UONGOZI wa Kamati ya Skuli ya Msingi na Maandalizi Furaha Wilaya ya Chake Chake, wametakiwa kuacha tabia ya kuvikopesha kwa jamii vifaa, vinavyotolewa na wahisani kwa ajili ya ujenzi wa skuli hiyo.
Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa jimbo la Wawi Wilaya hiyo, wakati alipokua akizungumza na viongozi wa kamati ya skuli hiyo mara baada ya kukabidhi vifaa mbali mbali vya kumalizia ujenzi wa jengo la kupikia uji wanafunzi wa maandalizi.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona vitu vya skuli vinakopeshwa kwa jamii, wakati skuli bado inashida nyingi na inaendelea kupatiwa vifaa.
Alifahamisha kuwa kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo, utaweza kusaidia vijana kupikiwa uji katika mazingira mazuri na salama, ikizingatiwa jengo la zamani ilikuwa katika mazingira mabaya.
“Kilio cha skuli ni watoto wa maandalizi kutokua na sehemu ya kupikiwa uji, hii imetokana tokea kuanguka kwa banda kongwe la miti, sasa tumeamua kuwajengea jipya na watakunywa uji pia”alisema.
Aidha aliutka uongozi wa skuli hiyo kuvitumia vyema vifaa hivyo kwa lengo lililokusudiwa, ili wanafunzi waweze kuendelea kupikia uji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Maendeleo ya Skuli ya Msingi na Maandalizi Furaha, Ibrahim Mohamed Saleh alisema msaada huo wameupokea kwa mikono miwili na kuahidi kutumiwa kwa lengo lililokusudiwa na sio vyengine.
Naye mwalim Mkuu wa Skuli hiyo Chumu Hamad Juma, alishukuru kupatiwa vifaa vya ujenzi pamoja na kujengwa kabisa kwa jengo hilo, ili kuweza kuwarusiha watoto skuli pale panapopikwa uji.
Alifahamisha kuwa licha ya kusaidiwa msaada huo, lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali, alisema wanafunzi kwa sasa wanasoma katika mazingira mabovu hususana Maandalizi, kutokana na rafu ya darasa kutokua rafiki kwao.
Alisema changamoto nyengine ni kukosekana kwa uzio, katika skuli yao hali inayopelekea baadhi ya vitu vya walimu kuibiwa, pamoja na wanyama kuharibu vipando vyao.
Skuli ya maandalizi Furaha inawanafunzi 140, huku mwakilishi wajimbo la wawi akikabidhi mifuko 13 ya saruji, matufali 400 pamoja na gari moja ya mchanga kwa lengo la kumalizia ujenzi wa jiko hilo.