Thursday, January 9

Kuapishwa kwa Joe Biden: Jinsi rais wa Marekani anavyotazamiwa kufuta nyayo za Trump Afrika

Maelezo ya picha, Joe Biden anatarajiwa kufuta baadhi ya sera za mtangulizi wake Donald Trump kuihusu Afrika
  • Mohammed AbdulRahman
  • Mchambuzi

Saa 6 zilizopita

Dunia inasubiri kushuhudia tukio kubwa katika siasa za Marekani. Ni kuapishwa mdemokrat Joe Biden kuwa Rais wa 46 wa taifa hilo kubwa . Tukio hilo pia litamaliza kipindi cha utawala wa miaka minne cha mrepublican Donald Trump, kilichokua na utata na mtikisiko katika siasa za kimataifa. Wakati huo huo baada ya kupewa mgongo na Trump bara la Afrika litarajie nini kutokana na utawala wa Biden na makamu wake Kamala Harris?

Afrika lilianza kupewa kipaumbele na Marekani mnamo miaka ya 1960, wakati mataifa kadhaa yalipoanza kujinasua na ukoloni na kuanza kujipatia uhuru. Lakini sera za uhusiano huo zilitofautiana kwa kutegemea utawala gani uko madarakani, wa Warepublican au Wademokrats.

Marekani ilitoa nafasi nyingi za elimu ya juu kwa wanafunzi kutoka mataifa kama Nigeria, Ghana na Kenya hasa wakati wa utawala wa muda mfupi wa mdemokrat John F.Kennedy.

Rais Kennedy na mdogo wake Robert aliyekuwa mwanasheria mkuu walijenga uhusiano wa karibu na bara la Afrika. Rais Kennedy aliuawa 1963 miaka miwili baada ya kuapishwa kuliongoza taifa hilo kubwa. Robert Kennedy aliyeamua kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania urais miaka michache baadaye naye aliuwawa Juni 1968 .

ADVERTISEMENT

Wakati huo ulikuwa ni enzi ya vita baridi, na Afrika ulikuwa zaidi uwanja wa kutafuta ushawishi wa kisiasa. Kilikuwa kipindi cha mvutano kati ya kambi ya Mashariki chini ya himaya ya Muungano wa Jamhuri za Kisovieti (Urusi ya zamani) na kambi ya Magharibi iliyoongozwa na Marekani.

Mojawapo ya maeneo ambayo Marekani ilijiingiza ni katika mgogoro wa Congo ambako wiki iliopita mnamo Januari 17 ilikuwa kumbukumbu ya miaka 60 tokea alipouwawa Waziri wake mkuu wa kwanza Patrice Emery Lumumba.

Dola ya kikoloni Ubeligiji na pia Marekani zilimshutumu kuwa akielemea upande wa Urusi na kuwa hatari kwa masilahi yake na Marekani. Utajiri mkubwa wa rasilimali nchini Congo ulikuwa muhimu kwa masilahi ya nchi za kigeni. Msaada wa Marekani ukitolewa kwa kuzingatia falsafa na muelekeo wa kisiasa wa nchi husika.

Marais waliobadili sura ya uhusiano na Afrika

Kuimarika hasa kwa uhusiano wa Marekani na Afrika kiuchumi kulianza baada ya kumalizika enzi ya vita baridi, wakati wa tawala za Bill Clinton, George W.Bush na Barack Obama ambapo ajenda kuhusu Afrika ilipata uungaji mkono kutoka vyama vyote na mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani, wawakilishi na Seneti.

Maelezo ya picha, Obama alirefusha zaidi mpango wa ushirikiano wa Marekani na Afrika maarufu kama AGOA ulioanzishwa na Bill Clinton.

Wakati wa utawala wa Clinton biashara ya Afrika chini ya ule mpango wa African Growth and Opportunity Act (AGOA) wa mwaka 2000 ambao uligeuka sheria ukirefushwa na Bush na Obama. Kimsingi umerefushwa hadi 2025.

Mkataba huo uliyafungulia mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara , soko la biashara nchini Marekani. Masharti yake yalikuwa nchi husika zihakikishe zinapiga hatua kuboresha demokrasia, utawala wa sharia na haki za binadamu.

Sera zao ziliungana na msaada mkubwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo barani humo. 2003 Bush alizindua mpango wa msaada wa dharura wa kupambana na Ukimwii, Emergency for Aids Relief

Utawala wa Obama ulitenga karibu dola bilioni 8 kwa mwaka kulisaidia bara hilo, hasa kupitia taasisi zilizoko chini ya Wizara ya mambo ya nchi za nje.

