- Anne Ngugi
- BBC Swahili
Maisha ya Bi. Alice Booth yamegeuka kuwa ya ajabu kila siku inayoitwa leo.
Bi Alice anasema kila anapofikiria maisha yake ya nyuma anashangaa ni vipi ameweza kupiga hatua chanya baada ya matukio mawili mazito kutokea katika maisha yake.
Tukio la kwanza lilikuwa ni kumpoteza mume wake wa kwanza na baadaye akaugua saratani.
Lakini bila kutarajia, alipata mpenzi mwingine ambaye wameweza kujaliwa mtoto licha ya umri wake kuwa mkubwa.
Awali madaktari walimwambia si rahisi kushika kwa yeye kushika mimba tena.
Maisha yalivyogeua kuwa machungu
Alice alikutana na mume wake wa kwanza aliyejulikana kwa jina la utani kama Gee wakiwa katika chuo kikuu cha Kenyatta nchini Kenya.
“Katika ndoa yangu ya kwanza, tulijaliwa watoto watatu, wawili wa kike na mmoja wa kiume hivi sasa wana umri wa miaka 21, 19, na 15 mtawalia ,” alisema Alice
Bi Alice anasema ilipofika mwaka 2006 mume wake alianza kuugua.
Walitafuta usaidizi wa kimatibabu hospitalini kwa miaka kadhaa na alipewa dawa za kumsaidia kupunguza maumivu ila hakupata nafuu.
Alipofanyiwa uchunguzi wa kina, alipatikana na ugonjwa wa moyo kwa jina ‘rheumatic heart disease’.
Mwaka wa 2007 alifanyiwa upasuaji kwenye moyo lakini alianza kupata matatizo zaidi baada ya upasuaji na akafariki dunia mwezi Novemba.
Maisha yaligeuka na kuwa machungu kwake.
Alice anakumbuka kuwa kukubali kifo cha mume wake haikuwa rahisi.
Mama huyu anasema kuwa aliamua kupiga moyo konde na kuchukua majukumu ya baba na mama katika kuwapatia mahitaji watoto wake ambao walikuwa na kati ya miaka 8 na 2 mahitaji yao.
Pigo baada ya pigo
Mnamo mwaka 2013 wakati alipokuwa ameanza kuzoea maisha ya kuwa mjane, aligundulika kuwa na ugonjwa wa saratani kwa jina ‘hodgkins lymphoma’.
Lymphoma ni kansa inayoendelea katika kundi la seli nyeupe za damu inayoitwa ‘lymphocytes’, ambapo mwili wa binadamu unategemea aina mbalimbali za seli kufanya kazi katika mfumo wa kinga.
Alice alitafuta tiba mpaka nchini India ambapo mwishoni mwa mwaka huo alipofanyiwa vipimo vingine alielezwa kuwa hakuwa na dalili zozote za saratani mwilini mwake.
Mwanamke huyu anakumbuka wakati wa mchakato wa matibabu, madaktari walikuwa wamemwambia kuwa huenda hangejaliweza kupata mtoto mwingine.
Njia ya kipekee ilikuwa ni kuyatoa mayai yake ya uzazi yahifadhiwe kitaalamu, na baadaye yarejeshwe.
Ila kwake, Alice wakati huo hakuwa na mawazo ya kupata mtoto mwengine au kufunga ndoa asijue kuwa baadaye angepata maisha mengine ya ndoa.
Maisha yake yaliporudisha
Mwishoni mwa mwezi Mei 2017, Alice alipoamua kusafiri kwenda nchini Marekani, kuwatembelea jamaa na marafiki zake, kwa hivyo alijipata akiwa na muda mwingi, hasa mchana wakati ambapo watu walikuwa kazini.
Pale alianza kudodosa mitandao ya kijamii, bila lengo lolote ila kukutana na watu wengine. Wakati huo alikumbuka mtandao mmoja aliokuwa ameufungua hapo awali uliohusiana na mapenzi, au wenye kuwaleta pamoja wanawake na wanaume kwa ajili ya kutafuta urafiki ambao pengine unaweza kuhitimu kuwa uhusiano wa maisha.
Alice aliufungua na akiwa katika pilikapilika za kuuchambua waliokuwa humo, alikutana na mwanaume mmoja kwa jina John.
Licha ya kuwa John asili yake ni Mzungu, Alice anasema kuwa kilichomvutia sana kwa akaunti ya John ilikuwa ni maadili yake na msimamo wake kiimani ambao uliwiana na wa kwake.
“Nilipoanza kusoma zaidi kuhusiana na John niligundua kuwa alikuwa na maadili sawia na ya kwangu,” anasema.
“Isitoshe kuwa alikuwa ameandika kuwa alikuwa tayari kuwalea watoto wa mwanamke ambaye wangependana naye, ila yeye alikuwa bado hajawahi kuoa wala kujaliwa mtoto. Hilo lilinivutia mno.”.
Haikuchukua muda kabla ya wapenzi hawa wawili kukutana. Kulingana na Alice alikutana na John kwa mara ya kwanza katika mji wa Manhattan jimbo la Kansas. Jinsi walivyoendelea kuzungumza walijikuta wakianza kupendana siku baada ya siku nyingine.
Hatimaye baada ya muda wa Alice kurudi nchini Kenya nyumbani kwa kufika yeye alirejea, ila kwa kuwa penzi lilikuwa limeanza kuota walianza uhusiano wa kimapenzi wakiwa mbali.
Mara kwa mara mmoja wao alisafiri Kenya au Marekani ili wakutane.
Miaka miwili baada ya uhusiano wao wa kimapenzi kuanza, hatimaye Alice na watoto wake watatu walihamia nchini Marekani mwaka wa 2019.
Baada ya wiki moja walifunga ndoa rasmi na kuwa mume na mke.
“Miezi miwili tu baada ya kufunga ndoa , wakati huo nikiwa na miaka 45 niligundua kuwa tayari nilikuwa na ujauzito , nilishtuka kwani tayari daktari aliwahi kuniambia kuwa nisingeweza kushika mimba tena baada ya kuugua saratani miaka ya nyuma,” Alice anakumbuka.
Alice na mume wake hawakuwa wanatarajia mtoto.
Mumewe pia akiwa na umri wa miaka 53 alikuwa hana mpango wa kuwa na mtoto, na kwa upande wa Alice alijihisi kana kwamba miaka ilikuwa imesonga mno kwa yeye kushika mimba. Kwa hivyo habari hizo ziliibua msisimko mkubwa katika nyumba yao.
Alice anataja ujauzito huo kama muujiza mkubwa katika maisha ya ndoa yao
“Sisi tulikuwa tunatarajia na tulipanga kuwa tarehe Machi 10 mwaka wa 2020 ambayo ni tarehe ya kuzaliwa kwa mume wangu, ndiyo siku ambayo mtoto angezaliwa kupitia njia ya upasuaji, ila nilijifungua mtoto wa kike siku moja baada ya tarehe niliyozaliwa. Mtoto huyu amekuwa ni baraka kubwa kwetu,” Alice anasema.
Kutokata tamaa
Alice kwa sasa huona mtoto wake aliyejaliwa na mume wake wa pili kama muujiza mkubwa kwa kuwa yeye hakutolewa mayai ya uzazi na alifanyiwa matibabu yote ya saratani.
Kwa hivi sasa Alice, mume wake na watoto wao wanne wanaishi Marekani.
Amekuwa katika mstari wa mbele kuzungumza na wanawake hasa katika mitandao ya kijamii kutokata tamaa wanapopatwa na changamoto aidha za ugonjwa, kifo au hata ya kijamii.