Sunday, January 5

VIJANA wajenga imani na Serekali ya Umoja wa Kitaifa.

 

NA ABDI SULEIMAN.

ILIKUWA ni Disemba 7/2020, Zanzibar imeandika hitoria kwa mara ya pili, baada ya mivutano mingi ya kisiasa kufuatia maalim Seif Sharif Hamad kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Kuteuliwa kwa Makamu wa kwanza wa Rais Maalimu Seif Sharif kutoka chama cha ACT-Wazalendo kumepunguza raghba  kwa baadhi ya wananchi, huku wengine wakianza kujenga matumaini na viongozi wa juu wa serikali iliyopo madarakani.

Kama tunavojuwa vijana ndio nguvu kazi kubwa ya Taifa lolote duniani, ndio wanaotumiwa vibaya na wanasiasa wakati wote wa kampeni lakini sasa wameonyesha kujawa na furaa kufuatia kuwepo kwa serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar.

Hivi karibuni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema wakati umefika kwa wazanzibari wote kuwa wamoja, wenye kufanya kazi kwa mashirikiano ili kuiweka nchi vizuri katika kipindi kifupi tokea Serikali ya awamu ya nane kukaa madarakani.

Amesema Zanzibar bila ya maridhiano ya pamoja kati ya vyama vilivyomo nchini, maendeleo hayawezi kupatikana hivyo ni vyema kila mmoja aweze kuthamini maridhiano yaliyopo.

“Nampongeza Dk, Mwinyi, kwa uamuzi wake kwani haikuwa rahisi kuungana kwetu bali tumeongozwa na maslahi ya Zanzibar na matakwa ya katiba yetu”,amesema.

VIJANA WANAMTAZAMO GANI WAO?

Rahma Mwadini Juma mkaazi wa Kichungwani yeye anasema maridhiano yaliyopo ameyapokea vizuri, kutokana na viongozi kuwa kitu kimoja, kwani hapo nyuma ilikuwa ngumu kufanya kazi zao vijana kutokana na kutafautiana.

“Sasa sio changamoto wala tataizo tena kwetu vijana saivi sote tunafanmya kazi kwa umoja, hapo nyuma katika baraza letu ilikua ngumu kila mtu alikuwa anafanya yake, maridhinaho haya yametusaidia hata sisi kungana tena”amesema.

Amesema kuwepo kwa serikali ya SUK tayari wameshajenga mategemeo makubwa kwao, ikiwemo kunufaika na miradi mbali mbali ambayo Rais Dk. Mwinyi tayari ameshaeleza kuwa inakuja.

Abdilla Saleh Issa Kutoka Wilaya ya Mkoani, amesema maridhiano amaeyapokea kwa moyo mkunjufu kwani ni ishara njema ya mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa Zanzibar.

Anasema hilo limempa matumaini kutokana na kauli anazozitoa Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi, juu ya dhamira anayotaka kuijenga serikali ya awamu ya nane, ikiwemo suala la kuwapa kipaombele zaidi Vijana.

“Vijana wanapaswa kuwa kitu kimoja, lazima washiriki kikamilifu katika kulinda amani na umoja uliopo, maendeleo ya vijana hayatopatikana, ikiwa nchi haina maridhiano miongoni mwao”amesema.

Kulthum Khamis Vuai mmoja ya vijana kutoka Wete, anasema baada ya kuwepo kwa maridhiano kila mmoja anapaswa kwa nafasi yake kuwajibika katika utendaji wa kazi ili malengo ya serikali yaweze kufikiwa.

“sisi vijana tunawategemea viongozi wetu kujua njia zipi tuzifuate ili kutimiza malengo yetu, sasa kama hakuna maridhiano umoja na mshikamano ni vigumu kusimama”amesema.

WANAHARAKATI WANAYAPI WAO

Tatu Abdalla Salim ni mwanaharakati wa kutetea haki za kimsingi kwa makundi yaliyopembezoni, amesema moja kwa moja wanafika kwa jamii na kushauri jamii kukubaliana na maridhiano yaliyopo na yanaweza kuleta mafanikio makubwa.

Amesema hushajihisha kushiriki katika shuhuli za kuleta maendeleo bila ya kuangalia sura au anatoka chama Fulani, bali wanapaswa kushiriki katika shuhuli zote za maendeleo, pamoja na viongozi kuacha tafauti zao ili kufikia maendeleo ya kweli.

Kwa upande mwengine mwanaharakati huyo amesema katika kufikia maridhiano ya kweli na maendeleo yanayohitajika, wanapaswa kuacha tabia ya kuambiana kuwa sio wetu,,,, kufanya hivo mafanikio yatapatikana.

“Hapo kabla kabla ya kuwepo maridhiano hata utendaji kazi katika taasisi ulikuwa ukizorota, watu wakijadili sana siasa na kutokuangalia faida ya jambo linalofanywa”anasema.

Mwanaisha Hamad Omar kutoka jumuiya ya maendeleo Tumbe, anasema kuwa tayari wananchi wameshaondosha tafauti zao na kushirikiana katika shuhuli mbali mbali za maendeleo.

“Sasa wananchi wameanza kuunganisha nguvu zao kwa kuona hili jambo ni lakwao, sio la CCM, ACT wala CUF, haya ndio maridhiano tunayoyataka ili kufikia malengo ya serikali yetu ya awamu ya nane”amesema.

