Friday, November 15

Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi akutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania JWTZ CDF Jenerali Venance Salvatory Mabeyo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania JWTZ CDF Jenerali Venance Salvatory Mabeyo (kushoto) wakati alipokuwa akizungumza nae leo alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kujitambulisha tokea kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana uliopita

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyiamelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kuendelea na kazi kubwa ya kuimarisha amani na kuilinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, aliyefika Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kumpongeza.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), limeendelea kufanya kazi kubwa ya kulinda amani nchini na kutoa pongezi maalum kwa kuisimamia amani hiyo hasa katika kipindi cha uchaguzi Mkuu uliopita.

Alisema kuwa wananchi wa Tanzania wanajivunia hatua hiyo ya Jeshi lao katika kuhakikisha wanakuwa salama wao pamoja na mali zao wakati wote na kumuhakikishia Jeneral Mabeyo kwamba Zanzibar iko salama.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba kutokana na kuwepo kwa ulinzi na usalama kumepelekea wananchi wa Zanzibar kuendelea kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo kwa amani.

Alisisitiza kwamba Zanzibar iko salamana kwa vile Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ)  lipo imara hatua hiyo imepelekea kuimarika zaidi.

“Tumeridhika kwa amani na utulivu uliopo na tunatoa shukurani kwa kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kwa kulinda mipaka yetu na kuendelea kusimamia amani na utulivu hapa nchini”,alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kushirikiana na vikosi vya ulinzi vya Zanzibar kikiwemo kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), katika suala zima la uzalishaji mali kama vile kilimo.

Alisema kuwa kwa vile shughuli zao zinakwenda sambamba kuwepo kwa mashirikiano hayo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji mali katika sekta ya kilimo hapa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba (JKT) wanauzoefu mkubwa katika shughuli hizo.

Aliongeza kuwa licha ya juhudi zinazofanyika katika uzalishaji mali lakini imeonekana bado uzalishaji ni mdogo sana hivyo mashirikiano hayo yatasaidia kufikia lengo lililokusudiwa.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi na shukurani kwa Jenerali Mabeyo pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendelea kuilinda amani na utulivu nchini pamoja na kuilinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dk. Mwinyi pia, alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa Jeshi hilo kufuatia kifo cha Brigedia Jeneral mstaafu, Emanuel Maganga aliyefariki dunia katika Hospitali ya Mirambo Manispaa ya Tabora alipokuwa akipata matibabu.Brigedia Jeneral Maganga aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma alifariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa ya Januari 22, 2021.

Nae Mkuu wa Jeshi la Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Salvatory Mabeyo kwa upande wake alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kushinda nafasi ya Urais wa Zanzibar na kueleza imani ya Jeshi hilo kutokana na utendaji wake wa kazi.

Katika maelezo yake, Jenerali Mabeyo alieleza kuwa kutokana na kumfahamu na kuutambua utendaji wa kazi wa Rais Dk. Mwinyi kwa vile aliwahi kufanya kazi nae ana matumaini makubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

 

Aidha, Jenerali Mabeyo alipongeza hatua na busara kubwa zilizotumika katika kuleta maridhiano hali ambayo itazidisha maelewano sanjari na kudumisha amani na umoja nchini.

 

Jenerali Mabeyo alitumia fursa hiyo, kutoa pongezi kwa wananchi wa Zanzibar kwa kundeleza amani, umoja na mshikamano  walionao.

 

Katika maelezo yake, Jenerali Mabeyo alimuhakikishia Rais Dk, Mwinyi kwamba (JWTZ) itaendelea kutoa ushirikiano wake  katika kuhakikisha amani inadumishwa katika maeneo yote nchini hasa ikizingatiwa kwamba yeye mwenyewe ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama.

 

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na Baba Askofu Michael Henry Hafidh ambapo katika maelezo yake alimpongeza Askofu huyo pamoja na Waumini wote wa Kanisa la Anglikana kwa kuendelea kuiombea nchi amani.

 

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alizipongeza juhudi za uongozi wa Kanisa hilo la kutaka kujenga Chuo cha Amali huko kisiwani Pemba pamoja na azma yao ya kutaka kuekeza katika eneo la Kiungani  Jijini Zanzibar.

 

Mapema Baba Askofu alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa ushindi mkubwa alioupata na kueleza matumaini makubwa waliyonayo wananchi wa Zanzibar kutokana na uongozi wake huku akimpongeza kwa kuwepo kwa maridhiano na hatimae kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar