NA ABDI SULEIMAN.
MBUNGE wa Viti Maalumu wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, amewataka vijana kisiwani Pemba kuendelea kuyajali na kuyathamini Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 kwani ndio yaliyotoa fursa sawa kwa wananchi wa Zanzibar.
Alisema vijana ndio wenye nguvu kwa sasa kuyalinda na kuyatetea, kwani wazee wamefanya kazi kuba hadi sasa kuhakikisha Mapinduzi hayo yatetereki, hivyo vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele na kutokukubali kubabaika kwa jambo lolote juu ya Mapinduzi hayo.
Mbunge huyo aliyaeleza hayo wakati alipokua akizungumza na Wananchi, WanaCCM na wazee wa Jojo Wilaya ya Wete, mara baada ya uwekaji wa Jiwe la Msingi Maskani ya CCM ya Dk. Ali Mohamed Shein iliyoko Jojo.
Alisema Mapinduzi ya 1964 yameweza kutoa fusa zote kwa wazanzibari, ikiwemo suala zima la elimu bure, matibabu bure, hivyo vijana wanapaswa kumuenzi Marehemu Mzee karume kwa Vitendo.
“Hatuna budi kuwashukuru viongozi wetu wa nchi Rasi wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi na Rais wa SMT Dk.John Magufuli, kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi zao walizoziweka kwa wananchi wao Zanzibar na Tanzania, pamoja na kuhakikisha suala la amani na utulivu linaendelea kuwepo”alisema.
Hata hivyo aliwataka vijana hao kujiandaa kuupokea uchumi wa buluu kwa vitendo, kwani viwanda mbali mbali vinatarajiwa kujengwa ikiwemo vya uvuvi pamoja na chumvi, mwani kwani viwanda hivyo vitaweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana.
Kwa upande wake katibu wa CCM Jimbo la Kojani Ali Omar Ali, alisema vijana hao sio wa kupanda gari na kushuka bali wameandaliwa na kukomaa kisiasa kwa sasa.
Naye Mohamed Khatib Faki kutoka Maskani ya Karume kruu ya Kambini Kichokochwe, alisema vijana wameanza vizuri kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya Nane, katika kupiga hatua kimaendeleo kwa kubuni miradi mbali mbali ya kimaendeleo.
Akisoma risala ya maskani ya Maskani ya Dk.Ali Mohamed Shein, kijana Bishara Suleiman Ali alisema ujenzi huo ulianza mwaka 2018 maskani ikiwa na vijana 12 hadi sasa inavijana 50.
Alisema jumla ya shilingi Milioni 7.5 zimetumika katika ujenzi wa maskani hiyo hadi kuezekwa, ambapo kwa sasa imebakia milango, madirisha na kupigwa palasta.
Aidha alisema lengo la kuanzishwa kwa maskani hiyo ni vijana kuamua kukaa pamoja na kujikwamua na umaskini kupitia kilimo, ufumaji na ufugaji wa kuku.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kaskazini Pemba Asia Sharif Omar, aliahidi kutoa fedha kwa ajili ya madirisha saba na milango mine ya maskani hiyo.