Ni kweli kuna vidonda vinaweza kuacha kovu na vyengine kovu kufutika kabisa madonda yako mengi, Baba yangu aliwahi kusema ‘donda la tumbili , kila achapiapo mti hujitonesha na kamwe haliwezi kupoa alikua akinidhihaki tu na donda langu lisilopoa wakati huo litapoa wapi na kila siku kufukuzana na kambare mtoni ,mechi za mpira wa chakacha na kutoneshwa na wenzangu kwa makusudi chuoni !Utani wa kitoto
Kuna hili linaloitwa ‘donda ndugu’ , hata sijui udugu umetokea wapi pengine madhara yake ya muda mrefu kwenye mwili huwafanya ndugu kupokezana kwa kuuguza ndio maana likaitwa ‘donda la ndugu’ linahitaji ukoo mzima kulishughulikia huyu kaleta pamba,mwengine kaleta majani ya mpera , mjomba katumwa kivumbashi na shangazi anatafuta majani ya mnanaa ili mradi jeraha lipoe ndio donda ndugu donda la ukoo.
Hili donda ndugu lazima liache kovu tena lisilofutika na mgonjwa kila siku anapoliangalia kovu , hataacha kusimulia machungu ya donda, mauvivu , pengine kero la uvundo ama hata jinsi ndugu zake walivyoteseka kuliuguza donda la ukoo .Simulizi ya leo haitasimulia yaliyopita .Inatosha !.
Na sisi Zanzibar tuna donda letu la ukoo donda ndugu donda la msimu kama vile mchoo na masika donda hunuka na kukera wakati wa kuuguzwa donda letu ni la hasara na faida kwa ukoo. wakati wa kuuguza donda, ndugu hugombana , Kondo ya asubuhi na jioni maskini donda hili limesababisha hata pingu za maisha kuvufunguka ndugu kubaguana, kusemana na kutukanana ndugu kutafunana wazima wazima ukoo hukoseshana fursa na vibarua lakini donda hili pia lina faida, wale waliouguza hufaidika na walionuna wakati wa kuuguza imekula kwao, mgonjwa anapobesa wauguzaji hugonganisha gilasi wakapeana zawadi na vyeo tena vyeo bila ya kuangalia ni nani muuguzaji na ni nani mtoneshaji makusudi wa donda ! Kula baba mkubwa na baba mdogo , wauguzaji wenza ,wauguzaji wasaidizi !
Kila baada ya miaka mitano kovu hili la donda hugeuka tena donda ndugu tunatonesha donda ,tunauguza donda na tunalinda kovu bichi , wengine hudiriki kulitia pilipili donda , Hammadi ….. mgonjwa huwa tafrani
Mwenye kaya yake anasema ,tusifukue makaburi kwa yote yaliyotekea wakati wa kuuguza mgonjwa namuunga mkono lakini tunapozika kaburi tuweke alama tupande mti wa kudumu tujenge vikuta ama chambilecho zamani tunaandika jina la mfu marehemu kafa kwa kuuguzwa donda ,mauti yamemchukua akiwa kwenye foleni ya dawa aidai haki yake ,haki ya kuuguza donda ndugu lakini daktari baada ya kumchoma sindano ama kumpa dawa ya kupunguza maumivu tunaambiwa alikosea akamchoma sindano ya sumu na kumnywesha sumu ya panya.
