RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kilichotokea leo Februari 2021 mnamo majira ya saa 5:26 asubuhi.
Akitangaza kutokea kwa msiba huo, Rais Dk. Mwinyi amesema kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amefariki dunia wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa tokea tarehe 09 Februari, 2021.
“Kwa niaba ya wananchi, nachukua fursa hii kutoa pole na salamu zangu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, Chama cha ACT-Wazalendo na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania na kuwataka wawe na subira na ustahamilivu katika kipindi hiki cha majonzi”, alisema Rais Dk. Mwinyi katika taarifa hiyo.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hakika Taifa limepoteza kiongozi Mzalendo na shupavu.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi katika taarifa hiyo maalum ya tanzia alieleza kuwa taarifa zaidi za msiba huo na maziko yake zitaendelea kutolewa na Serikali kwa ushirikiano wa karibu na familia pamoja na chama cha ACT-Wazalendo.
Rais Dk. Mwinyi alimuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahala pema peponi. Amin.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar