Monday, November 25

Mkutano wa pili wa Baraza la kumi la Wawakilishi kuanza tarehe 10/02/2021

Katibu wa Baraza la Wawakilishi Raya Issa Msellem akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali kuhusu shughuli za mkutano wa pili wa Baraza la kumi la Wawakilishi utakaoanza tarehe 10 februari, 2021 katika Ofisi za Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji Zanzibar.

 

Mkutano wa Pili wa Baraza la Kumi  la Wawakilishi Zanzibar unatarajiwa kuanza siku ya Jumatano  tarehe 10 February, 2021, saa tatu asubuhi.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu shughuli za mkutano wa pili wa Baraza la kumi katika Ofisi ya Baraza hilo Chukwani, Katibu wa Baraza Raya Issa Mselem  amesema masuala 91 yataulizwa na kujibiwa na Mawaziri husika.

Amesema ripoti ya nne ya Utekelezaji wa kazi za Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa mwaka 2019/2020 na ripoti ya Mdhibiti  na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa Mawizara, Mashirika  na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2018/2019 zitawasilishwa.

Katibu wa Baraza la Wawakilishi amesema kutakuwepo na mjadala wa hotuba ya Mh. Rais wa Zanzibar aliyoitoa katika ufunguzi wa Baraza la  kumi la Wawakilishi tarehe 11/11/2020.

Amesema kutawasilishwa mwelekeo wa Mpango wa Taifa kwa mwaka 2021/2022na mswaada wa dharura wa sheria ya mambo mbali mbali na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Katibu Raya ameongeza kwamba kutakuwa na ripoti ya jitihada ya kuzuiya Rushwa na uhujumu na uchumi Zanzibar na uchaguzi wa wenye viti wa Baraza  pamoja  na marekebisho ya jaduweli ya Pili ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma Zanzibar Nam 4 ya 2015.

Kazi nyengine itakayotekelezwa katika mkutano wa Pili wa Baraza la kumi la Wawakilishi ni kufanya uchaguzi wa wajumbe wa tano kuingia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanziania na uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya mbali mbali za Baraza (CPA, CWP, APNAC, UWAKUZA na Jumuiya ya Mabadiliko ya Tabia ya Nchi).