NA ABDI SULEIMAN.
MBUNGE wa Jimbo la Gando Kisiwani Pemba Kupitia chama cha Mapinduzi Salim Mussa Omar, amekabidhi baskeli nane (8) vya magurudumu matatu kwa watu wenye ulemavu waliomo ndani ya jimbo hilo, vikiwemo vinne (4) vinavyotumia Umeme na vinne vya kawaida, vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 12.
Baskeli hizo zilizokabidhiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa kwa wananchi wajimbo hilo, wakati akiomba kuwa kuwa atahakikisha walemavu wote wanapatiwa baskeli hizo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Akizungumza na walezi na wazazi katika hafla ya kukabidhi vibaskeli hivyo huko Gando, Mbunge huyo alisema atahakikisha kabla ya mwaka kumalizika kila mlemavu ndani ya jimbo hilo amepatiwa kifaa maalumu kwa ajili ya kumsaidia katika shuhuli zake.
Alisema kuwa watu wenye ulemavu hawakuomba bali ni rehma kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo haipendezi kuona watu hao wanadharauliwa na kuonekana kuwa hawana thamani ndani ya jamii.
Aidha ambunge huyo alisema fedha anazohudumia jimboni mwake ni fedha alizopatiwa na Bunge kwa ajili ya ununuzi wa gari, hivyo aliwataka wananchi na viongozi wa vyama vya upinzani kufahamu hivyo na sio kwamba anachokifanya ni sifa.
“Kumekua na maneno mengi kwa baadhi ya wananchi na hata viongozi wengine, wakidai kwamba mimi nafanya hivi kwa kujionesha bali nafanya kwa kusaidia wananchi wangu wa jimbo, fedha nilizopewa milioni Miamoja ndio hizi ninazozitoa na sio kama nimenunulia gari”alisema.
Hata hivyo aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumvumilia kwani kuna mambo makubwa yanakuja jimboni mwao, ikiwemo ujenzi wa ofisi ya Mbunge na Hospitali maalumu kwa ajili ya akinamama na itakuwa na madaktari wanawake watupu.
Katika hatua nyengine Mbunge huyo aliwataka wananchi wa jimbo hilo, kuhakikisha wanawadharau wananchi wenye nia mbaya ya kuvuruga mipango ya maendeleo ya jimbo ambayo mbunge huyo amepanga kuwapatia.
Mwenyekiti wakamati ya mbunge Hashim Maalim Kheir, aliwataka wananchi kutambua malengo yao, na kupokea kile ambacho wanachopatiwa, ifike wakati hakuna kero yoyote ndani ya jimbo hilo.
Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Gando Massoud Ismail Juma, alisema jukumu la mbunge ni kusaidia huduma za jamii jimboni kwake, hivyo yoyote atakaekabidhiwa vifaa hivyo anapaswa kuvitunza na kuvithamini ili vidumu kwa muda mrefu.
Hata hivyo aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumuunga mkono mbunge huyo katika harakati zakuibadilisha mazingira ya jimbo la gando na kuifanya Gando kuwa ya kisasa.
Kwa upande waKE Salim Abdalla Salim (Injia), mmoja ya vijana wenye ulemavu ambaye kwa sasa anajishuhulisha na uchomaji worldingi, alisema baskeli hiyo itamsaidia kufikisha katika kiwanda chake kwa haraka.
Aidha alim[pongeza mbunge huyo kwa kuwajali watu wenye ulemavu ndani ya jimbo lake, huku akiwataka wenzake kuvithamini na kuvitunza vifaa hivyo.
Salma Omar Abdalla, alisema baskeli hiyo itaweza kumsadiia mama yake kufika katika sehemu anazotaka kwenda, kwani hapo mwanzo ilikuwa ni ngumu kwake.