Monday, November 25

Mwanafunzi miaka 14 abebeshwa ujauzito.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MTOTO wa miaka 14 akutikana na ujauzito wa miezi minne katika Shehia ya Kengeja Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.

Mtoto huyo anesoma kidato cha kwanza kwa sasa, alipata ujauzito mwaka 2020 akiwa darasa la sita.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi shangazi wa mtoto alisema, Oktoba 26 mwaka jana alimchukua mtoto huyo kwa shangazi yake mwengine alipokuwa akiishi na kumpeleka kwake.

Alisema, baada ya kumaliza uchaguzi mkuu wa Zanzibar alikwenda baba wa mtoto huyo na kumueleza kuwa, ameambiwa na watu kwamba mtoto wake hamshughulikii, ambapo kwa ana miezi mitatu hajapata siku zake za hedhi.

“Nilimwambia hilo sijalisikia, ndipo niliamua kumuliza mtoto akanijibu na baadae nikamuuliza aliekuwa akiishi nae akanithibitishia kuwa ni kweli”, alisema shangazi huyo.

Alieleza, alishangazwa sana na dada yake ambae alikuwa anajua tatizo hilo la mtoto kutopata siku zake lakini akashindwa kumpeleka hospitali kujua kitu kinachomsibu.

Alifahamisha, alimchukua na kumpeleka kwa dada yake mwengine ambae ni daktari na kumwambia amuangalie, ambapo alimjibu kuwa, tayari ana ujauzito na kuwashauri waongozane kumpeleka hospitali.

“Baada ya kugundua hivyo tulimuuliza amtaje aliempa ujauzito, mwazo alitwambia ni mtu mzima ambae alimwambia akimtaja atamuua lakini baada ya kwenda hospitali alimtaja kijana mwengene anaeitwa Arif”, alisema.

Alisema, hakuendelea kuifuatilia tena kesi hiyo kutokana na familia kumuona mbaya, huku wakijaribu kutaka kwenda kuitoa mimba hiyo, jambo ambalo hakulikubali.

“Nilimpigia simu mwalimu mkuu wa skuli ya msingi Kengeja kumuelezea na yeye alimwita mtoto kumuhoji, ambapo kule alimwambia mwalimu hana ujauzito na amelazimishwa amtaje ami yake aliekuwa akiishi nae”, alisema shangazi huyo.

Kwa upande wa mtoto huyo alisema kuwa, ujauzito huo alipewa na kijana ambae ni mkaazi wa Ole Wilaya ya Chake Chake ambae alikwenda Kengeja wakati wa uchaguzi na alikuwa anakaa kwa bibi yake.

“Alikuwa akiniambia twende bondeni, tukifika ananibaka wala, naiomba Serikali imchukulie hatua kali alienifanyia kitendo hichi”, alisema mtoto huyo.

Baba wa mtoto huyo alieleza, baada ya kumuhoji tena mwanawe alimpeleka hospitali Mkoani na baadae kwenda kituo cha Polisi Kengeja kuripoti.

“Nimelifuatilia mwenyewe suala hili na kwa sasa jalada limeshafunguliwa, nitazidi kufuatilia kesi ya mwanangu hadi nijue khatma, tangu skuli ilipofunguliwa hajaanza kwenda kwani bado sijapata unifomu”, alisema baba huyo.

Msaidizi Mwalimu Mkuu skuli ya msingi Kengeja Shauri Salum Omar alisema walipokea taarifa za mtoto huyo kupata ujauzito kutoka kwa shangazi yake, ambapo walichukua hatua ya kumuandikia mkurugenzi barua kwa kuwepo kwa taarifa hiyo katika skuli yao.

“Tulipomuhoji mtoto alisema kuwa, amefanywa kitendo hicho na mtu kutoka Kaskazini aliekuja kwenye uchaguzi wa Oktoba, lakini kilichotushangaza ni kwamba tangu uchaguzi upite haijafika miezi minne na mtoto alitwambia hajapata siku zake kwa miezi minne sasa”, alisema mwalimu huyo.

Sheha wa Shehia hiyo Mohamed Kassim Mohamed alikiri kuwepo kwa tukio hilo katika shehia yake na kusema kuwa tayari limeshafikishwa kituo cha Polisi.

“Hili tukio lina utata utata, nilipata taarifa kwa mwalimu mkuu, hivyo niliandika ripoti yangu na tayari nimeshaipeleka kwa Mkuu wa Wilaya”, alisema Sheha huyo.

Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Kusini Pemba Richard Tadei Mchomvu alithibitisha kupokea taarifa hiyo ya mtoto kupewa ujauzito na kusema kuwa upelelezi unaendelea.

Alisema kuwa, Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta kijana huyo anaetuhumiwa kumpa ujauzito mtoto wa miaka 14 na atakapopatikana anatafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

“Hatujapata taarifa rasmi za kijana huyo lakini ana miaka zaidi ya 20, hivyo tunaendelea kumtafuta na tutakapomkamata atafikishwa mahakamani”, alisema Kamishna Msaidizi huyo.

Alieleza kuwa, walipomuhoji mtoto huyo aliwaambia kuwa kijana huyo alikuwa akimpa pesa na kumchukua kwenda kumfanyia kitendo ch ubakaji.

Alisema kuwa, bado jamii haijajua umuhimu wa kumuheshimu mtoto na kusababisha vitendo hivyo kuongezeka siku hadi siku, hivyo ipo haja ya kutolewa elimu ili kuona kwamba mtoto anaachwa salama.