Thursday, January 9

Kengeja nao wanatarajiwa kufikiwa na mradi wa VIUNGO Zanzibar.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WAKULIMA wa shehia ya Kengeja Wilaya ya Mkoani Pemba wanaotarajiwa kufikiwa na mradi wa VIUNGO Zanzibar, wameziomba taasisi zinatekeleza mradi huo kusimamia vyema matakwa ya mradi katika kuwawezesha, ili kijikomboa na umasikini.

Mradi huo wa Viungo Zanzibar unasimamiwa na Serikali na kutekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA), Jumuiya ya Uhifadhi wa Misitu Asili Pemba (CFP) na shirika la PDF la Dar-es-Salaam, wenye thamani ya Euro million 5 unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.

Wakizungumza mara baada ya kusajiliwa katika mradi huo ikiwa ni miongoni mwa hatua za awali za utekelezaji, wakulima hao walisema ipo haja ya kuzingatiwa uadilifu na kuyafuata malengo yote ya mradi katika utekelezaji wake, ili wafanikiwe.

Walisema kuwa, ni vyema kwa taasisi zinazosimamia mradi huo, kutekeleza yale yote yanayo hitajika kufanyiwa wakulima katika kuwawezesha, ili waweze kujikwamua na maisha duni.

Kwa upande wake Miza Ali ambae ni mkulima wa migomba na mboga alisema, uadilifu ni nyenzo muhimu katika kutekeleza majukumu, hivyo matarajio yake ni kumsaidia kujiongezea kipato, ili aondokanae na utegemezi.

“Wanaotekeleza mradi tunawaomba wawe waadilifu, hii itatusaidia kutatua matatizo yetu yaliyomo kwenye kilimo chetu na kujikomboa na maisha magumu, kwani tutazalisha sana”, alieleza mkulima huyo.

Nae mkulima Nassor Salim Mohamed anaejishuhulisha na ufugaji pamoja na kilimo cha mboga na matunda alisema, ni vizuri kuweza kuendelezwa kielimu ili utakapomalizika mradi waendelee na shughuli zao za kilimo kwa ajili ya kujipatia manufaa.

“Kwa kweli elimu ndio kila kitu, kwa sababu tutapata utaalamu wa kuzalisha mazao bora, kujua magonjwa yanayokumba mazao yetu na pia tutaweza kubuni miradi mengine itokanayo na mazao yetu”, alisema.

Mkulima Asha Mbarouk Hamad mwenye mazao mchanganyiko katika shamba lake alisema, wanakabiliwa na ukosefu wa dawa ambayo inawarejesha nyuma maendeleo ya kilimo kutokana na kuwa mazao mengi huharibika.

Meneja mradi Kanda ya Pemba Sharif Maalim Hamad amewashukuru wakulima kuweza kujitokeza kwa wingi katika usajili wa mradi huo, jambo ambalo limeonesha chachu ya mafanikio katika utekelezaji wa mradi.

Nae Mtaalamu wa Miundombinu kutoka mradi huo Amour Juma Mohamed amewatoa hofu wakulima kwa kusema kwamba mradi huo umeangalia vitu vingi katika utekelezaji, hivyo wakulima watarajie mafanikio na waache fikra potofu ya kuwa kilimo hakiwezi kuwanufaisha.

Zoezi hilo la usajili wa wakulima kwa Wilaya ya Mkoani limeonesha mwanzo mzuri, ambapo wakulima wengi walijitokeza kusajiliwa katika mradi huo.