Tuesday, January 7

CYD yawafunza vijana juu ya ufungaji kuku.

 

NA ABDI SULEIMAN.

KITUO cha Majadiliano kwa Vijana Zanzibar (CYD), kimewataka vijana kutoka shehia sita zilizomo ndani ya mradi wa Fursa Mia sita (Six Hundred Opportunities -SHOP), kuongeza utayari na kusimamia miradi waliobuni katika vikundi vyao vya ushirika ili iweze kuwaletea mafanikio pamoja na kuwapatia kipato.

Kwa wilaya ya Chake Chake shehia ambazo zimo ndani ya mradi huo ni Chonga, Mgelema na Mjini Ole, Wilaya ya Wete ni shehia ya Mtemani, Selemu na Kinyikani.

Akizungumza na vijana hao wakati wa mafunzo kwa njia ya vitendo juu ya ufugaji wakuku wa kisasa, kwa shehia ya Mgelema, Kinyikani na mjini ole, mratib wa CYD Ali Shabani, alisema baada ya vijana hao kubuni miradi wanayoitaka na CYD imelezimika kuwapatia mafunzo kwa njia ya vitendo ili waweze kujifunza moja kwa moja ufugaji huo.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuweza kuwasaidia vijana katika kuendeleza kipato chao kutokana na miradi walioichangua, ili kufikia malengo na maendeleo walioyakusudia.

“CYD inatoa ujuzi unaoenda sambamba na dhamira zao, wakufunzi wanaofundisha wataendelea kuwafundisha mapaka miradi yao inasimama”alisema.

Alifahamisha kuwa vijana baada ya mafunzo ya kutosha wametaka kuongezewa nguvu katika eneo la ufugaji wa kuku wa aina ya tafauti wa kisasa.

“Tulitoa fursa kwa vijana kuchagua miradi itakayotoa tija kwao ikiwemo kupata masoko, mitaji, awali tuliwafunza juu ya ongozi na masuala ya hisa na wamefanikiwa”alisema.

Hata hivyo aliwataka vijana kuzingatia mafunzo wanayopatiwa ikiwemo dhana ya ushirika, stadi zamaisha, tabia, ujasirimali, udhibiti wa fedha na masoko, sambamba na kushajihisha vijana wenzao mitaani ili kufikia malengo.

Kwa upande wake mkufunzi wa masuala ya mifugo Pemba Makame Nyange, aliwataka vijana kutambua mbinu mbali mbali za ufugaji wa kuku wa kisasa, pamoja na kutambua masoko ya bidhaa hiyo kuwa yapo na yakutosha ndani nje ya nchi.

“Ikiwa vijana wenyewe watakubali na kuwa tayari kufuga kuku wa kisasa, basi hakuna kijana atakaeweza kubaki mitaani na kutokuwa na kazi ya kufanya”alisema.

Hata hivyo aliahidi kujitolea kuwafundisha vijana hao ufugaji wa kuku wakisasa na kuhakikisha wanasimama katika ufugaji wao.

Nao vijana hao wamesema kuwa mafunzo hayo ya ufugaji wakuku wakisasa, kwa njia ya vitendo watahakikisha wanayatumia ipasavyo na kufikia malengo ya vikundi vyao.

Mohamed Yahya Ali alisema kwa sasa tayari wameshaanza ufugaji wa kuku, kilimo, ushoni pamoja na kudizaini Mikoba, ikiwa ni moja ya malengo ya CYD kila kijana mwisho kubuni miradi yake.