Alikufa siku kadhaa baadaye na hatimaye baba huyo akawaweka watoto ndani ya kikapu na kutoroka mzozo ili kupata hifadhi katika nchi jirani ya Sudan Kusini.
Akiwa pamoja na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitano na shemeji yake mwenye umri wa miaka 14 , kwa sasa anaishi katika kambi ya wakimbizi , ambako daktari Mmarekani anasaidia kuwatunza watoto hao mapacha wachanga.
Mapigano ya kulidhibiti jimbo la Tigray – lililoko katika eneo la kale la ustaarabu la Aksum -yameingia mwezi wa tatu.
Wapiganaji wa Tigray People’s Liberation Front na vikosi vinavyoongozwa na jeshi la Ethiopia wanapigana kwa ajili ya kuchukua mamlaka katika jimbo hilo linalokabiliwa na mzozo na mivutano ya kikabila.
Mzozo huo umewasambaratisha watu takriban milioni mbili, huku wengine wapatao 60,000 wakikimbilia nchini Sudan.
Kila yeyote aliyekimbia ana hadithi ya kusimulia – ya jinsi walivyohisi waliposikia mlio wa bunduki kwa mara ya kwanza, jinsi walivyojificha kweye mapango huku ndege zikirusha makombora, na jinsi walivyopigwa risasi na kunyanyaswa kingono.
Wengi wanakumbuka jinsi walivyoepuka kifo na kuendelea na safari kwa siku nyingi, bila chakula na maji, ili kufika eneo salama.
Hii ni hadithi ya mwanaume mjane Abraha Kinfe:
Nina umri wa miaka 40. Mke wangu , Letai Tsegay, alikua na umri wa miaka 29. Tulioana miaka 13 iliyopita, na tulikuwa na watoto watatu.
Tulikua tunaishi eneo la mashambani karibu na mji wa Mai-Kadra magharibi mwa Tigray. Tarehe 10 Novemba, wanajeshi wa muungano waliingia katika eneo letu na kupita kwenye nyumba zetu.
Hawakututambua. Ilikua ni ahueni kubwa.
Halafu tulienda kijificha katika msitu karibu na nyumba yetu pamoja na majirani wetu wanne. Mke wangu alikuwa ana uchungu mkali wa kujifungua, lakini nilikua mwenye uoga sana kumpeleka katika kliniki katika mji wa Mai-Kadra.
Mke wangu alijifungua watoto mapacha wa kike ndani ya msitu kwa usaidizi wa mwanamke aliyekuwa amejificha pamoja nasi.
Baadae siku hiyo tulienda nyumbani. Kwa bahati mbaya na la kusikitisha Letai hakupata matibabu ya baada ya kujifungua.
Hakupata sindano ambayo ingemzuia kutokwa damu. Baada ya siku zipatazo 10, Letai alifariki dunia.
Kilikuwa kitu kilichonivunja moyo sana. Nikiwa pamoja na majirani zangu wanne tulimzika katika shamba letu.
Natamani ningelimpeleka katika kliniki, lakini wakati mambo wakati huo mambo yalikua mabaya mjini na watu walikuwa wakimbia kunusuru maisha yao .
Mji ulibakia mtupu.
Miaka mitano iliyopita, mimi na familia yangu tulikimbia kutoka mji wa Metama katika jimbo jirani la Amhara kutokana na mapigano ya kikabila.
Tulihamia eneo la Mai-Kadra kuyajenga upya maisha yetu kuanzia mwanzo. Tulipewa kipande cha ardhi na mtawala wa eneo kwa ajili ya kulima.
Katika makazi yetu mapya tulijenga nyumba ndogo kwa mbao na matope. Lilikua ni eneo zuru kwangu mimi na mke wangu.
Mtoto wetu wa kiume alizaliwa pale. Lilikuwa ni eneo ambalo mimi na mke wangu tulilifurahia. Hata watoto wangu mapacha wa kike walizaliwa pale, lakini baada ya siku 20 tuliondoka huko.
Wakati mke wangu alipokufa nilihisi dunia imeanguka . Nililia na na nikalia huku nimemshika mikononi mwangu. Nilichukia sana vita ambavyo vilituletea tabu.
Mke wangu mpendwa, mama wa watoto wangu, alikufa kwasababu hakuweza kupata matibabu ya kimsingi
Kwasababu hali ilikuwa bado ni ya kutisha, majirani zangu walikwenda Sudan. Nilibaki nyuma, na mapacha wangu, mtoto wangu wa kiume na shemeji yangu.
Tulikua tunaenda kujificha katika msitu kila mara tulipowaona wanajeshi. Ilikua ni vigumu sana kuwatunza mapacha peke yangu, bila hata majirani.
Watoto wachanga wanahitaji mama yao wa kuwanyonyesha. Niliwatunza kwa kuwapatia matone ya maji, sukari na kuweka kidole changu katika chakula kilichosagwa katika supu na kuwlisha mara kwa mara.
Baada ya takriban siku 20, nilienda katika kituo cha jeshi la shirikisho lililokua katika eneo na nikawaomba kama ninaweza kuwapeleka mapacha wangu katika kliniki mjini Humera, mji mwingine uliokuwa karibu.
Kwa bahati nzuri waliniruhusu kupita, lakini nilipita nilivuka mto Tekeze kwa boti ili kufikiaeneo la Hamdayit nchini Sudan.
Niliwapeka mapacha wangu ndani ya kikapu, na watoto wengine wawili walikua pamoja nami.
Kwa sasa tumepata hifadhi katika kambi ya Hamdayit. Daktari Mmarekani kutoka shirika la msalaba mwekundu anawatunza mapacha.
Anawapatia hudumua muhimu na kupima ukuaji wao kila baada ya siku tatu. Mungu ambariki kwa ukarimu wake na usaidizi ambao amekuwa akiutoa kwa wakimbizi wote.
Kuwabatiza mapacha
Mapacha kwa sasa wana umri wa zaidi ya miezi miwili. Ninaona wameongezeka uzito . Lakini mvulana wangu wa miaka mitano -huwa anamuulizia mama yake kila mara . Hilo huwa linanisikitisha sana. Sipendi kumdanganya kuwa siku moja tutaungana tena na mama yake.
Ninaendelea kuhangaika kukubali kuwa Letai hayupo nasi tena. Maisha kwa kweli yanaumiza. Hapa kuna mapacha wangu na ninakiri kwamba kila mara wananikumbusha mke wangu aliyefia mikononi mwangu.
Wakimbizi wenzake wananihurumia kutokana na hali yangu na wanajaribu sana kunifariji kwa kiasi fulani.
Walipendekeza niwaite mapacha wangu majina Eden [jina la bustani inayozungumziwa katika hadithi ya Biblia ], na Trefi kuamini kuwa kunusurika kwao tayari ni muujiza kutoka kwa Mungu .
Trefi lina maanisha “usitoke karibu ” jina linalotumiwa sana katika lugha ya Tigrinya inayozungumzwa sana Tigray na jimbo jirani la Eritrea.
Kwa mujibu wa utamaduni wa Wakristo wa Orthodox, watoto wachanga wa kike wanapaswa kubatizwa katika siku ya 80 baada ya kuzaliwa.
Siku hiyo inakuja, lakini hakuna huduma ya kanisa katika kambi ya wakimbizi
Bado ninahuzuni ya kufiwa na ninamuomba Mungu kwamba anipe nguvu za kuwakuza watoto wangu katika mazingira salama. Natumai mzozo huu utamalizika na tutaweza kuendeleza maisha yetu pale tulipokuwa tumefikia.