Sunday, November 24

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla ahudhuria mazishi ya Naibu Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Ali Abdulla Ali

Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Qabi akiongoza Dua ya kumuomba Marehemu Ali Abdulaa Ali Naibu Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Naibu Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Ali Abdulla Ali aliyefariki Dunia Jumatano baada ya kuugua kwa muda mrefu alipokuwa akisumbuliwa na Maradhi ya Kisukari amezikwa Kijijini Kwao Bumbwini Misufini Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mamia ya Wananchi, Waumini wa Dini tofauti, Viongozi wa Kiserikali, Vyama vya Kisiasa pamoja na Wana Familia wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla walihudhuria Mazishi hayo mapema  Asubuhi.

Marehemu Ali Abdulla Ali kama walivyo Watoto wa Ukanda wa Mwambao wa Afrika ya Mashariki aliwajibika kupata Elimu yake ya Madrasa iliyokwenda sambamba na ile ya Kidunia ambapo katika Ujana wake ilimuwezesha kuingia katika mfumo wa Utumishi wa Umma na baadae kutinga katika ulingo wa Kisiasa.

Katika Uhai wake Marehemu Naibu Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Ali Abdulla Ali alibahatika kupata nafasi hiyo ya Unaibu Spika kupitia Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akiwawakilisha Wananchi wa Jimbo la Mfenesini kwa muda mrefu.

Marehemu Ali Abdulla Ali aliwahi pia kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi na kabla ya hapo aliwahi kushika wadhifa wa iliyokuwa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Sita.

Mchango wa Marehemu Ali Abdulla Ali mbali ya kuwatumikia Wananchi wa Jimbo la Mfenesini lakini pia uligusa Kundi kubwa la Vijana katika Mabaraza yao ya Vijana alipokuwa mstari wa mbele katika kuona Nguvu za Vijana zinaendelea kutumika ndani ya Taifa hili.

Ushahidi wa hayo ni pale Marehemu Mzee Ali Abdulla Ali alipojumuika pamoja na Wajumbe wa Baraza Kuu la Vijana Zanzibar wakati wa Mdahalo Maalum wa Sherehe za Maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 kutimia Miaka 50.

Marehemu Ali Abdulla Ali ameacha Kizuka Mmoja na Watoto Watatu wa Kike. Allah amjaalie wepesi wa safari yake ya halali ya kudumu isiyo na shaka baada ya kuonja mauti. Amin.

Jamaa na Wana Familia wakiubeba Mwili wa Marehemu Ali Abdulla Ali kuupeleka Msikitini kwa ajili ya kwenda kukamilisha taratibu za sala ya Maiti.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiwafariji Watoto wa Naibu Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Marehema Ali Abdulla Ali hapo Kijijini kwao Bumbwini Misufini alipozikwa.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar