Monday, November 25

Akina baba watakiwa kuwaunga mkono wanawake katika masuala ya uongozi.

 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

AKINABABA kisiwani Pemba wametakiwa kuwaunga mkono wanawake katika masuala ya uongozi, ili kutimiza malengo yao katika kuingia kwenye vyombo vya kutoa maamuzi.

Akizungumza na wananchi wa shehia ya Pandani Wilaya ya Wete Ofisa uwezeshaji kutoka chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Pemba, Asha Mussa Omar alisema, kuna mambo ambayo yanawahusu wanawake moja kwa moja, hivyo watakapoingia kwenye vyombo vya kutoa maamuzi waweze kujitetea.

Alieleza kuwa, ipo haja kwa akinababa na wananchi kwa ujumla kuwashirikisha, kuwahamasisha na kuwaandaa wanawake katika misingi mizuri, ili waingie katika vyombo vya kutoa maamuzi, jambo ambalo litasaidia kutetea haki zao.

“Wanawake ni waaminifu, wachapa kazi na watetezi, hivyo tunaamini kwamba watakapopata uongozi wataleta mabadiliko makubwa katika jamii, hivyo tusiwaache nyuma”, alisema.

Alisema kuwa, wameandaa timu ya wanaume wa mabadiliko kwa lengo la kuihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa mwanamke kuwa kiongozi.

Mwenyekiti wa timu hiyo Suleiman Massoud Said alisema kuwa, wanawake ni muhimu kushiriki katika uongozi, kwani ni wahanga wakubwa wa matatizo na ndio walezi wa familia, hivyo ni wasimamizi wazuri.

Aliwataka wanaume na familia kwa ujumla kumpa ridhaa mwanamke ya kuingia katika uongozi huku wakimshauri achunge heshima yake, ajisitiri, ili akawatetee kwa kufuata misingi ya dini yake.

Kwa upande wake Isack Maganzo Nzilamoshi kutoka kanisa la Katoliki alisema, dini haijamkataza mwanamke kuwa kiongozi ingawa watanakiwa wasivuke mipaka ya dini yao.

“Tusiwafungie ndani wanawake, tuwape nafasi wale ambao wameamua kugombea, ili waingie katika uongozi kwani wana vipaji vingi, hivyo tuache kuisingizia dini kwamba inakataza”, alisema Isack.

Nae Sultan Khalfan Nassor alisema, wanawake wanafanya vizuri wakati wanapokuwa viongozi, kwani wanajituma na kutatua migogoro katika jamii.

Mohamed Hassan Ali kutoka kwenye timu hiyo aliwataka wazazi kumjenga mtoto wa kike tangu akiwa mdogo na kuepuka kuwaoza waume mapema.

“Wazazi ndio wanaowakatisha watoto masomo, halafu tunalalamika kuwa wake zetu wanapokwenda hospitali wanazalishwa na wanaume, ili kuepuka hilo tuwasomeshe watoto wa kike”, alisema.

Sheha wa shehia hiyo Said Hamad Shehe alisema kuwa, elimu ni muhimu hivyo wanapaswa kuwatengeneza watoto mapema, ili kuwa bora na kuwa msaada kwa jamii iliyomzunguka.

Wakichangia katika Mkutano huo mshiriki Ali Swaleh Nassor aliwataka akinababa wenzake kuwathamini wanawake na kuacha tabia ya kuwabugua na kuwapiga, kwani wao ndio wasimamizi wa familia na jamii.

“Mwanamke anaweza kuwa kiongozi kwa sababu hayo majukumu aliyonayo katika familia ni makubwa na anayamudu, mambo anayoyabeba mwanamke sisi wanaume hatuyawezi, hivyo ipo haja ya kuwaunga mkono”, alisema mzee huyo.

Mshiriki Hamad Omar aliiomba timu hiyo kuishauri Serikali iruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi, ili iwe ni rahisi wanawake kugombea nafasi za uongozi.

“Kuna wanawake wana uwezo wa kuwa kiongozi lakini kama chama hakijamkubali hawawezi kumpitisha, hivyo ikiwa kutakuwa na mgombea binafsi naamini wanawake wengi watajitokeza”, alifahamisha.

Mkutano huo ni muendelezo wa mikutano ya kuwahamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi kwenye shehia mbali mbali kisiwani Pemba, ambao umeandaliwa na chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Pemba.