NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WAKULIMA wa mboga, matunda na viungo Wambaa Wilaya ya Mkoani wamesema, kwa sasa wanatarajia kunufaika zaidi na kilimo chao iwapo mradi wa Viungo Zanzibar utachukua hatua ya kuwatatulia changamoto zinazowakabili.
Walisema kuwa, matumaini yao ni kuona kwamba changamoto zinazorejesha maendeleo ya kilimo chao yanapatiwa ufumbuzi, hali ambayo itawasaidia kuzalisha mazao bora.
Wakizungumza mara baada ya kusajiliwa na mradi huo walisema, kupitia mradi huo wanataka waone mabadiliko ya vitendo, ili waweze kunufaika wao na vizazi vijavyo.
“Kwa sasa tunakabiliwa na matatizo mengi, mazao yetu yanaharibika wala hatujui cha kufanya, hivyo kupitia mradi huu tunaamini tutafaidika”, alieleza.
Mmoja wa wakulima hao Haji Juma Haji alisema, anatumai mradi huo utawasaidia vitendea kazi mbali mbali pamoja na mafunzo, ili kupata utaalamu zaidi wa kuzalisha.
“Shamba langu lina ekari moja, nalima kilimo endelevu na kisichotumia mbolea za kemikali, katika shamba langu nazalisha ndimu, malimau, maparachichi, pashen na mananasi”, alisema.
Aliwaomba wasimamizi wa mradi huo kuwasaidia maji kwenye mashamba yao, kwani kuna baadhi ya mazao hufa kutokana na kukosa huduma hiyo.
Kwa upande wake mkulima wa matunda na mboga Ali Abdi Mohamed alisema, kwa mfumo waliokuja nao wana mradi hao wanategemea kupata mafanikio makubwa ya kuoengeza kipato iwapo watasaidiwa yale ambayo wameyaahidi.
“Kuna wengi huja kama hawa ila hatufaidiki chochote, lakini kama kweli watatusaidia pembejeo na kutupatia elimu tutavuna zaidi ya kile tunachokivuna sasa”, alisema.
Alieleza kuwa, mradi huo ameupokea kwa furaha kutokana na kile walichokieleza wenyewe na kuwaomba wasirudi nyuma katika kutekeleza kile ambacho wamekisema.
Nae mkulima Aze Mbarouk Juma mkaazi wa Wambaa kwa Azani aliema, anategemea maendeleo zaidi katika kilimo chake ikiwa atapata usaidizi wa mradi, kwani watapata mbegu za kisasa, dawa, mbolea na vitendea kazi.
“Tunalima sana lakini mazao yetu yanaathirika kwa wadudu na kukosa mbolea, hivyo tukisaidiwa mambo haya tutafanikiwa, nalima kilimo mseto cha migomba, mihogo, minanasi, mpunga, kunde na njugu mawe”, alisema.
Alieleza kuwa, changamoto inayowakabili wakulima hasa wanawake ni kulima kwenye mashamba ya kuazima hali ambayo inawarudisha nyuma kwani mwenyewe anapoona unapata mafanikio tu hukwambia analitaka.
Aliwaomba wahusika wa mradi kuwatafutia maeneo ya Serikali kwa ajili ya kilimo, ili wawe na uhakiki wa chakula cha kila siku pamoja na kujipatia kipato.
Mkukulima Hawa Hamza Kaleje alisema, msimu ulopita alilima mpunga ingawa hakupata hata kipolo kimoja kutokana na kuingiwa na maradhi, hivyo mradi uwasaidie mbegu na mbolea ili wapate mavuno mengi.
Mtaalamu wa Miundo mbinu katika mradi huo Amour Juma Mohamed alisema, zoezi la usajili kwa wanufaika linaendelea vizuri ambapo baada ya kumalizika wanatarajia kukutana nao tena kwa ajli ya utafiti wa mahitaji, ili hatimae waweze kuingia katika utekelezaji wa mradi.
“Dhamira hasa ni kuweza kuondoa vikwazo ambavyo vinawakabili wakulima hawa katika uzalishaji wa mazao ya viungo, hivyo watarajie elimu na nyenzo kama mbegu, miche ya miti na matunda na pia baadhi yao watapewa miundombinu ya umwagiliaji maji pamoja na zana zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji”, alisema.
Nae Meneja wa mradi Pemba Sharif Maalim Hamad alisema, kuna muitikio mzuri wa wananchi katika usajili huo, ingawa kwa upande wao walikabiliwa na changamoto ya ujazaji wa fomu kwa hatua ya mwanzo na kufahamisha kuwa, kila wanapoendelea wanazidi kujifunza.
Mradi wa Viungo Zanzibar kwa upande wa Pemba, unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA), Jumuiya ya Uhifadhi wa Misitu Asili Pemba (CFP) na shirika la PDR la Dar-es-Salaam, umeanza kuwasajili wakulima katika shehia mbali mbali za Wilaya ya Mkoani.