Monday, November 25

Watatu wakamwatwa, wawili watafutwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za ulawiti.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba linaendelea kuwatafuta vijana wawili wakaazi wa Michakaeni shehia ya Msingini Chake Chake kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa kiume mwenye miaka saba (7).

Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Kusini Pemba Richard Tadei Mchomvu alisema kuwa, baada ya Jeshi hilo kupokea taarifa kutoka kwa mama mzazi wa mtoto huyo, walianza kufanya upelelezi na kufanikiwa kuwakamata vijana watatu kati ya watano wanaoshutumiwa.

Alisema kuwa, sasa wanaendelea kuwatafuta vijana wawili waliobakia na baada ya uchunguzi kukamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kamishna huyo alisema, bado jamii haijajua umuhimu wa kumuheshimu mtoto na kusababisha vitendo hivyo kuongezeka siku hadi siku.

“Matukio ya udhalilishaji yamekuwa yakongezeaka siku hadi siku kutokana na jamii bado haijaelewa umuhimu wa mtoto, hivyo ni vyema elimu ikatolewa ili kuhakikisha mtoto anaheshimiwa na kuachwa salama”, alisema kamanda huyo.

Alieleza kuwa, Jeshi la Polisi halitomvumilia mtu yeyote atakaefanya uhalifu katika mkoa huo ikiwemo wanaowadhalilisha watoto na atakaebainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mapema mama mzazi wa mtoto huyo alisema kuwa, alimgundua mwanawe amedhoofika hali ya mwili, ingawa alikuwa anakula kama kawaida yake.

Alisema kuwa, hali hiyo ilikuwa ikiendelea kila siku zinaposonga mbele, ambapo alihisi huenda mwanawe anasumbuliwa na ugonjwa wowote.

“Nilikuwa namuuliza unaumwa na nini, ananijibu haumwi na chochote na ndipo nilipoondoa shaka ya kuwa mwanangu anaumwa”, alisema mama huyo.

Alieleza kuwa, siku ya Januari 12 usiku alimuona mwanwe hali imezidi kuwa mbaya na kufikia kukaa upande huku akijiegemeza mito, hali ambyo ilimtia wasiwasi mkubwa.

Alifahamisha kuwa, alimuuliza kwa mara nyengine kitu kinachomsumbua mpaka kufikia kukaa kitako upande upande, ambapo alimuelezea kwamba kuna vijana wanamfanyia kitendo cha ulawiti.

“Nilishtuka sana, nikamchukua hadi chumbani nikamvua suruali kumuangalia, tayari alikua wazi unamuona hadi ndani”, alisema mama huyo.

Alisema kuwa, alimchukua na kumpeleka kwa jirani yake wa karibu na kumuelezea ile hali iliyomtokea mwanawe ambayo hakupaswa kutendewa hivyo.

“Tulimuangalia tena, jirani yangu alimwambia asukume pumzi ambapo alitoka haja kubwa ikiwa na mafunza, kwa kweli nimeumia sana”, alisema.

Mama huyo alieleza, siku ya pili walimpeleka kituo cha mkono kwa mkono Chake Chake na kisha kwenda kufungua kesi kituo cha Polisi.

Mama huyo alieleza, ilimuuma sana kuona majirani zake wanamkebehi na kusema kuwa watoto wao hawewezi kufungwa kutokana na kuwa askari mpelelezi kwamba hakuona chochote alichokitaja mtoto kwa ajili ya ushahidi.

“Hivi sasa nishaanza kutengwa, kununiwa kwa sababu nimekwenda kuwashitaki watoto wao na ukizingatia wanne wana miaka kuanzia 20 na mmoja tu ndie mwenye miaka 16”, alifahamisha.

Alisema, kilichomuumiza zaidi ni kwamba siku aliyoambiwa ashirikiane na askari mpelezi katika kuwakamata watuhumiwa, aliporudi alimkuta mwanawe tayari ameshafanyiwa tena kitendo cha ulawiti.

Nae Diwani wa wadi ya Tibirinzi jimbo la Chake Chake Fatma Juma Khamis alisema kuwa alikuja mama mzazi wa mtoto huyo kumueleza kadhia iliyomkumba, ambapo alimpa ushauri na kumtaka asirudi nyuma akimbilie kwenye vyombo vya sheria kuripoti.

Diwani huyo alivishauri vyombo husika kusimamia ipasavyo kesi za udhalilishaji wa watoto, ili wanaofanya vitendo hivyo wapatiwe hatia.

Kwa upande wake Mwanaharakati wa kupambana na vitendo vya katili na udhalilishaji kutoka jumuiya ya TUJIPE Pemba Tatu Abdalla Mselemu alieleza, watahakikisha wanafatilia hatua kwa hatua juu ya suala hilo ili kuona haki inapatikana kwa mtoto.

Alifahamisha kuwa, pamoja na mama mzazi kuwataja watuhumiwa watano wanaodaiwa kumlawiti mtoto huyo lakini wana wasiwasi ya kuwa inawezekana ni zaidi ya hao, hivyo uchunguzi zaidi unahitajika kuhakikisha matukio hayo yanakomeshwa.

Nae Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Pemba, Fat-hiya Mussa Said alisema, tukio hilo alilipokea kwa masikitiko makubwa kutoka kwa mama huyo alipokwenda kuripoti katika ofisi hiyo na kueleza kwamba hatua za haraka zinahitaji zichukuliwe.