TANGU Tanzania iingie kwenye mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, kumekuwa na mivutano mingi ikitokea ambayo mengine inatishia ustawi wa taifa.
Ingawa lengo la mfumo huu ni kukuza demokrasia na utawala bora, lakini yanayotokea hasa nyakati za uchaguzi, ni donda linalopaswa kutafutiwa tiba ya kudumu.
Matukio ya kusigana kati ya vyama vya siasa hasa vya upinzani na vyombo vya dola, sio miongoni mwa mambo yanayopendwa na wengi kwani yanavuruga amani ya nchi tunayojivunia.
Mathalan, unapovizuia vyama kuendesha harakati za kisiasa ikiwemo kufanya mikutano ya ndani na nje, ni dhahiri unajenga taswira mbaya kuwa serikali haiko tayari kwa mfumo wa vyama vingi.
Hali inakuwa mbaya zaidi pale zuio hilo linapobagua na kukiacha chama tawala kikifanya mambo yake bila kuguswa huku wengine wakibanwa, na pale wanapojaribu kutimiza haki yao hiyo kikatiba, jeshi la Polisi linapambana nao.
Haileti picha nzuri kushuhudia vyumba vya mahabusu vikijaa viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani kwa sababu tu wamekuwa wakipigania haki yao iliyopo kisheria
Pengine haya yanatokea kutokana na mfumo wa kuwapata viongozi wa Tume zetu za uchaguzi kuanzia Wenyeviti na makamishna wao
Inafahamika kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na ile ya Taifa Tanzania (NEC) ni viongozi wanaochaguliwa na marais wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Tunatambua kwamba hili ni takwa la sheria , lakini kama tutalenga jicho la mbali la kutafuta muafaka wa kisiasa kabla ya uchaguzi hili ni jambo la kulifikiria sana
Upatikanaji wa wakuu wa taasisi hizo nyeti kupitia uteuzi wa marais, si njia inayohakikisha haki kutendeka hasa katika mchakato wa uchaguzi mkuu kuanzia uandikishaji wa wapiga kura hadi kumalizika kwake na kupata viongozi.
Katika nchi zetu za Afrika, Mwenyekiti gani wa Tume ya Uchaguzi mwenye ubavu wa kufumba macho na kukubali matokeo yanayompa ushindi mgombea urais wa chama cha upinzani?
Ni tume gani itakayoridhia kiongozi aliyeichagulia Mwenyekiti wake ashindwe na kumtangaza mpinzani wake kuwa kidedea?
Hizi ndizo tunazoziita ‘Conflicts of interests’ (Migogoro ya kimaslahi), ambapo Mwenyekiti wa Tume anakuwepo kitini kwa ajili ya kulinda nafasi ya aliyemteua, na haya yakitendeka, baada ya uchaguzi lazima atakuwa na donge nono kama zawadi kutoka kwa bosi wake.
Aidha, si aghalabu kuona Mwenyekiti anayepewa dhamana ya kuongoza Tume ya Uchaguzi kuwa ni mtu anayetokea katika mrengo wa wapinzani wanaowania kuung’oa utawala uliopo.
Kwa muktadha huo, nimepata wazo la kuzishauri serikali zote mbili, SMZ na SMT zibadilishe mfumo huo kwa kuwavua marais kofia za kuteua Wenyeviti wa Tume za Uchaguzi, ZEC na NEC pamoja na makamishna wao.Hili litasaidia sana kupunguza manunguniko pengine na hata maafa wakati wa uchaguzi kama tulivyozoea
Nafasi hizo sasa ziwe ajira za mkataba zitakazoratibiwa na kutangazwa kupitia Kamisheni za Utumishi, ili kila anaehisi anavyo vigezo stahiki aombe bila kuangaliwa ni wa mrengo gani kisiasa.
Baada ya Tume kujiridhisha ifanye mchujo na kuwaita wachache kwa ajili ya kufanyiwa usaili, na watakaopata alama za juu ndio wakabidhiwa majukumu ya kuziongoza tume hizo baada ya kuapishwa kuzitumikia kwa haki na uadilifu.
Halikadhalika, Wenyeviti hao ndio watakaokuwa na wajibu wa kuteua makamishna kutoka vyama tofauti na kwa uwiano ulio sawa.
Sisemi hatua hii itaondosha kabisa uwezekano wa Wenyeviti kuonesha upendeleo kwa chama tawala, bali angalau itakuwa mwanzo wa safari kuelekea kwenye tume huru za uchaguzi ambazo kambi za upinzani zimekuwa zikizililia kila uchao.
Naelewa wazi kwamba hao watakaoomba na kuajiriwa watakuwa na vyama vyao, lakini katika kazi ninaamini wataweka kando ushabiki na umamluki wa kuvibeba na badala yake wataongozwa na viapo na mikataba watakayosaini kufanyia kazi.
Tume za Utumishi zitakazowaajiri zitakuwa na haki ya kuwaengua pale watakapoonekana wanakwenda kinyume na masharti ya mikataba.
Sote ni mashuhuda wa yaliyotokea katika chaguzi kadhaa za Zanzibar zilizohusisha vyama vingi, ikiwemo Mwenyekiti kufuta matokeo mwaka 2015 baada ya kubainika wazi ushindi wa chama cha upinzani hauzuiliki. Hatutaki hayo yajirejee.
Katika mfumo wa sasa, ni vigumu kwa tume zetu kutenda haki ingawa kauli zao hutolewa kuuaminisha umma na mataifa kwamba wao ni tume huru.Waswahili wanasema anaemkodi kabili ndie mwenye uwezo wa kuchagua wimbo autakao . Na hawa makabili wa Tume za Uchaguzi inawezekana wakachagua nyimbo na hata mdundo wa kucheza iwapo mifumo ya Tume hizi itaendelea
Kama kweli tumedhamiria kukuza demokrasia na kupata viongozi wanaoshinda kwa haki, ninashauri tuangalie uwezekano huu wa kuwa na Wenyeviti na makamisha wa ZEC na NEC walioajiriwa kwa utaratibu maalumu badala ya kuwa wateule wa marais.
Hivi sasa kila mtu anaimba wimbo wa amani , umoja , utulivu na mshikamano. Kwenye majukwaa ya kisiasa , misikitini na hata shughuli za kitaifa . Ni sawa tuendelee kuuimba wimbo huu kuku tukicheza mdundo wake kwa upendo. Makovu ya vidonda vya uchaguzi tumeanza kuyasahau lakini si vyema tukaendelea kukata majeraha mengine kila baada ya miaka mitano. Tuseme inatosha