Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema serikali ya mapinduzi Zanzibar imefungua milango yake kwa waekezaji wa sekta binafsi kutoka ndani na nje ya nchi kuekeza katika miradi mbali mbali kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi na kuimarisha ustawi wa wananchi wake.
Mhe. Hemed ameleza hayo wakati akizungumza na viongozi na wataalamu wa Kampuni ya SoftLine kutoka nchini Urusi waliofika ofisini kwake Vuga jijini Zanzibar kwa lengo la kuwasilisha mpango wao na kuonesha nia ya kuekeza kupitia mradi wa mji Salama.
Akigusia juu ya mradi wa mji salama ambao kampuni hiyo imeonesha nia yake ya kuekeza Makamu wa Pili wa Rais aliwaeleza wawekezaji hao kwamba, kwa vile Zanzibar ni nchi kisiwa kama zilivyo nje nyengine akitolea mfani nchi ya Moritus alisema inahitaji miradi ya aina hiyo kwa lengo la kuimarisha usalama wa watalii wanaofika nchini.
Mhe. Hemed alisema serikali inaendelea kuimarisha mazingira mazuri ya uwekezaji kwa kuzipitia na kuzifanyia marekebisho sheria mbali mbali ili ziweze kutoa urahsi Zaidi kwa wawekezaji kwa kuzingatia upatikanaji wa maslahi baina ya pande mbili (Win Win Situation).
Kwa upande wake Mkurugenzi wa maendeleo ya bishara kutoka kampuni ya Softline Evgeniy Chizhov alimueleza Mhe. Makamu wa Pili wa Rais kuwa kampuni yao ina uzoefu mkubwa katika masuala ya kuimarisha ulinzi wa miji kutokana na kufanya kazi kwake kwa muda mrefu sasa.
Kampuni ya Softline kutoka Urusi imeshatekeleza miradi na kufanya kazi zake katika nchi mbali mbali ikiwemo India, Bangladeshi na Nchi nyengine mbali mbali zilizopo katika muunganiko wa iliokuwa muungano wa nchi za Sovieti.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Febuari 22, 2021.