Sunday, November 24

WAKULIMA 120 wanufaika na kilimo cha umwagiliaji.

WAKULIMA apatao 120 wa kilimo umwagiliaji cha mpunga wa bonde la Kindani Darajani Makombeni Wilaya ya Mkoani, wamerudisha imani ya kuzalisha polo 16 za mpunga katika ploti ya nusu eka, baada ya kisima wanachotumia kumwagilia kutengemezwa na kurudisha huduma ya maji kama awali.

Hayo yamebainikia wakati wa zoezi la usafishaji wa kisima na uwekaji wa mpira wa kusukumia maji wenye urefu mita 50 na huduma za umeme kwa miaka mitatu, vilivyogharimu shilingi milioni tano (5,000,000) ikwa ni utekelezaji wa ahadi za mbunge wa jimbo la Mkoani Profesa Makame Mbarawa Mnyaa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mkulima wa mpunga wa umwagiliaji katika bonde hilo, Fatma Khamis Iddi alisema kabla ya kilimo cha umwagiliaji akilima nusu eka na mavuno yakiwa sio mazuri, kwani walikua wakitegemea mvua sasa kilimo cha umwagiliaji wanavuna polo 16 hadi polo 10.

“Mategemeo yao ni kupata mavuno mengi baada ya kuwa na kilimo cha umwagiliaji maji, sasa hata kisima kikiongezwa basi mafanikio yatakua makubwa”alisema.

Naye mkulima Khalfani Said Ali alisema uzalishaji wa zao la mpunga ulishuka kutoka na maji waliyokuwa wakipata ni kidogo, na hulazimika kugawana hali ambayo kilimo hicho kilishindwa kunawiri.

Alisema kuwepo miundombinu hiyo inahitaji kukamilika, serikali na wadau mbali mbali kukamilishwa miundombinu, pamoja na kupatiwa mabomba za maji zitakazoweza kufikisha maji haraka katika mashamba yao.

“Bonde zima lina ekari 30 ni ekari 15 ndizo zinazotumiwa kwa umwagiliaji, huku zilizobakia zikihitaji nazo kuingia katika kilimo hicho”alisema.

Aidha alisema hapo zamani eka nzima akilima hata polo tatu hapati, sasa kilimo cha umwagiliaji amelazimika shamba kuligawa mara nne, kila ploti moja huvuna polo 14 hadi 16 kwa msimu mmoja huvuna mara mbili.

Sheha wa shehia ya Ng’ombeni Subira Iddi Mohd, alisema sasa kilio chao kkmeshatatuliwa cha kukosa maji, huku akitarajiwa kuvuna na kupata kilimo kikubwa zaidi.

Alisema kwa mwaka kilimo cha umwagiliaji hulima mara mbili, huku ploti moja mtu anavuna polo tano hadi sita za mpunga jambo ambalo linawapa matumaini makubwa wakulima.

Katibu Mwenezi wa CCM Jimbo la Kojani Abdalla Mohamed Abdalla, aliwataka wakulima hao kujitolea kwao katika kulinda na kuutunza mradi huo, kwani vifaa hivyo ni vyenye thamani kubwa.

Akikabidhi mpira huo katibu wa mbunge wa jimbo la Mkoani Maryam Said Khamis, alisema kilimo ni uti wa mgogo katika uchumi, hivyo aliwataka wakulima hao kuongeza bidii katika uzalishaji wa mpunga.

Alisema serikali iliyopo madarakani sio serikali ya mdomo mdomo, ni serikali ya vitu ambavyo vitu vyake vinaonekana na viongozi kutekeleza ahadi zao walizoziweka kwa wananchi.

“kiongozi wenu wa jimbo ameahidi kuufanyia matengenezo mtaro wa maji, kisiwa kitaweza kuwanufaisha wakulima wengi wa kilimo cha umwagiliaji”alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bonde la Kindani Darajani Makombeni, Nassor Hakim Haji alisema bonde hilo linatumia shehia tatu, makombeni, ng’ombeni na uweleni, huku akiwashukuru serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa kwa kujenga kisima hicho.

Aidha aliwaomba wafadhili na wadau wengine kuwasaidia mchikichi mwengine wa kusukumia maji, ambao utaweza kuwasaidia wananchi wengi zaidi kwa wakati mmoja.

Bonde wa la kilimo cha mpunga cha umwagiliaji la Kilindani Darajani lenye ukubwa wa eke 30, ikiwa 15 zinatumika kwa umwagiliaji linawakulima 120 wakiwemo  wanawake 89 ni kutoka shehia ya Makombeni, Uweleni na Ngómbeni za wilaya ya Mkoani.