Tuesday, January 7

Turudi kwenye nyimbo za kuhimiza umoja, maendeleo sio ‘chinja, fyekafyeka wapinzani’

Salum Vuai

NILIVUTIWA na kauli ya Rais mpya wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi aliyoitoa muda mfupi baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa urais Oktoba 29, 2020 pale Maruhubi mjini Unguja.

Kauli hiyo ni ile ya kuwataka wanachama na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi kusherehekea ushindi kwa staha na uungwana badala ya kuwakejeli walioshindwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa maneno na nyimbo zenye kukirihisha.

“Ili sisi tuwepo na tuweze kushindanisha sera, tunawahitaji katika ushindani wa kisiasa”.

Hiyo ilikuwa kauli ya Rais Dkt. Mwinyi, akiwakumbusha wana CCM kuzingatia amani ili wasiwakwaze wengine wakati wakisherehekea.

Alisema wazi kuwa bila ya wao wapinzani, hakuwezi kuwepo kipimo kizuri cha demokrasia ya vyama vingi nchini, akisisitiza kuwa mfumo huo wa kisiasa si ugomvi na kwamba haukuja kubagua na kuwagombanisha watu.

Kiona mbali inafarajika kwa kauli hiyo iliyotoka kinywani mwa kiongozi mkuu wa nchi, akionesha wazi kutopendezwa kwake na namna watu wengine walivyoupokea mfumo wa siasa za vyama vingi, wakiuhusisha na chuki na uhasama kati ya raia wa nchi moja.

Kwa muktadha huo, nimepata fikra ya kutoa maoni yangu ili kukazia kauli hiyo kwa kushauri mambo kadhaa kwa lengo la kutaka Wazanzibari warudi katika uasili wao wa kupendana, kuishi kwa umoja na mshikamano.

Ni vyema tusiwe watumwa wa siasa bali tuitumie kutuunganisha badala ya kutugawa ili tusije kuwaachia watoto, wajukuu na virembwe vyetu nchi iliyokatika vipande vipande, kwani washindi na walioshindwa wote ni Wazanzibari na ndugu tangu enzi na dahari.

Ninajifunza katika nchi za magharibi ambazo ndiko kulikoanza siasa za vyama vingi tulizokopia katika miaka ya 1990, kwamba siasa hizo si jukwaa la kupandikiza chuki na kujengeana uadui kati ya watu wa nchi moja hata kufika kupambana na kuumizana.

Kubwa wanachoangalia ni mawazo yenye tija kwa mataifa na wananchi wao hata kama yatatoka katika chama kisichokuwa madarakani.

Hapa ndipo ninapoona umuhimu wa kauli ya ‘Nchi kwanza chama baadae’, kwani vyama huzaliwa na kufa, huja na kuondoka lakini nchi zitabaki kuwepo hadi parapanda la kiyama litakapopulizwa.

Hii inanikumbusha miaka ya nyuma pale wasanii wetu wa aina mbalimbali za muziki wakiwemo wa ngoma za asili ambao utunzi wa nyimbo na sanaa zao ulijikita katika kupeleka ujumbe wenye manufaa kwa nchi na wananchi.

Nyimbo zao zilihimiza shughuli za maendeleo, kama vile elimu, kujenga afya kwa kula chakula bora, kilimo bora, uendeshaji mzuri wa gari ili kuepuka ajali za barabarani na mfano wa hayo.

Kwa bahati mbaya sana, ujio wa siasa za vyama vingi umewasahaulisha Watanzania utunzi wa nyimbo kama hizo na sasa wamejikita kwenye sanaa zinazopanda mbegu mbaya kwao na kwa kizazi kijacho.

Ashakum si matusi, sitakosea nikisema kuwa nyimbo nyingi za sasa hasa zinazotungwa na kuimbwa nyakati za uchaguzi zimejaa maudhui yanayowagawa wananchi badala ya kuwaleta pamoja.

Utasikia mistari ya nyimbo hizo isemayo: “Wapinzani tuwapige, tuwafyekefyeke, tuwachinjeeee”, “Wapinzani tupa kule, kanyaga kanyaga” na mengi kama hayo ambayo kwa maoni ya Kiona mbali, hayaleti afya kwa demokrasia tuliyopania kuijenga nchini.

Kwa kukariri maneno ya Mheshimiwa Rais, ni rai ya Kiona mbali kwamba sasa umefika wakati wa kuachana na utunzi wa aina hiyo na badala yake wasanii warudi katika tungo zinazohimiza uzalendo na mapenzi baina yao bila kujali tafauti zao za kiitikadi.

Hivi  karibuni kumekua na   juhudi kubwa zinazofanywa na viongozi wa juu  serikalini ,na vyama vya  kisiasa kufanya siasa  za kiungwana zinasoshajiisha amani , mshikamano na  maridhiano . Wanaharakati na asasi za kiraia kama vile Jumuia ya Waandishi wa Habari wa Pemba  – Pemba Press Club kwa kushirikiana na Shirika la Internews  Tanzania  kuwafunza waadishi  wa habari juu ya kuandika habari zanye maudhuwi  haya .Kampeni hii imefana sana kwani vyombo vya habari na waandishi wa habari  wenyewe wana nafasi kubwa  ya kuelimisha jamii  juu ya haja  ya kuwepo kwa maridhiano ya kitaifa  yatakayodumisha  umoja , mshikamano  na macaw ya kuvumiliana . Hii itasaidia sana muleta utulivu  wa kisiasa  na kuwafanya wananchi  wawe na wazo moja tu  la pujenga chi .

Sasa za vyama vingi liwe jukwaa la kushindana kwa sera bora na kwa namna inayofaa ambapo baada ya uchaguzi kila mtu atatoka amefurahi, tukipongezana na kuiombea nchi kheri na amani endelevu.

Simu: 0777 865050/0714 425556

Baruapepe: salumss@yahoo.co.uk