RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kuhakikisha amani na usalama vinaimarishwa hapa nchini.
Hayo aliyasema leo wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Boniface Simbachawene Ikulu Jijijini Zanzibar akiwa amefuatana na ujumbe wake akiwemo Naibu wa Wizara hiyo Khamis Hamza Chilo.
katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Waziri huyo kwamba mashirikiano zaidi yanahitajika katika kuhakikisha Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano inaendeleza amani na usalama ambao ndio tunu ya Taifa.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimueleza kiongozi huyo juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza sekta ya uwekezaji hapa nchini.
Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Wizara hiyo ya kushirikiana na Serikali na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha sekta hiyo inazidi kuimarika hasa ikizingatiwa mchango wake katika uchumi wa Zanzibar.
Mapema katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alipokea pole kutoka kwa Waziri Chimbachawene kufuatia kifo cha aliyekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alipokea pongezi kutoka kwa kiongozi huyo kufuatia ushindi wake wa kishindo wa nafasi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alioupata katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Geoge Boniface Simbachawene alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Wizara anayoiongoza itaendeleza ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba Wizara hiyo ni ya Muungano.
Aidha, Waziri Simbachawene alieleza hatua zitakazochukuliwa katika kuhakikisha mashirikiano yanaimarika katika kuimarisha na kuendeleza sekta ya uwekezaji hapa Zanzibar.
Waziri Simbachawene pia, alitumia fursa hiyo kumpa pole Rais Dk. Mwinyi kufuatia kifo cha aliyekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kilichotokea hivi karibuni.
Sambamba na hayo, Waziri Simbachawene alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana 2020.
Waziri Simbachawene alimueleza Rais Dk. Mwinyi matumaini makubwa waliyonayo wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutokana na mwanga wa matumaini aliouonesha Dk. Mwinyi ndani ya siku mia moja za uongozi wake.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
|
|