NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MABIBI na Mabwana shamba kisiwani Pemba wametakiwa kufanya utafiti katika mazao ya wakulima, ili kupambana na wadudu ambao huharibu mazao hayo.
Akifunga mafunzo katika Ukumbi wa Wizara ya Kilimo Weni Wete Pemba, Katibu Tawala Wilaya ndogo Kojani Makame Khamis Makame alisema, ni vyema mabibi na mabwana shamba kujitolea katika kuhakikisha wakulima wanazalisha mazao bora.
Alisema kuwa, wakulima hukata tamaa pale mazao yao yanapoiharibiwa na wadudu, hivyo ipo haja kwa mabibi na mabwana shamba kufanya utafiti kwenye mashamba ya wakulima, ili mazao yao yawe imara na kuzalisha zaidi.
“Watu wanajitahidi kulima mboga na viungo lakini kitu kinachowakumba ni kuwa mazao hayo huliwa na wadudu, hivyo tujitolee kwa moyo wetu wote, tutapata fadhila kwa Allah kwa sababu watapata kuzisaidia familia zao”, alisema Katibu huyo.
Aidha aliwataka watekelezaji wa mradi huo kuhakikisha kwamba wakulima wanaendelea kuzalisha hata utakapomalizika mradi, ili maisha ya wakulima yaboreke.
“Tuna aibu, inapomalizika mradi tu hatuoni muendelezo wake, unakuta hali za wakulima hazibadiliki, hivyo tunaweza kuwakosa wafadhili wetu kama hatutojirekebisha”, alielaza.
Katibu huyo pia aliwapongeza watekelezaji wa mradi huo wa viungo kwa kufanya utafiti na kubaini kuwa mradi huo unaweza kubadilisha maisha ya wakulima kwa kujipatia kipato kitakachowasaidia kujikwamua na maisha magumu.
Kwa upande wake meneja mradi Kanda ya Pemba Sharif Maalim Hamad alisema, lengo la mafunzo hao ni kuwa na taaluma juu ya Uwezeshaji wa skuli za wakulima, namna ya kuendesha shamba darasa na umuhimu wake, mbinu watakazotumia katika kuwawezesha wakulima pamoja na kuwaelimisha wakulima watu wazima.
“Sisi tunawafundisha mabibi na mabwana shamba, ili wafanye uchunguzi wa mashamba ya wakulima na kuwapa mafunzo yatakayowawezesha kujua dhana nzima ya uzalishaji, hii itasaidia kunyanyua kiapato cha wakulima”, alifahamisha.
Nae muwezeshaji wa skuli za wakulima Pemba Said Kombo aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kujituma zaidi kwa kutafuta elimu mtandaoni, kwani maradhi mengi visababishi vyake havionekani kwa macho.
“Mara nyingi tunaangalia athari na dalili tu, hatuangalii nini kilichosababisha, hivyo tusiridhike na mafunzo haya tu, tuwe na kawaida ya kupekuwa mtandaoni tutajifunza vitu mbali mbali ambavyo tutasaidia kuwaendeleza wakulima wetu”, alisema.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wameshukuru kupatiwa mafunzo hayo, kwani wamejifunza vitu vingi na kujifunza kwa vitendo zaidi, ambapo waliahidi kuyafanyia kazi kuhakikisha wanafanikiwa lengo walilolikusudia.
Mkutano huo wa siku tano kwa mabibi na mabwana shamba uliandaliwa na Chama Cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Jumuiya ya Uihifadhi wa Misitu Asili Pemba CFP na Shirika la PDF la Dar-es Saalaam, chini ya mradi wa viungo unaosimamiwa na Serikali na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya.