Tuesday, January 7

Ujue mchezo wa Ng’ombe.

‘’Kajayo,Kajayo,Simba mle Nyama,ukitamla nyama Ukamle Nyama.

Nangwe ,nangwe, twende mbio utakuja kwenye nangwe.

Hoya ,hoya,wee   huyo ng’ombe’’.

 

Hizo ni miongoni mwa nyimbo ambazo ni maalum kutokana na mchezo wa ng’ombe ambazo  uimbwa   na kufatiwa na zumari kwa ajili ya kivutio zaidi ,ikiwa ni miongoni mwa  vitu ambavyo huwapatia hamasa wananchi ama watazamaji wanaofika kwenye eneo lenye mchezo huo.

Pia nyimbo hizo zinapoimbwa ikifuatiwa na sauti ya zumari basi hata Ng’ombe wenyewe hua na hamu kubwa na kuhamasika zaidi  kua mkali kupitiliza ,wachezaji pia hupata hamu ya kucheza mchezo huo wakati  ng’ombe anapoingia tu katikati ya uwanja   aliotayarishiwa kwa ajili ya  mchezo wake.

Mchezo wa  Ng’ombe  katika Kisiwa cha Pemba  ndio asili yake na hadi leo mchezo huo unachezwa ,iwe siku za kawaida na hata kwa siku za herehe kama siku za Skukuu,sherehe za Serikali ,kipindi cha mavuno ya Kilimo cha mpunga , pia mchezo huo  umaarufu wake upo katika  Kijiji cha Chwale (Madenjani)Wilaya ya Wete Mkoa Kaskazini Pemba.

Mchezo wa Ng’ombe ni miongoni mwa michezo  maarufu  inayochezwa ambayo ni ya kihistoria Kisiwani Pemba , hususan Mkoa wa Kaskazini, mchezo huu  hadi leo hii bado haujapoteza  uhalisia wake,ni tofauti na michezo mengine inayofahamika ,huo mchezo ni mzuri na wenye kuvutia zaidi kiutalii.

Kihistoria hasa ya Mchezo wa Ngo’ombe katika Kisiwa cha Pemba kutokana na maelezo ambayo mwandishi wa Makala hii ameyapata ni kuwa ,unatokana ama uliletwa na wageni ambao ni Wareno .

Wareno hao walitawala katika Visiwa hivi kwa muda mkubwa hadi pale Utawala huo ulipoondolewa na utawala wa Kiarabu.

Mchezo huo kwa Pemba yalikuwepo baadhi ya maeneo ambayo wananchi  wa maeneo hayo walikua wakicheza ,kama vile eneo la Kijiji cha Chwale ,Shengejuu,na Kambini  kwa Wilaya ya Wete,Pujini Wilaya ya Chake Chake,Wingwi  ,Tumbe kwa Wilaya ya Micheweni .

Wakati wa karne hizo walikuwpo ng’ombe maaruf ambao hao ni kwa ajili ya kuchezwa kwenye mchezo huo,ambao wakijulikana kwa majina maarufu kama vile Kipole,Kijiba,Sanda mkobani,pamoja jina jengine ni Kitamu  huonjwa.

‘’Hayo ndio miongoni mwa majina ambayo yalikuwa yakitumiliwa kuitwa baadhi ya ng’ombe waliotayarishwa kwa ajili ya kuchezwa kwa siku ya mchezo wenyewe ,na ilikuwa kila ng’ombe analijua jina lake .

Kwa mujibu wa maelezo yaliyopatikanakwa baadhiya wazee  ni kuwa  ng’ombe hao  wanapoitwa    majina hujifahamu   na kuanza  kuingia kwenye uwanja    uliotayarishwa ambao  umejaa watu kwa ajili ya kuangalia nani mkali miongoni mwa ng’ombe waliotayarishwa kwa mchezo’’,.

Katika matayarisho ya mchezo huo kwakweli hauna matayarisho makubwa kiivyo , bali nikutafutwa   eneo  maalum  ambalo litakuwa  kubwa lenye upana ambao watu atakaa kwa kujinafasi  wakiwa watu wazima na hata watoto ,wakiume na wakike.

Ilielezwa kuwa ambapo   mtu atapata sehemu ya kukimbia mara tu ng’ombe  anapoonekana kuanza   kukasirika  ili wapate  kukimbia kwenye  eneo jengine la usalama zaidi  amabapo  uwanja  huo huonekana  kujaa  watu .

Mara nyingi uwanja wa mchezo huo ni lazima kuwa mkubwa kwani   ng’ombe anapoanza kukasirika  inakua ni matatizo hasa kwa watoto wadogo pamoja wazee wasiojiweza  ,hivyo uwanja huo unakua mkubwa ili watu wapate  kukimbia kwa uarahisi.

‘’Hiyo inakua ni sehemu tosha ya  kukimbia  na  watoto wao, ili wasijewakazurika ,kwani hukasirika vibaya mno kufikia hata kuuwa mtu wakati mwengine ama kuweza kumsababishia maumivu makali mtu aliepo nje ya uwanja ama hata yule ambae yupo katikati ya uwanja ambae amekodiwa kwa ajili ya kumcheza.

Mchezo huo hutafutwa wachezaji maalum ambao ni maarufu wanajua jinsi ya kucheza mchezo huo bila kupata matatizo yoyote yatokanayo na ng’ombe huyo    pia hutafuta ng’ombe maalum wenye vigenzo vinavyotakiwa kwa ajili ya mchezo huo.

Ilielezwa kuwa  ng’ombe anaehitajika katika mchezo huo asiwe mkubwa kupitiliza,anakuwa wa kiasi   asiwe  amechoka amekonda  ,awe anakula vizuri anashiba,pia awe mkali  mwenye uzoefu uyo ndio ng’ombe anaependeza katika mchezo.

Makala hii pia ilieleza kuwa ng’ombe akiwa ni mkali anapiga ndio mchezo wenyewe unaponoga ,watu kufurahi ,lakini ikiwa ng’ombe alofikishwa kwenye mchezo yupo lezi lezi amelegea hata akiitwa anakua hana hisia yoyote ,anakua hana nguvu mwilini za kukimbia inakua ni kazi bure mara nyingi mchezo huo haunogi kama ilivyokawaida yake.

Mwandishi wa nakala hii alielezwa kuwa katika enzi hizo za zama za kale ,mchezo wa ng’ombe unaelezewa kuwa ulikuwa ukichezwa kwa mashindano yani watu walikuwa wakishindanisha ng’ombe  kwa  ng’ombe kutoka sehemu moja na nyengine,licha ya hivyo mchezo huo mara nyingi hutumiwa kuchezwa kwa ushirikina na hata wachezaji wake walikua ni watu maarufu kwa mchezo huo.

Kabla ya mchezo huo kuanza ni lazima ng’ombe atafutwe ,ngombe   mwenye kuweza  kuhimili  vishindo  vya mchezo wenyewe kwani ni mgumu sana unavishindo vizito,baade tena lazima awekwe na njaa  hadi siku yakumalizika kwa mchezo,pia  sehemu   anayokaa ni maalum sehemu ambayo sio  rahisi kwa watu kufika kila mara ,ambapo hapo hutolewa kamba yake ya awali na bada yake kufungwa kamba maalum ambayo ni tofauti na kamba ambayo amezoea .

Kamba hiyo inakuwa ipo tofauti saa na kamba ambayo meizoea   mabayo anachungiwa nayo  ,na hivyo badala ya kamba hiyo kuwekwa kwenye pua basi huwekwa kwenye mguu nayo hujilikana  kama   ngoweyo,kama hiyo hufungwa katika mguu kwa lengo watu wapate kumvuta vizuri ili asijekudhuru watu.

Haya yote wasomaji wangu ambayo mumeyaona hapo juu mwandishi wa nakala hii hakusema yeye kama yeye kimatakwa yake bali alihakikisha anafika kwa hao walngwa wanoujua mchuzo huu,na miongoni mwa hao waliofikwa  ni pamoja mzee mmoja wa miaka (70)Mussa Hmad Bakari mkaazi wa Kijiji  hicho,na kueleza kama ambavyo alipata kuuona mchezo huo.

Alisema kuwa katika ufahamu wake mzee mussa alifahamu akiwa bado mdogo kabisa akiwa na umri   wa miaka (15)ambapo alijikuta nay eye kuanza kujiingiza kucheza mchezo huo,kwa kufuata wakubwa wake ambao walikuwa tayari wameshauzoea.

Alisema kuwa  mchezo huo uliingia Kisiwani humo tangu enzi na enzi za babu wa mababu zao,na ulikuwa ukichezwa  na watu kutoka kila pande ya Kijiji hicho na nje ya Kijiji  hicho,wageni pia walikuwa wakifika kwenye mchezo huo kuona jinsi ulivyo ,unavyochezwa  na hata kujua unahamasisha vipi jamii ,ambao ulikua unaoneka kuwa ni kivutio kikuu kwa wageni wanaofika Pemba na Zanzibar kwa ujumla.

‘’Mchezo huu ninaokusimulia jinsi nilivyoufahamu  ulikuwa ukihezwakatika vijiji mbali mbali vivyo ambavyo nimekutajia hapo juu,lakini pia yapo maeneo mengine yalikuwa maarufu ya mchezo huo ,Mtambwe,Kojani,Mchagamdogo,pamoja na Kijiji cha Kambini,lakini kwa sasa mchezo huo kuonekana kupotea kabisa kwa baadhi ya Vijiji hivyo na mwisho wake umebaki asili yake katika Kijiji hicho  tu na ndio hadi leo mchezo huo unaendelezwa’’,alifahamisha  mzee huyo.

Alisema baada ya kuonekana kwa baadhi ya Vijiji kupotea kabisa  mchezo huo  kwa sababu zisizoepukiaka ,lakini kulikuwa na ushirikina mkubwa hadi  leo  kati  ya Vijiji hivyo na Kijiji hicho cha Chwale ,ambapo watu walifanya juhudi za kujiingiza tena katika katika kucheza mchezo huo kutokana na sili yake ya Kizanzibari.

Alisema kuwa kutokana na changamoto hizo kwa Vijiji vyengine ndipo wananchi wa Kijiji cha Chwale walipoamua kukaa na wenzao kutoka katika Vijiji vyengine vya  karibu zaidi viliamua kuendeleza na kuimarisha zaidi ,ili uweze kubaki katika asili yake ,ingawaje hali ya kimaisha inarejesha nyuma juhui hizo.

‘’Katika enzi zao  mchezo huo ulikuwa unachezeshwa bure bila ya malipo yoyote kwa wenyeji na hata kwa wageni ambao hufika katika eneo hilo kuangalia mchezo huo,lakini chakusikitisha sasa hivi mchezo huu umeonekana kuwa kibiashara zaidi  na kujipatia maslahi katika maisha yao kwa hawa Vijana ambao wananchezesha mchezo huu kwa karne tulionayo sasa’’,alisema.

Alifahamisha kuwa mchezo huo haukuwa unachezwa tu ovyo ovyo ,bali ulikuwa unachezeshwa kwa siku maalum,kati ya jumamosi  na jumatano  tena majira ya saa 10:00 jioni sio asubuhi wala mchana ,na mwisho wa mchezo huo inakuwa saa  kumi na mbili za jioni 12:00 ,muda ambao ulikuwa unatoa fursa kwa wageni  waliotoka katika sehemu mbali mbali kupata muda wa kurejea walikotoka.

Kwa upande wake mzee  wa miaka (55)Said Hamad Said alisema kuwa ufahamu wake  kuhusu mchezo huo alikuja akaukuta tayari huo mchezo ushakua maarufu sana ndani ya Kijiji hicho na wapo baahi ya watu tayari wameshakua wazee hata kutembea hawawezi tena wanatembelea mkongojo ambao wazee hao walikuwa maarufu  miongoni mwa wachezaji wa mchezo huo.

Alisema yeye kama yeye kipindi hicho yupo mdogo akiwa na miaka (10) wakati anasoma darasa la nne katika Skuli ya Shengejuu  iliyomo  ndani ya Wilaya ya Wete ,alijikuta kuanza kufata fata watu  kila wanapokwenda  katika  shuhuli  hizo  za mchezo wa ng’ombe   hadi kufikia darasa la saba  alianza kuachana nao kwa vile alikuwa tayari ni muda wakushuhulikia msomo tu,licha yakuwa alikuwa anupenda sana mchezo huo kutokana na  ulivyo.

Alisema kuwa mchezo huo kabla haujachezeshwa kulikuwa na matayrisho yake kwanza hutayarishwa ili mazingira yake yawe katika hali ya kuvutia yenye kupendeza   kwa wageni na hata kwa wenyeji wa mchezo huo,matayarisho yenyewe kwa mchezo huo ni kama vile kutafutwa ng’ombe zaidi ya mmoja,ambao ng’ombe hao walikuwa wakipatikana kwa kukodishwa ,kwa kazi hiyo tu na bei yake ni kufikia shilingi 30,000 kwa kila ng’ombe mmoja katika enzi hizo  za mababu .

‘’Yapo matayarisho mengine ambayo ni pamoja na ujenzi wa sehemu maalumu  itakayo wafanya watu kukaa wakiwa na amani bila woga wowote na kuhakikisha kwamba hakuna athari zozote zinazoweza kuwapata zitokanazo na wanyama huo wakati wamchezo huo hadi kumalizika,pia kujengwa jengo mfano wa duara kwa ajili ya kuwahifadhia wanyama hao kwa muda wa masaa tisa hadi pale watakapo maliza mchezo wao ,alisema.

Pia watu huharamika kwa kujenga jengo la kukaa wageni maalum  ambalo kwa   huitwa ( dungu)   husimamisha vigogo vya miti   vya mnazi  nane  kuchimbwa mashimo  kila mstari ,hapo husimamishwa  yakiwa madhubuti  ,baadae kunakuwepo na miti mengine mirefu  ikiwa ya mkandaa   hufungwa kamba na vile vigogo kwa  mujibu wenyewe wanvyofahamu ,ilimradi tu kuwa madhubuti .

Baadae tena kuweka miti midogo midogo ya kupanga mwanzo hadi mwisho  kuhakikisha mtu haanguki wala anapo kaa kitako makalio yake hayaonekani zinakuwa zipo sawa , inakua mfano wa dari  ya nyumba ya  miti ndivyo inavyokuwa .

Mzee huyo alimalizia kuhadithia nakala hii kwa kusemakuwa baada ya kukamilisha taratibu zote hizo ,ndipo sheha wa Kijiji hicho kuanza kupiga upatu kuwajulisha watu nini kitakuwepo kwa siku  inayofata ,pia mzee huyo kuwataka wananchi pamoja na wadau wengine kuhakikisha michezo kama hiyo ya kihistoria wanaitunza na kuona kwamba inabakia katika historia yake kwa faida ya Serikali katika kutangaza utalii na hata kwa Jamii kwa ujumla katika kuwaletea maendelao.