Unguja  ambao ni 46 na Pemba 3.
Msamaha huo hutolewa kila mwaka katika kipindi cha sherehe za Mapinduzi matukufu, huwahusisha wanafunzi ambao ni wazee sana, wenye maradhi sugu au wenye makosa madogo ambao wamebakisha muda mfupi wa kutumikia chuoni, wanaoonesha nidhamu nzuri chuoni na kujutia makosa yao.
Wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo, wenye makosa kama vile kuua kwa makusudi, wizi wa kutumia nguvu, wizi wa mali ya Umma, makosa ya kudhalilisha wanawake na watoto, makosa ya dawa za kulevya na wenye makosa mengi ya zamani kwa kawaida huwa hawapewi msamaha.