Monday, November 25

Dkt Mwinyi aongoza mazishi ya Makamo wa Kwanza Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi, akiwasilia katika kijiji cha Mtambwe Nyali Wilaya ya Wete, kwa ajili ya kushiriki katika mazishi ya aliyekua Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefariki dunia Hospita;li ya Muhimbili jijini Dar Salam.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

NA WAANDISHI WETU .PEMBA.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti  wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar , Alhajj Dk , Hussein Ali Mwinyi, ameongoza mazishi ya aliekuwa Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliefariki dunia katika Hospitali ya Muhimbili alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

Pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuongoza mazishi hayo pia viongozi mbali mbali wa Serikali wakiwemo Viongozi wastaafu akiwemo Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk, Ali Moh’d Shein walihudhuria maziko hayo huko katika kijiji cha Nyali Mtambwe.

Muili wa marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kuwasili katika kiwanja cha ndege cha Karume Pemba, na kupokelewa na viongozi mbali mbali wa Serikali na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama ulipelekwa katika kiwanja cha Gombani Pemba ukipitia maeneo mbali mbali ya mji wa Chake Chake kwa ajili ya kusaliwa .

Baada ya wananchi na Viongozi mbali mbali wa Serikali  kupata fursa ya kuusalia mwili wa aliekuwa Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar  maalim Seif Sharif , muili huo ulipelekwa moja kwa moja katika maeneo ya kijijini kwao Mtambwe Nyali Mkoa wa Kaskazini Pemba  kwa ajili ya mazishi  ikiwa ni safari yake ya mwisho.

Marehemu makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar , Maalim Seif Sharif Hamad baada ya kuwasili mwili wake kijijini kwao Mtambwe Nyali wananchi , wafuasi wa Chama chake cha ACT na ndugu zake nao walipata fursa ya kipekee kwa kuuwaga muili wa mpendwa wao kwa kumsalia na baadae kuzikwa katika makabuni yao ya familia.

Kwa upande wake makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla akitowa salamu za Serikali ya Mapinduzi , aliwashukuru wananchi wote kwa ushirikiano wao waliouonesha katika kumsitiri makamo wa kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad.

Alisema marehemu maalim Seif, alianza kuuguwa tarehe 29/1/2021  na kulazwa katika Hospitali ya Mnazi mmoja Unguja na baada ya kuonekana kupata nafuu alipelekwa katika         Hospitali ya Muhimbili Dar-es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi .

“ Tunawashukuru madaktari wote wa Hospitali ya Mnazi mmoja na wale wa Muhimbili kwa mchango wenu mkubwa katika kusimamia matibabu ya marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, lakini hata hivyo Mwenyeezi Mungu amechukuwa kiumbe chake,”alisema.

Alifahamisa kuwa katika uhai wake Maalim Seif alitowa mchango mkubwa Zanzibar kwani mbali na kuwa mwanasiasa bali alikuwa mwalimu wa Skuli mbali mbali ambae aliwapatia watu wengi Elimu ambayo wanaitumia hadi sasa.

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar , Hemed Suleiman Abdalla, alisema Serikali itaendelea kumkumbuka kwani alishiriki katika mchakato wa maridhiano ya kisiasa Zanzibar kwa vipindi vyote.

“ Serikali ya Mapinduzi Zanzibar , inatowa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa  na John Pombe Magufuli kwa kusimamia matibabu ya kiongozi huyo”, alisema.

Aidha alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar , inatowa pole kwa wafiwa wote , wananchi na Viongozi wa chama cha ACT wazalendo kwa msiba wa Kiongozi huyo muhimu na kuwataka kuwa na subra.

Akisoma wasifu wa marehemu maalim Seif Sharif Hamad , waziri wa nchi Ofisi ya Makamo wa pili wa Rais Sera na uratibu na shughuli za baraza la Wakilishi  Zanzibar Khalid Salum Moh’d , alisema alizaliwa tarehe 22 Octoba mwaka 1943 , mtambwe nayali na alipitia skuli  za uondwe na skuli  ya wavulana ya wete kisiwani Pemba kati ya 1950 – 1957.