Bahati mbaya donda letu hili ndugu huambukiza tena kama korona wakati wa jereha wapo wanaopona wapo wanaotangulia mbele ya haki Alhamdulilah tumeanza kusahau, wa vizuka walionyolewa para nywele zimeanza kuota huku familia zikitunza mayatima, wako wanaoguza majeraha , vitandani , hospitalini , wako pia watakaobakia vilema kwa maisha yao yote , Mungu awasaidie na awape subra , wako pia wanafunzi wa vile vyuo tunavyosema vinafunza amali njema kwa makosa yaleyale ya mtihani wa kuuguza donda ndugu , maskini wakati huu tukishikana mikono kwa kufurahia nafuu ya mgonjwa wenzetu hawa wanaacha familia zao wakishuhudia fashifashi na nduru za mwaka mpya wakifunzwa amali na tabia njema na utii wa sheria bila shuruti , Mungu awasalimu salama ,wamalize warudi wakiwa raia wema na simulizi kama hizi miaka ijayo iwe ni hadithi za babu zimwi
Tuwasamehe wauguzaji na watoneshaji donda ?Waliotia pilipili kwa makusudi?Waliomnywesha mgonjwa sumu ya panya na hata waliotonesha kwa makusudi tuwasamehe ?Tuvumiliane,tusameheane , tuombane msamaha kwani yaliyopita si ndweli tugange yajayo, hayo yote yanawezekana
Leo tunataka kufuta kovu la donda ndugu kama tulivyofuta hapo zamani baada ya kikao cha makubaliano cha ukoo, tunakumbushana sisi ni ndugu wa ukoo mmoja, Shangazi kwa mjomba hatupaswi kugombania fito kwani tunajenga nyuma moja ,nyumba hii si nyumba ya uyoga kama ni ya nguzo moja ni nyumba ya watu wawili ,wauguzaji wakubwa na wauguzaji wadogo wapo wanaojiona wana hati miliki ya kiwanja , wapo waliojenga msingi , wa kunyanyua viambaza na wa kuezeka paaa na wa kufanya matengenezo , nyumba hii ya ukoo ina mchwa pia wanaotafuna fito , makuti na makabati ya nguo , panya tunawafuga wenyewe kwani paka alikua marafiki na panya wamekula waya za umeme, wamechimba mashimo na usufi na hata kodoro tunalolalia, sasa tunalala sakafuni
Wakati tunauguza donda kwa mbali kovu imeanza kuota jeraha limepungua machungu kwa mashirikiano ya mwenye nia ya dhati ya kufuta kovu tunahubiri umoja ,amani ,umoja mshikamano ndugu waliogombana kwa kuuguza mgonjwa leo wanashikana mikono,kula pamoja ,safarini pamoja .Kilio kinaweza kuwa furaha eti , mkisikizana na kusameheana , hatufukui kaburi ya kuuliza nani aliweka pilipili kwenye donda ,nani alimmywesha mgonjwa sumu ya panya nani alitafuta majani ya kuponja mgonjwa, huu ni uungwana kwani muungwana nguo zikivuka huchutama, na kweli nguo zilikaribia kuvuka wauguzaji tukabakia watupu tukakaa utupu mbele ya wakwe na watoto ,aibu ya mkusanyiko wa kuuguza mgonjwa
Wakati tunaponya jeraha hili basi nyumba tuijenge pamoja, panya wakamatwe , mchwa watiwe dawa tushirikiane kuinyanyua upya nyumba hii kwani ni vigumu kusema tumefika hatua gani ya ujenzi ukarabati ufanywe tuepuke yale ya jumba la maajabu kuporomoka siku ya chrismasi . Makaburi yasifukuliwe lakini si vibaya kulijua kaburi la babu tukalipalilia upya tukakata magumu tukaandika jina ili vilembwe vijavyo wamjue babu yao alikufa lini pengine hata bila ya kuwaambia kama alifariki kwa maumivu ya donda linalotibika
Msimu wa kuuguza mgonjwa hauko mbali kiangazi hakiwezi kubakia kwa miaka minne ijayo inawezekana kuzuia kila dalili ya donda ndugu jipya, mapanga yazikwe na wale washika mapanga washikishwe adabu wajue vya kuyatumia, nwenye chokochoko za kusababisha ugomvi wakae pembeni waachwe wenye nia njema, wasiopenda umoja wa ukoo huu si muda wao huu ni wakati wa wenye huruma wanaojua kuuguza mgonjwa, wauguzaji wazalendo si wa kumtii baba tu kwa sababu ana nia ya dhati ya kuunganisha familia bali ni wa dhati kutoka mtima wa moyo .
Namalizia simulizi hii ya donda ndugu kwa kisa cha mjomba alieuguza miezi minne akiwa hospitali tatizo la mgonjwa lilikua ni kutokua na uwezo wa kula basi muuguzaji akawa na kazi ya kula kila anacholetewa mgonjwa .Mjomba akaanza kunenepa na baada ya miezi mitano puresha ikawa juu na yeye akalazwa hospitali ikabidi auguzwe, mjomba alishindwa kula hata alicholetewa hospitali, basi tuuguze kwa busara , hekima na huruma tukitambua kwamba akili ya mgonjwa ipo kwa muuguzaji.
Sisi tunaondika habari aidha kwa umakini ama weledi wa simulizi ya donda ndugu , tunaifahamu thamani ya nguvu ya ukoo na familia yenye upendo tunaweza kuishi kwa umoja , upendo na mshikamano simulizi hizi zinaungwa mkono na wenzetu wa Internews Tanzania ,ambao sote tunaamini amani ni zao la haki na kila mmoja wetu anao muarubaini wa kuponya gonjwa letu .
Tupendane hili donda linatibika !