NA MWANDISHI WETU, PEMBA
WANANCHI kisiwani Pemba wamesema, wamepokea kwa mshtuko taarifa ya kifo Cha Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na kwamba hawatomsahau kwa mchango wake wa kuwaweka pamoja katika kudumisha amani na mshikamani.
Walisema kuwa, marehemu alikuwa anapenda kutetea maslahi ya wananchi wa Zanzibar kipindi cha uhai wake na kwamba hakuchoka kupigania mpaka umauti kumfika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema, watamkumbuka Maalim Seif kwa mchango wake mkubwa wa kutetea haki zao na kamwe hwatoacha kumuombe dua.
“Kwa kweli Maalim Seif alikuwa ni mtu jasiri, mpiganaji na asiechoka na mwenye huruma, licha ya changamoto alizokuwa akikumbana nazo lakini hakukata tamaa, tutamuenzi na kumuombea dua kila siku Allah amlaze mahala pema peponi”, walisema wananchi hao.
Walieleza kuwa, Maalim Seif amewaachia wananchi wa Zanzibar zawadi kubwa ya kuwaweka pamoja na kuepukana na ubaguzi, jambo ambalo ni faraja kwani ameondoka bila ya dhima.
“Ameondoka akiwa msafi kwa sababu watu wote ni wamoja, hakuna mifarakano wala mipasuko, hii ni faida kwetu na ni sadaka kwake yeye huko aendako”, walieleza.
Mmoja wa wananchi mkaazi wa Chake Chake Asha Abdalla Hamad alisema kuwa, wameumia sana kuondoka kwa Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif, ingawa kitu kinachowapa faraja ni kule kuwaweka pamoja wananchi wa Zanzibar.
“Kifo ni muandiko wa mwenyewe Allah, hakuna awezae kukiepuka, hivyo imefika siku yake lililobakia ni kumuombea dua kwa wingi”, alieleza.
Nae Rukia Yussuf mkaazi wa Wete alisema, hakuna mtu mwengine atakaeweza kumfikia Maalim Seif, kwani alikuwa ni mwenye huruma wala asie na kiburi kwa wenzake.
“Nipopewa taarifa ilikuwa nakula, chakula kilinishinda kwa sababu nakumbuka alivyokuwa akipigania haki zetu, hakuna mwengine atakaemfikia yeye”, alisema mama huyo.
Mwananchi wa Chake Chake ambae hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa, kinachomuuma zaidi ni kutokana na kukosa taarifa sahihi wakati alipokuwa mgonjwa, jambo ambalo linawasikitisha.
“Yule ni kiongozi wa kitaifa hivyo Serikali ilipaswa itoe taarifa za ugonjwa wake hatua kwa hatua, ili wananchi wajue, kwa kweli hatukutendewa haki”, alisema mwananchi huyo.
Nae mwananchi Khamis Ali Omar alisema, ili kumuenzi zaidi marehemu, ipo haja ya kuendeleza umoja na mshikamano aliouwacha kwa wananchi wa Zanzibar, ili kumpa furaha ya milele.
Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amefariki Febuari 17 katika hospitali ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu na amezikwa kijijini kwao Mtambwe Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mungu ailaze roho ya marehemu mahala Pema Peponi Amiin.