Saturday, March 15

Wafungwa 1,789 wa Ethiopia walioko Tanzania kurejeshwa kwao Eagan Salla

BBC Swahili, Dar es Salaam

Rais wa Ethiopia akipiga ngoma mara baada ya kuwasili mjini Chato, Tanzania ambapo alipokelewa na mwenyeji wake rais wa Tanzania.Image caption: Rais wa Ethiopia akipiga ngoma mara baada ya kuwasili mjini Chato, Tanzania ambapo alipokelewa na mwenyeji wake rais wa Tanzania.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ameridhia kuwarejesha kwao wafungwa 1789 raia wa Ethiopia waliko kwenye magereza mbalimbali nchini Tanzania wakituhumiwa kuingia nchini kinyume na sheria

Tanzania imeitaka Ethiopia kufanya taratibu za kuwarejesha nyumbani wakalitumikie na kulijenga taifa lao

Maamuzi haya yametolewa katika mazungumzo ya kuhitimisha ziara ya siku moja ya rais wa Ethiopia Sahle Zedwe ambaye aliwasilia kwenye uwanja wa ndege wa Chato na kupokelewa na mwenyeji wake rais Magufuli na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana kwa takribani saa tatu kabla ya kujitokeza tena hadharani.

Mataifa haya mawili pia yameazimia kushirikia kwenye biashara ya wanyama na mazao yatokanayo na wanyama kwani Ethiopia imepiga hatua zaidi katika sekta hiyo, hivyo Tanzania itajifunza na kuweza kunufaika katika ushirikiano huo.

Rais wa Ethiopia Salhe Zedwe alieleza kufurahi kurejea Tanzania na kwamba wamekubaliana na raisi Magufuli kuwa Kiswahili kianze kufundishwa Chuo kikuu cha Adis Ababa huko Ethiopia, Rais Zedwe anasema maneno ya kwanza ya Kiswahili aliyojifunza ni “Acha kelele mtoto amelala”

Tanzania na Ethiopia zimekuwa na mahusiano ya kihistoria na katika kudumisha uhusiano huo Ethiopia imeahidi kuipatia tena Tanzania eneo la Kujenga ubalozi wake baada ya eneo la awali kuchuliwa na serikali kutokana na kutokuendelezwa na serikali ya Tanzania.