Monday, November 25

“NAIAGIZA WIAZARA YA ARDHI NA MAENDELEO YA MAKAAZI KUENDELEA KUTATUA MIGOGORO ILI KWAPATIA HAKI WANANCHI WANYONGE” MHE. HEMED MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza uongozi wa Wizara ya ardhi na maendeleo ya makaazi kufuatilia na kuharakisha utatuzi wa kesi za migogoro ya ardhi sambamba na kuwachukulia hatua kali watendaji wote wanaohusika katika migogoro hiyo.
Mhe. Hemed alilieza hayo wakati akiakhirisha mkutano wa pili wa baraza la kumi (10) ulionza vikao vyake febuari 10, mwaka huu katika ukumbi wa baraza la wawakilishi chukwani nje kidogo ya jiji la Zanzibar.
Alifafanua kwamba mbali na kero ya uwepo wa migogoro ya ardhi lakini pia kumekuwepo na muendelezo wa vitendo viovu vya rushwa katika upatikanaji wa haki ndani ya taasisi na katika jamii kwa ujumla.
Alisema kutokana kukithiri kwa changamoto hizo Serikali ya Awamu ya Nane imeamua kuimarisha utawala bora unaosiamamia sheria kwa kuhakikisha inazipatia ufumbuzi changamoto hizo kwa kuanzisha mahakama maalum kwa kesi zinazohusiana na rushwa pamoja na uhujumu wa uchumi wa nchi.
Akigusia tatizo la masuala ya udhalilishaji Mhe. Hemed ameleza bado jamii inaendelea kukumbwa na vitendo hivyo.
 Ambapo katika kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kuzifanyia marekebisho, ambapo ameeleza uwamuzi wa Serikali kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia kesi za masuala ya udhalilishaji.
Kwa upande wa kisiwa cha Pemba Mhe. Hemed amesema serikali inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi imedhamiria kueka kipaumbele maalum kwa uwekezaji ili kuleta uwiano katika visiwa viwili kwa kuifanya Pemba kuwa eneo la mkakati la uwekezaji lenye vivutio vitakavyowavutia na kuwashajihisha wawekezaji kujitokeza kwa wingi kwa kuanzisha na kuendesha miradi mikubwa ya kiuchumi kisiwani  humo.
Akilezea juu mapambano dhidi ya maradhi mbali mbali, Zanzibar ikiwa ni sehemu ya dunia aliwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na watalamu wa Afya kwa kufuata maelekezo na miongozo katika kujikinga maradhi mbali mbali yanayoambukiza na yasioambukiza.
Baraza la wawakilishi limeakhirishwa hadi Jumatano ya tarehe 05 Mei 2021 Majira ya saa Tatu kamili za Asubuhi (3:00).
Imetolewa na Kitengo  cha Habari (OMPR)
Febuari 25, 2021