Friday, November 8

Wavuvi Wilaya ya Micheweni wamuomba Mh Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi kutekeleza ahadi alizoahidi wakati wa kampeni.

NA FATMA HAMAD FAKI

Wavuvi wanaotumia bandari ya Shumba mjini Wilaya ya Micheweni  Mkoa wa Kaskazini Pemba wamemuomba  Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dr Hussein Ali Hassan Mwinyi kutekeleza ahadi alizoahidi wakati wa kampeni  juu ya  kuwawekea Boti ya uokozi  katika bandari hiyo.   

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi huko bandarini kwao shumba mjini wamesema  kutekeleza ahadi kutatoa matumaini kwa wananchi katika Nyanja mbali mbali za kimaendeleo.

Aidha wananchi hao wamesema wanamatumaini makubwa ya kupata maendeleo  katika Serikali ya awamu  ya Nane kwani imeanza kuonesha dalili njema kwa wananchi wake.

Sambamba na hayo wavuvi hao wamesema ingawa hali ya maisha bado ni ngumu lakini wamefurahishwa kwa hali ya utulivu na amani iliyopo huku wakifanya shughuli zao bila ya kubughudhiwa na mtu yoyote.

Kwa upande wake mwenyekiti wa wavuvi wa bandari  hiyo  Hussein Rashid  amemkumbusha Rais Mwinyi kuifanya bandari ya shumba mjini kuwa huru kwa wasafiri wanaotoka  bandari ya Shimoni Kenya na pamoja na kisiwa cha Pemba.

Hata hivyo amewataka wananchi wote kushirikiana kwa pamoja katika harakati za kimaendeleo bila ya kubaguana kutokana na tafauti za kisiasa

 

Nae Afisa mkuu idara ya maendeleo ya Uvuvi Pemba Sharif Muhammed Khamis amewatoa hofu  wavuvi hao na kusema kuwa muda utakaporuhusu watapatiwa wanachokihitajia.