Sunday, March 16

“Tumieni vyema elimu ya nadharia na vitendo mnayopatiwa kupitia miradi mbali mbali ili kuleta tija na maendeleo”Ofisa Mdhamini Wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo.

AFISA Mdhamini Wizara ya Habari Vijan Utamaduni na Michezo Pemba Salum Ubwa Nassor, akizunguma na vikundi vya vijana kutoka Mgelema na Chonga ambavyo vipo chini ya mradi wa Fursa 600 kwa vijana unaosimamiwa na kituo cha majadiliano kwa vijana (CYD) Zanzibar.

WAJASIRIAMALI wa vikundi vya ushirika Kisiwani Pemba, wametakiwa kuitumia vyema elimu ya nadharia na vitendo wanayopatiwa kupitia miradi mbali mbali ili kuleta tija na maendeleo katika kuboresha shughuli zao za kila siku.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Mdhamini Wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo Salim Ubwa Nassor wakati alipokua akifunga mafunzo kwa vikundi vya wajasiriamali vijana wa Shehia ya Chonga na Mgelema Wilaya ya Chake chake Mkoa wa kusini Pemba.

Alieleza kuwa, kupitia wizara yake atahakikisha kila sekta anaitendea haki kwa mujibu wa kazi aliopewa huku akiwekeza zaidi kwa vijana kwani alisema, Rais wa Zanzibar Dk, Hussein Mwinyi anadhamira kubwa kwa vijana ili kuwaletea maendeleo.

“Niipongeze taasisi hii ya kituo cha majadiliano ya vijana CYD kwa kuwapatia elimu hii nawaombeni sana tuitumie ipaswavyo ili tuweze kufika pale ambapo tumepakusudia” alisema.

Alifahamisha kuwa, wizara hiyo kupitia Idara ya vijana itahakikisha inasimamia vyema miradi ya vijana na kuweza kuwasaidia katika hatua za kujikwamua na umasikini wa kipato ikiwemo kuwapatia taaluma na nyenzo zitakazowapelekea kujiajiri kupitia shughuli mbali mbali za ujasiriamali.

Aidha alisema, Serikali ya awamu ya nane katika vipaombele vyake ni pamoja na kuwawezesha vijana hivyo, aliwataka vijana hao kujenga mashirikiano ya pamoja katika harakati zao na kubuni miradi mbali mbali ambayo itaweza kuwaletea tija na kupunguza kundi la vijana tegemezi.

Mapema Mratibu wa Taasisi ya kituo cha majadiliano ya vijana CYD Pemba Ali Shaaban Mtwana alisema, CYD imeundwa kwa dhamira ya kuwakomboa vijana na kuwatoa katika hali duni na kuwapeleka katika sehemu ambayo itawapatia maendeleo.

“Malengo ya mradi wetu ni kuongeza ujuzi, tija na kipato kwa vijana wa leo na kesho na ndio maana mradi huu umejikita zaidi na kutoa mafunzo ambayo yatawabadilisha vijana kwa kujitambua wao wenyewe na kujikomboa kiuchumi” alisema.

Hata hivyo alisema, mradi huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kutoa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa vijana, kuwajengea uwezo katika suala zima la dhana ya ujasiriamali, mafunzo ya udhibiti na usimamizi wa fedha na mafunzo ya kutafuta fursa za masoko.

Afisa vijana na Mkufunzi wa mafunzo kutoka Idara ya vijana Pemba Seif Edward Kabeyu alisema, kupitia fursa walioipata kwa CYD ameweza kutekeleza majukumu na kuisaidia idara yake kwani alisema, endapo wataendelea kuishirikisha taasisi hiyo katika mipango yao watapiga hatua zaidi za kimaendeleo.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo  walisema CYD ni mkombozi mkubwa wa vijana kuwapatia taaluma za aina mbali mbali za kuwaendesha shughuli zao na kuiomba Serikali kuendelea kuwaunga mkono na kuwatatulia changamoto zao ambazo zimekua zikiwakabili.