Monday, November 25

MTU mmoja amefariki dunia baada ya chombo Chake kupindukia na kuzama baharini .

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MTU mmoja amefariki dunia baada ya chombo Chake kupindukia na kuzama huko katika bahari ya Makangale Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Akithibisha kufariki kwa kijana huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Sadi Khamis alimtaja aliyefariki kuwa ni Juma Ali Saleh mkaazi wa Kinazini Makangale Wilaya ya Micheweni.

Alifahamisha kuwa tukio hilo lilitokea hapo jana majira ya saa 8:30 za mchana ambapo marehemu alikuwa akisafirisha mwani kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyengine na hivyo chombo alichukuwa akitumia kupindukia na hatimae kuzama.

“Ni kweli Kuna mmoja alikuwa akitambulika kwa jina la mkaazi alipatwa na mauti wakati alipokuwa akijaribu kusafirisha mwani kutoka sehemu moja kwenda sehemu kwa kutumia dau kupinduka na kuzama,”alifahamisha Kamanda Sadi.

Hata hivyo baada ya mashirikiano makubwa kutoka kwa wananchi waliokuwa karibu na tukio hilo waliweza kufanikiwa kuupata mwili wa marehemu huyo majira ya saa 10:00 za jioni.

“Mwili wa marehemu uliweza kupatikana saa 10:00 za jioni na baada ya kufanyiwa vipimo vyote mwili ulikabidhiwa kwa jamaa zake kwa ajili ya mazishi.

Kamanda Sadi aliwataka wananchi kuwa waangalifu sana wakati wanapokuwa katika harakati zao za kujitafutia riziki mahali popote pale.

Aidha aliwataka wananchi hasa wale wanaotumia vyombo vya baharini kutoenda katika shughuli zao mtu mmoja mmoja na badalayake wawe kuanzia wawili ili litakapotokezea tatizo waweze kusaidiana.

“Ni vyema tuwe waangalifu sana na tunapokwenda katika harakati zetu za kutafuta riziki hasa kwa wale ambao wanatumia bahari ni vizuri tuwe kuanzia wawili na kuendelea ili litakapotokezea tatizo lolote lile tuweze kusaidiana,”alisema Kamanda Sadi.