NA ZUHURA JUMA, PEMBA
JUMLA ya kesi 285 za udhalilishaji zimefikishwa kituo cha Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba kuanzia mwaka 2019 hadi Januari mwaka huu.
Kati ya kesi hizo, mwaka 2019 ziliripotiwa kesi 157, mwaka 2020 ziliripotiwa kesi 124 na mwezi Januari mwaka huu ni kesi nne (4).
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Juma Sadi Khamis alisema kuwa, kwa mwaka 2019 na mwaka 2020 kesi za kubaka ni 144, kujaribu kubaka ni nne, kutorosha 61, kulawiti 30, shambulio la aibu 37 na kumuingilia punguani tano.
Alisema kuwa, kwa mwaka 2020 pekee kesi zilizopelekwa mahakamani ni 12, zilizopata hatia mbili (2), zilizopo kwa mkurugenzi wa mashitaka tisa (9), kwa mkemia moja (1), zinazofanyiwa upelelezi 77 na zilizofungwa Polisi 19.
“Kuna kesi ambazo zimefungwa kituo cha Polisi, hii ni kutokana na kukosa ushirikiano wa kutoa ushahidi kwa watendewa wa makosa hayo, jambo ambalo tunashindwa kupeleka majalada mahakamani”, alisema Kamanda huyo.
Alieleza kuwa, sasa wamejipanga kuwachukulia hatua wale wote wanaozuia kesi hizo kwenda kwenye vyombo vya sheria, kwani wanasababisha kuongezeka kwa matukio hayo siku hadi siku kutokana na kuwafichia wahalifu.
“Sasa tumejipanga vya kutosha kwa yeyote atakaezuia ama kwa kumuoza mtoto mume au kukataa kutoa mashirikiano katika kupata ushahidi na yeye atakuwa mtuhumiwa, hatutokubali kuyafunga majalada, kwa sababu huwa wanajua ukweli ila wanaficha”, alisema.
Alifahamisha kuwa, kesi za udhalilishaji zimepungua kidogo mwaka 2020 ukilinganisha na mwaka 2019, hiyo ni kutokana na watu kuelimika katika jamii.
“Tunashkuru watu wameelimika tofauti na zamani, hivyo tuna imani yatapungua, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake atimize wajibu wake kuhakikisha tunapiga vita”, alisema Kamanda huyo.
Alieleza kuwa, matukio ya uhalifu kiujumla katika mkoa wa Kaskazini Pemba sio ya kushtua ingawa kwa upande wa kesi za udhalilishaji unatia huzuni na kusikitisha, kwani kwa mwezi wa Januari tayari wameshapokea kesi nne (4).
Kamanda Sadi aliwataka wazazi pamoja na walimu kushirikiana pamoja katika malezi ya watoto, ili wawe na maadili mema yatakayowafanya kuwa watoto wenye heshima katika jamii.