Sunday, November 24

DK, Mwinyi atekeleza ahadi yake Matale.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, amekabidhi vifaa kwa wanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM) tawi la matale, kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa shughuli za chama na maendeleo kwa wanaushirika.

vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni viti thamanini (80), charahani tano (5), kompyuta seti moja (1) na meza mbili (2), ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa kwa wanachama hao, wakati alipolifungua tawi hilo mwanzoni mwa mwaka huu.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa Mwenyekiti wa Chama Mkoa, kwa niaba ya Rais Dk.Hussein Mwinyi, Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba huo Mattar Zahor Massoud alisema vifaa hivyo ni mali ya chama na sio mali ya mtu binafsi, hivyo ni vyema vikatumiwa kwa lengo lililokusudiwa na wala sio vyenginenyo.

Alisema vyarahani hivyo vitawasaidia sana katika shuhuli zao za ushoni, kwani mwisho wasiku zitawaongezea kipato chao kwa lengo la kuondokana na umasikini.

“Mtarajio yetu ni kutumiwa kama ilivyokusudiwa na vyarahani hivyo sio mali ya mtu vizuri vikaheshimiwa na kutumiwa na vijana wote wanaotumia tawi hili”alisema.

Aidha aliwataka vijana hao kujiendeleza zaidi kielimu, ili kuweza kufikia malengo yao pamoja na kubuni miradi mengine ambayo itaweza kuwaongezea kipato ukiachilia ushoni uliopo sasa.

Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba Yussuf Ali Juma, aliwataka wanachama wa ccm tawi la matale kuvitunza na kuvithamini vifaa waliopatiwa.

Mwenyekiti huyo aliwasihi vijana na wanachama hao, kuzingatia na kudumisha umoja na mshikamano na kubuni mbinu za kuvitumia vizuri vifaa hivyo ili viweze kuwaletea tija.

“Vifaa hivi ni vyenu Rais ameamua kutekeleza kwa vitendo ahadi zake, sisi tuliopatiwa ni bora tukavithamini ili viweze kudumu kwa muda mrefu, tunapaswa pia kuona sisi tumepata bahati ya kipekee kuwa wa kwanza kupatiwa msaada na Rais Dk.Mwinyi”alisema.

kwa upande wake mwenyekiti wa ccm tawi la matale Ali Bakar Ali,  aliahidi kuvitunza vifaa hivyo pamoja na kuvitumia kama vilivyokusudiwa kwa maslahi ya chama, wanachama na taifa kwa ujumla.

Aidha alimshukuru Rais Dk.Mwinyi kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi yake aliyoitoa ndani ya kipindi kifupi kwake, huku akiahidi kuwachukulia hatua wanachama watakao kwenda kinyume na malengo ya vifaa hivyo.

Nao baadhi ya wanachama wa tawi hilo, walimshukuru Rais Dk.Miwnyi kwa kuwapatia vifaa hivyo, sambamba kuwataka wanachama wenzao kuwa tayari kubuni miradi mengine ya maendeleo.