MKURUGENZI wa Taasisi ya Utafi ti ya Dawa Asili Muhimbili (MUHAS), Dk Joseph Otieno, amesema kujifukiza ni tiba ambayo ikitumika vizuri, inaboresha mfumo wa upumuaji na kuusaidia mwili kupata nguvu ya kupambana na maradhi.
Akizungumza na HabariLeo jijini Dar es Salaam, Dk Otieno alisema kwenye mlipuko wa virusi vya corona, ni vyema wananchi bila kujali kama wameathirika au la, wajenge tabia ya kujifukiza angalau mara mbili kwa siku ili kuukinga mwili usipate virusi hivyo. Kwa mujibu wa Dk Otieno, kujifukiza ni tiba iliyokuwa ikitumika katika jamii nchini na ilionesha matokeo chanya.
“Nasisitiza tena kama nilivyosisitiza mwaka jana wakati wa janga la corona lilipoingia nchini, kujifukiza kwa njia sahihi ni kinga dhidi ya maradhi haya, cha msingi ni kutumia viungo sahihi na kufuata maelekezo jinsi ya kuvichanganya na kujifukiza,”alisema.
Alizungumzia namna ya kudhibiti virusi vya corona kwa kutumia njia za asili ikiwemo ya kujifukiza maarufu kupiga nyungu, Dk Otieno alishauri kuwa kwa mazingira ya Tanzania, aina tatu za majani zinapatikana kwa urahisi na zimefanyiwa utafiti na kuthibitika ubora wake, lakini pia zina machapisho.
Alitaja majani hayo kuwa ni ya kivumbasi (kashwagala), mkaratusi na mchaichai. Alisema usalama wa majani hayo, umethibitika na yana mafuta tete yanayosaidia kufungua mfumo wa upumuaji ili mwili upate nguvu ya kupambana na maradhi.
“Nyungu inafaa sana kama virusi bado viko kwenye mfumo wa upumuaji havijaingia kwenye seli za damu, kwa sababu unapojifukiza kwa kutumia vitu hivyo vitatu kwa njia sahihi, hayo mafuta tete yanapenya vizuri na kuingia kwenye mfumo wa upumuaji na kuuzibua, hapo mwili unapata nguvu na kupambana vizuri’’alisema Dk Otieno.
Alisema, iwapo virusi vya corona vitakuwa vimeingia kwenye seli za damu, njia sahihi ya kuusaidia mwili kupambana navyo ni kutumia maji ya moto yaliyochanganywa na tangawizi ili kusaidia damu isigande kwenye mishipa wakati huo mwili ukipambana na virusi.
Dk Otieno alisema kiungo kingine kinachofanya kazi sawa na tangawizi katika kupambana na corona ni kitunguu saumu, ambacho kazi yake ni kusaidia damu isigande wakati mwili unapambana na maradhi.
Alisema kitunguu saumu katika tiba hii, kinatakiwa kisagwe na kuwekwa kwenye maji baridi au kukitafuna kibichi, kwa sababu ukikichemsha unaua nguvu yake na hapo hakitafanya kazi kusudiwa.
Kwa mujibu wa Dk Otieno, kwa kawaida virusi havina tiba na vinapoingia mwilini hupambana na kinga ya mwili na kama mwili ukiwa na kinga nzuri huvishinda na kuviua, lakini ukiwa na kinga dhaifu mwili hushindwa kupambana navyo na matokeo yake ni kifo. Alisema watu wengi hukosea namna ya kujifukiza, kwa kuwa wanachemsha majani ya mimea hiyo hadi yanapoteza mafuta tete yanayohitajika.
Dk Otieno alisema ili kujifukiza, inabidi kuchemsha maji hadi yatokote kisha unaweka majani ya mchaichai, mkaratusi na kivumbasi (kashwagala) na kukoroga, kisha kuyaepua na kuanza kujifukizwa kwa kujifunika na shuka zito au blanketi kwa dakika kati ya tano hadi 10 kulingana na uwezo wa mwili.
“Wengi wanakosea wanadhani unachemshia hivyo vitu huko wee, kufanya hivyo unaua mafuta tete yote yanayohitajika,”alisema.
Dk Otieno alisema kujifukiza si lazima mtumiaji atumie vitu hivyo vitatu, anaweza kutumia kimojawapo na kuzingatia maelekezo, afanye hivyo kwa mara mbili kwa siku na kusisitiza kujifukiza kuwa sehemu ya maisha ya wananchi kila siku.
Alisema mtu anayejifukiza anapaswa kufunga macho, kuachama mdomo na pua, kisha aendelee kuhema kawaida ili kuruhusu mvuke kupita kwenye mfumo wa upumuaji na akishaepua nyungu, akoroge mara moja ili ule mvuke mkali utoke kisha ndio ajifunike na shuka au blanketi.
Alishauri kuwa wagonjwa, wazee na watoto, wasijifukize ila wanywe maji ya moto yenye tangawizi, au iliki na mdalasini.
*Chanzo: HabariLeo*