Friday, November 15

Ongezeko la utajiri wa mabilionea 10 linaweza kugharamikia chanjo ya corona ya kila mtu duniani

CHANZO CHA PICHA,AFP Maelezo ya picha, Jeff Bezos alikuwa na uwezo wa kumpatia kila mfanyakazi wake $105,000 na fedha alizojipatia tangu mwezi Machi

Utajiri wa jumla wa watu kumi matajiri zaidi duniani uliongezeka na kufikia $540bn (£400bn) wakati wa mlipuko wa virusi vya corona, kulingana na Oxfam.

Shirika hilo la hisani linasema kwamba fedha hizo zinatosha kuzuia dunia kukumbwa na ufukara kutokana na virusi hivyo na kuweza kulipa gharama ya chanjo kwa watu wote duniani.

Shirika hilo linatoa wito kwa serikali kufikiria kuwatoza kodi ya kiwango cha juu watu matajiri.

Ripoti hiyo ya Oxfam inajiri huku viongozi duniani wakikongamana katika mkutano wa kiuchumi unaofanyika mjini Davos kupitia njia ya video.

Mwezi Disemba 2020, jumla ya utajiri wa mabilionea duniani ulifikia $11.95tn – sawa na matumizi ya mataifa yote yenye uwezo mkubwa duniani G-20 kulingana na shirika hilo la hisani.

Watu 10 matajiri zaidi duniani ambao utajiri wao uliongezeka kwa $540bn tangu Mwezi Machi 2020, ni pamoja na mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos, mwenzake wa Tesla Elon Musk na mwanzilishi wa Facebook Mark Zuckerberg.

Oxfam linadai kwamba utajiri wa mabilionea hao uliongezeka kutokana na sababu ya kuongezeka kwa masoko ya hisa na “uchumi mbaya”, na kusababisha kukosekana kwa usawa wakati wa “mtikisiko wa kiuchumi katika karne hii”.

Hisa na mauzo ya Makampuni mengi ya teknoilojia yaliongezeka mwaka 2020 huku masharti ya kutotoka nje yakisababisha ongezeko la mahitaji ya hudumu za kidijitali.

Hatua hiyo iliongeza utajiri wa watu kama Bezos , ambaye utajiri wake unatokana na thamani ya kumiliki mali na hisa badala ya mishahara. Hatahivyo utajiri hauko sawa na mapato.

Makadirio ya utajiri hutokana na thamani ya mtu binafsi, pesa zao, thamani ya mali na ile ya hisa wanazomiliki.

Kupanda kwa bei ya hisa kunatokana na thamani ya kampuni kwa jumla badala ya wanahisa wenyewe.

Kuishi na umasikini

Ripoti hiyo ilisema kwamba thamani ya Bezos ilipanda sana kati ya mwezi Machi na Septemba 2020 , hali ya kwamba alikuwa na uwezo wa kuwapatia wafanyakazi wake 876,000 nyongeza ya $105,000 kila mmoja wao na bado akasalia na utajiri aliokuwa nao kabla ya mlipuko wa virusi hivyo.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Hii ni tofati na watu masikini duniani ambao kujinasua kwao kiuchumi kunaweza kuchukua zaidi ya muongo mmoja .

“Tunafikiri kwamba hii ni fursa ya kufanya mabadiliko kupitia kujinasua kupitia usawa na badala yake kufikiria kutoza kodi ya juu makampuni ili kuhakikisha kuwa kila raia anaimarika kimsingi , Danny Sriskandarajah, Afisa mkuu wa Oxfam afisa aliambia BBC, akisema kodi hiyo inaweza kuchangisha mamilioni ya fedha.