Star Khamis Salum ambaye ni mwanaharakati katika masuala ya vijana, amezishukuru Serikali ya SMT na SMZ, kwa kudumisha amani na utulivu katika muda waote wa uchaguzi na baada ya uchguzi, pamoja kuendeleza uwepo wa serikali ya SUK nchini.

Serikali haikukosea wala kufanya jambo baya kwani maridhiano hayo ni kuchenga nchi, ili kuhakikisha maendeleo yanakuwepo pamoja na kuungwa mkono na mashirika mbali mbali ya maendeleo.

Amesema kazi iliyobakia ni kuhakikisha wananchi wanayaendeleza maridhiano hayo, kwa lengo la kuhakikisha wanafikia maendeleo ya kiuchumi, kijamii kama ilivyodhamira za viongozi husika.

VIONGOZI WA DINI WAO WANASEMAJE.

Mufti mkuu wa Zanzibar sheikh Saleh Omar Kaabi, amesema uvumilivu wa asili kwa wazanzibari na kushiba kwao dini, ndiko kulikopelekea kuwa hadi sasa, kuendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu.

Asili ya wazanzibari ni watu wa kuvumiliana, kusaidiana, kuheshimiana, kupendana na waliojaaliwa kuwa wameshiba dini, ambapo hayo yote hupelekea wanapokosana kisha kupatana.

Zipo nchi kadhaa za ukanda wa Afrika mashariki na kati, zimeingia kwenye migogoro na kujaribu kutafuta sulhu na kisha kushindikana hadi wanapowatafuta wasuluhishi kutoka nje ya miongoni mwao.

tayari nchi kama za Kenya, Uganda, Sudan zimeshatuma wajumbe wao na kufika Zanzibar, ili kujifunza, namna mbavyo na wao wanaweza kuiga.

“Hata wiki iliyopita niliwapokea wenzetu kutoka nchini Sudan, wamekuja kujifunza namna ya kutatua changamoto za mizozo ndani ya mataifa, kama tunavyofanya sisi hapa Zanzibar,’’alieleza.

Amewasisitiza vijana kutokubali kutumiwa na wachache, kwa lengo la kuichafua amani iliyopo,hivyo wakikubali kutumiwa kama silaha ya uchafuzi wa amani, waathirika wakubwa baada ya nawawake na watoto hufuata wao.

 

Askofu Michael hafidh Henry Hafidh kutoka kanisa la Anglikana Zanzibar, amesema amani na utulivu ndio muhimili wa nchi katika shuhuli za kimaendeleo, hivyo wananchi wanapaswa kuitunza na kuithamini amani hiyo.

Amesema wanapaswa kuendeleza amani na utulivu iliyopo nchini, pamoja na kuvumiliana ili kufanikisha harakati zamaendeleo Serikalini.

“Wazanzibari wanajivunia amani ni watu wanaoishi kwa upendo toka zamani, wanapendana, wanavumiliana ni watu wa dini, vyama, wakiristo na waislamu sio watu wakugombana bali ni wavumilivu”alisema.

Viongozi wa vyama vya siasa nchini kuendelea kuvumiliana, pamoja na kuwa wamoja kama alivyofanya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwanyi na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo kuvumiliana hadi kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, baada ya kuweka uzalendo wa nchi mbele.

Hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwasilimia waumini wa dini ya Kiislamu, katika Masjid Afraa Bint Issa (Msikiti Shurba), Kidongochekundu, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja mara baada ya kujumuika nao katika Sala ya Ijumaa, alisema mambo matatu muhimu ambayo yakifuatwa yataleta maendeleo ikiwemo amani, umoja na suala zima la uwajibikaji.

 

Huku Maalim Seif ambaye ni makamo wa kwanza wa Rais amesihi wananchi kuacha tofauti zao za kisiasa kwani ndizo zinazoleta mifarakano na badala yake waungane kwa kuleta maendeleo ya wazanzibari.

 

“Mimi na Rais Mwinyi tunafanya kazi kwa pamoja  kama  katiba yetu inavotutaka na niwahakikishie katika Serikali hii ya awamu ya nane hayatotokea maovu kwani viongozi tuko makini”,amesema.

Wazanzibari wote ni wamoja na wenye maslahi ya hatma ya Zanzibar na hakuna haja ya kuleta malumbano kwani kufanya hivyo kunaipotezea hadhi nchi na wananchi wote.

Hivi karibuni Jumuiya ya waandishi wa habari Kisiwani Pemba (PPC)imeendesha mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari, ambapo Mkufunzi wa mafunzo hayo Khatib Juma Mjaja, amesema hao wanapaswa kutumia kalamu zao vizuri katika kuhamasisha amani nchini, ili wananchi waendelee kuitunza.

Amesema amani inahitajika siku zote katika jamii, hivyo kuna haja kwa waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuwaelimisha wananchi, ili wapate uelewa zaidi, jambo ambalo litasaidia kuendelea kuitunza amani.

 

“Sisi ni sauti ya wasio na sauti, kwa kutumia vyombo vyetu tusuluhishe migogoro na tusiendeleze, hivyo tutakuwa tumeisaidia sana jamii yetu”, amesema Mjaja.

 

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) Bakar Mussa Juma amesema waandishi wa habari wana dhima kubwa ya kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza amani nchini.

 

“Amani ikitoweka hakuna kitu kinachofanyika, hivyo kama waandishi muda huu tuutumie kuwaelimisha wananchi, ili kuendeleza kuitunza amani iliyopo”, amesema.

 

Kwa pamoja tunaweza kuendeleza, kuyalinda na kuthamini maridhinao yaliyopo, katika suala zima la kulinda amani ya nchi.