Chama cha ACT Wazalendo kimepongeza hatua ya utiaji saini Mkataba wa Maelewano baina ya Oman na Serikali ya Umoja wa Kitaifa SUK juu ya ujenzi wa Bandari Jumuishi huko Mangapwani, Kaskazini mwa Zanzibar
Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano Kwa Umma wa Chama Cha ACT Wazalendo, Ndugu Salim Bimani amesema.”Hii ni hatua kubwa na muhimu kwa ajili ya uchumi na ukuaji wa Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk Hussein Mwinyi”.
Utiaji saini wa makubaliano hayo yaliyofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Bwana, Amour Hamil Bakari na kwa upande kwa upande wa Oman alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji cha Oman Sheikh Mohammed Al-Tooqi ambaye aliongoza ujumbe kutoka Mamlaka hiyo ya Oman. Chini ya makubaliano hayo Oman imeweka nia kujenga bandari kadhaa kama vile ya mizigo na makontena, Petroli na gesi, Uvuvi na pia kuwepo chelezo kwa ajili ya matengenezo ya meli za ndani na nje katika ukanda huu.
Pia kuweko eneo la viwanda, eneo la biashara na makaazi ya kisasa, imeelezwa na Rais Mwinyi amesema huu ni mwanzo mzuri kwa Zanzibar ” Lengo letu ni kuleta mabadiliko makubwa kwa maslahi mapana ya nchi yetu na fursa na faida kwa watu wote.”
Chama cha ACT Wazalendo kinawataka wananchi wote wasimame na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa umoja wao iki kuitia hima na shime katika kuijenga Zanzibar yetu “Kila tukishikamana ndio tutaipa nguvu Serikali ya Umoja wa Kitaifa kufanya kazi na nchi mbali mbali na makampuni mbali. Tunaamini mazingira mazuri zaidi yatandikwa kushawishi wawekezaji zaidi,” alisema Bimani
Pia Bimani aliishukuru Serikali na watu wa Oman kudhihirisha uhusiano na udugu wa kweli kwa Zanzibar kwa kuweka nia ya mradi huo utakaotoa ajira kwa maelfu.
Itakumbukwa Oman imefanya miradi kadhaa kikiwemo kilichokuwa Chuo cha Afya cha Mbweni na sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Zanzibar SUZA na pia Oman inasimamia ujenzi na uhifadhi wa Jengo la Beit Al Ajaib ambalo sehemu yake kubwa iliporomoka Disemba 25, 2020
Imetolewa na.
Salim A. Bimani
Katibu, Habari, Uenezi na Mahusiano Kwa Umma.