Mshikamano wa viongozi hao na Afrika ulidhihirika zaidi, Julai 2013, wakati walipokutana wote nchini Tanzania, wakati wa ziara ya Obama nchini humo. Lilikuwa tukio la aina yake kwa marais wawili wa zamani wa Marekani na mwenzao aliyekuwa madarakani kukutana katika nchi moja ya kigeni kwa wakati mmoja. Miaka minne ya Trump iliuvuruga kabisa uhusiano wa Marekani na Afrika.

jinsi sera ya Trump ilivyo hujumu uhusiano huo

Miaka minne ya utawala wa Donald Trump, chini ya kauli yake mbiu ya “Marekani kwanza” haikulitilia maanani hata kidogo bara la Afrika. Kwa mshangao wa wengi, kiongozi huyo alikwenda umbali wa kuzikashifu nchi za Kiafrika akitumia lugha chafu na akaupuuza hata wito wa kumtaka aombe radhi.

Maelezo ya picha, Utawala wa Donald Trump haukutilia maanani masuala ya Afrika na badala yake aliikashifu.

Msimamo wake kuhusu Afrika, ulihujumu ushirikiano wa kibiashara na mataifa mbali mbali pamoja na Jumuiya za kiuchumi barani humo. Utawala wa Biden unaangaliwa kwa matumaini na Afrika hasa katika wakati ambapo hivi karibuni bara hilo limezindua rasmi mpango wake wa kuwa eneo la biashara huru.

Chini ya utaratibu huo miongoni mwa watakaonufaika ni Jumuiya ya Afrika Mashariki na hususan nchi kama Kenya yenye uchumi wenye nguvu katika ukanda huo.

Kuna matumaini pia Biden ataondoa kikwazo cha Trump kuzuia kuchanguliwa Mnigeria Bibi Ngozi Okonjo-Iweala kuwa mkuu wa Shirika la Biashara Duniani WTO.

Amani na Demokrasia

Mtihani mkubwa kwa utawala wa Biden utakuwa ni kuzisaidia nchi za Kiafrika kupambana na ugaidi kuanzia kundi la Al Shabab nchini Somalia, Boko Haram Nigeria na Waislamu wa Itikadi kali nchini Mali na Msumbiji.

Maelezo ya picha, Kibarua kikubwa kwa Joe Biden kitakua ni kukabiliana na makundi ya ugaidi katika nchi za Afrika

Vilevile Waafrika wanamtarajia Biden kama alivyoahidi kubatilisha uamuzi wa Trump kupiga marufuku raia wa nchi sita za Afrika zenye idadi kubwa ya Waislamu kuingia Marekani. Nchi hizo ni Nigeria, Sudani, Tanzania, Eritrea, Libya na Somalia. Tangazo lake lilikua la nyongeza katika marufuku aliyoitangaza dhidi ya nchi kadhaa za Kiislamu .

Aidha kuna suala kuu la demokrasia na utawala bora, ambapo miaka minne ya Trump imeshuhudia nchi nyingi barani humo zikirudi nyuma katika suala la demokrasia na sura za kidikteta zikiongezeka.

Sababu moja wapo ni kwamba kutokana na utawala wa Trump kutojali matukio barani Afrika, watawala wakandamizaji walijihisi wako huru na vitisho vya awali vya kuwekewa masharti kama vile vikwazo, kuhakisha chaguzi zinakuwa huru na haki havipo tena.

Hapa wanaharakati ambao kwa kawaida huyageukia mataifa makubwa kulalamika,mambo yanapokwenda kombo,watatarajia kutakuwa tena na shinikizo ili hali ibadilike.

Utatuzi wa changamoto za ndani ndiyo ufunguo

Pamoja na kuzuka matumaini mapya kutokana na Biden kuingia Ikulu, kiongozi huyo anakabiliwa na changamoto kubwa ambayo ni Janga la Covid-19 .

Trump alilipuuza janga hilo na kuiacha Marekani ikishikilia nafasi ya kwanza ya kuwa na idadi kubwa ya maambukizi na vifo duniani.

Biden ameahidi katika siku 100 za kwanza za utawala wake atahakikisha zoezi la chanjo ya kinga dhidi ya Corona linakwenda haraka.

Mabadiliko ya sera za Marekani kuelekea Afrika bila shaka yatakuwa katika muktadha wa marekebisho ya sera zake katika siasa za Kimataifa na la msingi ni kwamba kutategemea ni kwa kasi ya kiasi gani utawala wa Biden utafanikiwa kukabiliana na changamoto za ndani.

Zaidi ya yote atahitaji kuliunganisha pamoja taifa hilo ambalo limegawika zaidi baada ya uchaguzi wa Novemba 3, kwasababu ya Trump kukataa kuyakubali matokeo ya uchaguzi kwa hoja ya kwamba kulikuwa na wizi, madai ambayo ameshindwa kuyathibitisha.

 

  • Mohammed AbdulRahman
  • Mchambuzi

Saa 6 zilizopita