Thursday, March 13

Wafanyaakazi wa NGOs wametakiwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuweza kupata utetezi.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

 

WAFANYAKAZI wa taasisi zisizo za kiserikali wametakiwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuweza kupata utetezi pale ambapo wanapotokezewa na matatizo katika sehemu zao za kazi.

 

Akizungumza na wafanyakazi wa taasisi za Serikali na binafsi huko katika ukumbi wa Wizara ya kilimo Weni, Mwenyekiti taifa wa ‘CHODAU’ Issa Nassor Bakar alisema kuwa imeonekana wafanyakazi wengi wa sekta  hiyo bado hawajajiunga na vyama vya wafanyakazi, hivyo kushindwa kutatua changamoto ambazo zinazotokea katika maeneo yao ya kazi.

 

Alifahamisha kuwa kumekuwa na baadhi ya waajiri kuwazuia wafanyakazi wao katika kujiunga na vyama hivyo jambo ambalo sio zuri hata kidogo.

 

Sambamba na hayo Mwenyekiti huyo aliwataka wafanyakazi hao kujiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii ZSSF ili kuweza kunufaika na na mfuko huo hapo baadae.

 

“Bado kuna changamoto kubwa ya wafanyakazi wa sekta zisizo za kiserikali kutojiunga na vyama vya wafanyakazi, kwani muamko wao bado ni mdogo sana,”alisema Issa.

 

Mapema akizungumzia suala la majukumu ya Chama chao, Mwenyekiti huyo alieleza kuwa jukumu kubwa ni kuweza kuweka mahusiano mazuri baina ya mwajiri na mwajiriwa.

 

“Lakini pia kuangalia wa maeneo ambayo waajiriwa wanayafanyia kazi iko yako salama,”alisema Mwenyekiti huyo.

 

Mbali na hayo lakini pia Chodau kimekuwa na jukumu la kuhakikisha waajiriwa wote wanapatiwa stahiki zao muhimu kutoka kwa waajiri wao ikiwa ni pamoja na mishahara yao,taarifa muhimu za kila siku na mambo ambayo ni haki kwa wafanyakazi.

 

“Pia Chodau kimekuwa kikiwapatia taaluma waajiri wote ili kuweza kuondosha changamoto ambazo zimo katika maeneo yao,”alisema Issa.