Monday, November 25

“SMZ INATHAMINI MCHANGO WA VYUO VINAVYOTOA TAALUM NCHINI” MHE. HEMED

Uwepo wa waatalamu wa fani tofauti wanaofinyangwa kupitia vyuo mbali mbali nchini, ni moja ya sababu inayopelekea kupatikana kwa taifa la wasomi watakaochangia kuleta maendeleo kwenye sekta mbali mbali nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, ameyasema hayo alipofanya mazungumzo na uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, alipokutana nao ofisini kwake Vuga Zanzibar.
Mheshimiwa Hemed ameelezea faraja yake kutokana na kasi ya Taasisi hiyo ya Elimu inayokwenda sambamba na utayari wa Awamu ya Nane wa kuleta maendeleo kwa wananchi ikiwategemea Zaidi wasomi hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Pro. Shadrack Mwakalila amesema Wanafunzi na hata Wakufunzi wa Chuo hicho wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa Dakhalia.
Katika kukabiliana na tatizo hilo linalichangia kupunguza muda wa masomo Prof Mwakalila alieleza kwamba Uongozi wa Chuo hicho umeshaandaa utaratibu wa kuanza ujenzi wa Majengo ya Dakhalia itakayotoa huduma kwa wanafunzi 1,960.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar kilianza na wanafunzi 22 mwaka 2013, ambapo hadi kufikia 2020 kina jumla ya wanafunzi 1,920.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)