Monday, November 25

Ijue Historia ya Maalim Seif Sharif Hamad.

Seif Sharif Hamad

Maalim Seif Shariff Hamad (amezaliwa Nyali, Mtambwe kisiwani Pemba, 22 Oktoba 1943 – na amefariki  Dar es Salaam, 17 Februari 2021) alikuwa mwanasiasa wa Zanzibar (Tanzania).

Aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa serikali ya Zanzibar (1984-1988) akagombea mara kadhaa Urais wa nchi hiyo . Mara mbili alipata kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Maisha

Alipata elimu yake ya msingi katika skuli ya msingi Uondwe, 1950 na baadaye alijiunga na elimu ya sekondari katika skuli ya watoto wa kiume Wete Pemba 1952. Baadaye aliendelea na elimu ya sekondari katika skuli ya King George na kuhitimu kidato cha sita mwaka 1963 ambapo baadaye kati ya mwaka 1972 na 1975 alihitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutunukiwa shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa (Political Science).

Kazi

Kati ya mwaka 1972 na 1975 alifundisha katika skuli mbalimbali za Unguja na Pemba, zikiwemo Fidel Castro na Lumumba.

Siasa

Baadaye Maalim Seif alianza kuingia katika masuala ya siasa, ambapo mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni na Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi.

Mwaka 1977 hadi 1987, alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na kuwa Mjumbe wa Kamati kuu ya chama hicho.

Mwaka 1982 hadi 1987 alikuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya Chama cha Mapinduzi na 1984 aliteuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hadi mwaka 1988.

Baada hapo, misukosuko mikubwa ya kisiasa ilianza kumkumba ambapo Januari 1988 alipoteza nafasi ya Uwaziri Kiongozi na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi baada ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Idrisa Abdulwakil kutangaza kulivunja Baraza la Mawaziri.

Alikuwa makamu wa kwanza wa raisi katika serikali ya awamu ya nane ya raisi Huseyn Mwinyi

 

Kujiengua na CCM na kujiunga na upinzani

Mnamo Mei 1988, Maalim Seif alitoka katika chama cha CCM.

Mwaka 1992, Maalim Seif alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama cha upinzani CUF (Chama cha Wananchi). Kwa muda mrefu alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Tarehe 18 Machi 2019 alitangaza kujiunga na chama cha ACT Wazalendo: maamuzi hayo yalifanywa muda mchache baada ya kesi iliyokuwa mahakamani kuishia kumtambua profesa Ibrahim Lipumba kuwa ndiye Mwenyekiti halali wa chama cha CUF.

Hamad alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa ACT Wazalendo, nafasi aliyopewa kando ya kiongozi wa kitaifa Zitto Kabwe

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 alirudia nafasi yake ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika serikali ya umoja wa taifa aliyokuwanayo hadi mwaka 2015.

Kifo

Seif Sharifu Hamadi alifariki tarehe 17 Februari 2021 katika hospitali ya taifa ya Muhimbili

 

 

CHANZO CHA HABARI WIKIPEDIA KAMUSI ELEZO HURU