Alisoma  Elimu yake  ya sekondari katika skuli ya KING GEORGE Memorial mjini Zanzibar, Lumumba  na aliendelea na masomo ya cheti cha cha sekondari katika skuli  hiyo.

Mwaka 1972 -1975 , alijiunga na chuo kikuu cha Dar-es –Salaam ,shahada ya  mwaka 1977 alianza rasmi safari yake ya kisiasa na mwaka 1984-1988 alikuwa waziri kiongozi wa Zanzibar.

Mwaka 1995 marehemu maalim Seif Sharif Hamad, aligombea nafasi ya urais wa Zanzibar kwa mara ya kwanza kwa tiketi ya Chama cha CUF, wakati mwaka 2000, 2005 2010 na mwaka 2015 pia aligombea nafasi hiyo ya Urais wa Zanzibar kupitia chama cha  CUF.

Marehemu maalim Seif Sharif Hamad  mwaka 2010 aliteuliwa kuwa makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kutoka chama cha CUF na mwaka 2019 katika misuko suko ya kisiasa alijitowa katika chama cha CUF na kujiunga na Chama cha ACT na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama hicho Taifa.

Mnamo mwaka 2020 marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, aligombea tena Urais wa Zanzibar mara hii akiwa na Chama cha ACT Wazalendo na pamoja na kwamba hakushinda lakini kutokana na kura alizopata Dk,Mwinyi alimteuwa kuwa makamo wa kwanza wa Rais hadi mauti yakimfikia huko katika Hospitali ya Muhimbili.

Maalim Seif atakumbukwa katika visiwa vya Zanzibar nan je ya Zanzibar na duniani kote, pia alikuwa ni muanzilishi wa mazungumzo ya kisiasa Zanzibar.

Aidha Maalim Seif ameacha kizuka na watoto wanne.

Kwa upande wake Kiongozi mkuu wa ACT Wazalendo Taifa, Zito Zubeir Kabwe, akitowa salamu za Chama chake aliwashukuru Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa nchini kwa mashirikiano yao katika kuiweka mahala pazuri roho ya Mwenyekiti wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad.

Aliwataka Wananchi wa Zanzibar kutohuzunika kwa kuondokewa na Maalim Seif Sharif Hamad bali wafurahie maisha yake kwa jimsi alivyoyatowa juu ya kupigania haki zao.

Kiongozi mkuu huyo wa ACT Wazalendo, alimuelezea Maalim Seif katika uhai wake alikuwa ni baba wa Demokrasia na mapambanaji wa haki za watu wote na Chama kimepoteza mtu muhimu , mpatanishi wa ndani ya Chama  chao.

Alisema madhila yote aliopitia marehemu  Maalim Seif Sharif , alisimama imara katika kusimamia na kutetea haki za watu wote, alikuwa msamehevu na hakukata tamaa kwa jambo lolote ambalo analiamini katika kusimamia haki na kupambania maisha ya watu.

Zito Kabwe , alinukuu maneno ya marehemu ya maalimu Seif aliyoyatowa  katika Kiwanja cha Tibirinzi Pemba kwa kuwaambia wananchi kwamba “ Nipo nanyi , na waahidi nikiwa ndani ya chama au nje ya Chama, ndani ya Serikali nan je ya Serikali “mwisho wa kunukuu.

Alifahamisha katika uhai wake Maalimu Seif alikuwa ni mpigania uhuru , aliipenda nchi na amani ya nchi yake na aliwafundisha suala la amani na maridhiano kwa viongozi wa mataifa mbali mbali waliowakidhania Siasa za upinzani ni ugomvi.

Alisema katika hilo alikuwa na kifua kipana cha kuhimili suala la maridhiano wakati wote wa maisha yake na ndio mpaka anafikwa na umati alikuwa ni muumini wa suala la maridhiano ya kisiasa ndani ya nchi yake.

Maziko ya makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, marehemu Seif Sharif Hamad , yamefanyika kijijini kwao Mtambwe Nyali na kuhudhuriwa na watu mbali mbali wakiwemo Viongozi wakuu wa Vyama vya Siasa na Serikali .