- Anne Ngugi
- BBC Swahili
Ukimuona mwanamke huyo inawezekana ukamtazama tena kwa jinsi alivyojaza misuli kama mwanaume.
Lakini je alifanya nini kupata muonekano huo
Hili si jambo rahisi, bi. Everlyn ametumia takribani miaka tisa kupata muonekano alionao kwa sasa unaomfanya kuwa mwanamke mwenye umbo la kipekee.
Hali hii ilianza aje ?
Mwaka 2012, Everlyn alikuwa naibu meneja katika benki moja nchini Kenya , aligundua kuwa ameanza kuongezeka uzito , na kama ilivyo kwa wanawake wengi baada ya kujifungua huwa wanaongezeka mwili na hivyo huamua kuanza kufanya mazoezi.
“Niliamua kuanza mazoezi ili kupungua , nilianza kwa kwenda kwenye nyumba za mazoezi(Gym) ” Eve anaeleza.
Wakati huohuo mume wake alianza kumpa motisha kwani aliona ari na bidii aliokuwa nayo.
Muda sio mrefu alianza kuona matokeo chanya kwa mwili kupungua hivyo ikampa faraja.
Wakati akiendelea kufanya mazoezi bi. Eve alihamasika kuanza kunyanyua vyuma vinavyotengeneza misuli ya mwili wake.
Alianza kunyanyua vyuma vyenye uzito mdogo lakini kadri siku zinavyozidi kwenda akawa anabeba vyuma vyenye uzito wa juu zaidi.
Kinachostaajabisha kwa mwanamke huyu aliamua kufanya uamuzi ambao sio wa kawaida wa kuacha kazi yake benki na muda huo kutumia kufanya mazoezi ya kujenga misuli.
“Nilipata ari ya kuwasidia watu wengine hasa wanawake kupunguza uzito na kuwa na muonekano kama wangu,”anasema Eve.
Awali, Eve alikuwa mwalimu kipindi cha miaka mitano kabla ya kuanza kufanya kazi benki, ambako alifanya kazi kwa miaka kumi.
Baada ya kuacha kazi benki , maisha yalibadilika vipi?
CHANZO CHA PICHA,EVERLYN OKINYI OWALA
Eve anaeleza maisha yake mapya yanamfanya kuwa na amani na furaha.
Alianza kwa kumsaidia aliyekuwa meneja wake wa zamani ambaye alikuwa mnene.
Na kadri siku zilivyoenda alizidi kupata wateja wengi haswa wanawake.
Akiendelea na kazi ya kuwafanyisha watu mazoezi , aliingia kwenye mashindano ya unene wa misuli kwa upande wa wanawake.
Mwaka 2016 alishinda taji la mwanamke mwenye umbo zuri nchini Kenya ‘Miss Figure Kenya’ .
CHANZO CHA PICHA,EVERLYN OKINYI OWALA
Mnamo mwaka 2019 , huko nchini Afrika Kusini alishinda mataji mawili ya kimataifa ya mwanamke mwenye misuli mikubwa.
Eve anasema mataji hayo yalimpa motisha kuendeleza taaluma yake.
Changamoto za kazi
Kwa kuwa hali ya kuwa na misuli huonekana kuwa jambo la kawaida kwa wanaume , hatua yake kama mwanamke kujitokeza waziwazi inamfanya kuonekana mtu tofauti .
Changamoto nyingine ilikuwa kipindi alipoanza mashindano ya misuli, wazazi wake walikuwa na wasiwasi juu ya kazi hiyo kutokana na mavazi ambayo yanavaliwa ili kuonesha misuli
“Baada ya kushinda taji la Miss figure picha iliyochapishwa kwenye magazeti ilinionesha nikiwa nimevalia kama muogeleaji na hivyo kuonesha sehemu kubwa ya mwili wangu kuwa wazi. Baba alinipigia simu na kuniuliza iwapo siku hizi niliamua kuonesha uchi wangu kwa ulimwengu – ilinichukua muda wa miezi sita kumfafanulia kazi ninayofanya na maana ya ile picha” anakumbuka Eve.
Lakini kwa sasa Eve anasema kuwa wazazi wake wameelewa kazi anazofanya hasa katika kuimarisha afya ya binadamu.