PICHA NA – OMPR-ZNZ
NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
Kampuni yamataifa ya Semcrete kutoka Nchini Misri inayojihusisha na Miundombinu ya Uwekezaji katika Miradi ya Bandari, Bara bara, Afya, Maji, Elimu na Umeme imeonyesha utayari wake wa kutaka kuwekeza Miradi yake Visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo Mhandisi Sherif Nazmy alitoa kauli hiyo wakati Ujumbe aliyouongoza wa Taasisi hiyo ya Miundombinu walipofanya mazungumao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla Afisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Sherif Nazmy alisema kutokana na mazingira rafiki ya Uwekezaji yanayokwenda sambamba na ukarimu wa Watu wa Visiwa vya Zanzibar Uongozi wa Samcrete tayari umeshajitolea wakati wowote kuanzia sasa kutaka kuwekeza Mradi utakaochaguliwa kwa Awamu ya mwanzo.
“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina fursa ya kuchagua Miundombinu yoyote ambayo Kampuni yetu itakuwa tayari kuanza nayo katika muelekeo wa kuzitumia fursa za Uwekezaji”. Alisema Mhandisi Sherif Nazmy.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kampumu ya Semcrete alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hatua hiyo ya Uongozi wa Taasisi yake ya Miundombinu imelenga kuona Ustawi wa Wananchi wa Zanzibar inaendelea kuimarika.
Mapema Afisa Mkuu wa Kampuni hiyo ya Kimataifa ya Semcrete kutoka Nchini Misri Bwana Sherf Sabry alisema Kampuni yao iko makini wakati wote Kitaaluma pamoja na Kifedha katika kuona Miradi yake inayoanzisha mahala popote inakamilika kwa wakati.
Bwana Sabri alisema Kampuni ya Semcrete tayari imeshajipatia uzoefu wa kutosha kwa Miaka mingi sasa ikiendelea kusambaa katika pembe mbali mbali za Dunia, Afrika ikiwemo Tanzania hasa katika uendelezaji wa Miradi ya Miundombinu ya Bara bara na Maduka Makubwa.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla aliueleza Uongozi huo wa Kampuni ya Semcrete kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejizatiti katika kuona Miradi ya Uwekezaji inafanikiwa vyema.
Mheshimiwa Hemed Suleiman alilazimika ndani ya mazungumzo na Uongozi huo kuwasiliana moja kwa moja kwa njia ya simu na Waziri anayesimamia masuala ya Uchumi na Uwekezeaji Zanzibar Mh. Mudrik Suleiman Soraga kukutana na Uongozi huo ili kuuchukulia hatua za haraka utayari wa Kampuni hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Kampuni ya Semcrete kwa nia yake ya kutaka kuzitumia fursa za Uwekezaji zilizopo Zanzibar na kuahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashirikiana nao ili yale malengo ya utayari wao yaweze kufanikiwa vyema.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibat tayari imeshajiandaa kuiimarisha Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA} itekeleze majukumu yake kwa kasi kubwa itakayowawezesha Wawekezaji kukamilisha maombi ya Miradi yao ndani ya kipindi kifupi.