RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Dk. Hussein Ali Mwinyi leo amewaapisha Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria aliowateua hivi karibuni.
Walioapishwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar ni Ibrahim Mzee Ibrahim na Haji Omar Haji.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, alieapishwa hivi leo ni Khadija Shamte Mzee.
Hafla ya kuapishwa viongozi hao ilifanyika Ikulu Jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Mwinyi Talib Haji.
Wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Mhandisi Zena Ahmed Said, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa, Majaji wa Mahakama Kuu, Makatibu Wakuu, Viongozi wa dini, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, viongozi wengine wa Serikali pamoja na Wanafamilia.
Majaji hao waliteuliwa tarehe 01 Februari 2021 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya Kifungu Namba 94 (2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Nae Khadija Shamte Mzee aliteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi mnamo tarehe 07 Januari, 2021.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar