Sunday, November 24

Wanawake watakiwa kuushiriki kikamilifu katika vyama vya Siasa ili waweze kuchaguliwa katika nafasi mbali mbali za uongozi

 

CHAMA cha Waandishi wa habari  Wanawake Tanzania Tawi la Pemba, kimewataka wanawake kushiriki kikamilifu katika vyama vya Siasa ili waweze kuchaguliwa katika nafasi mbali mbali za uongozi.

Hayo yalielezwa na Hafidh Abdi Said (CHADEMA) wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Shehia ya Gando Wilaya ya Wete, katika mkutano ulioandaliwa na TAMWA ikiwa ni kuwahamasisha akinamama kugombania nafasi za uongozi.

Aliwataka wanawake wote nchini kushiriki katika vyama vya Siasa kwa kuanzia uchukuaji wa kadi za uanachama na kuzilipia,kushiriki katika uchukuaji wa fomu za kugombania wakati wa uchaguzi kuanzia Tawi hadi Taifa kwa ujumla.

Hafidh aliwaeleza wananchi hao kuwa kushiriki katika vyama vya Siasa ni haki ya kila mwananchi, hivyo aliwasisitiza wanawake hao kujitoa ili waweze kuchaguliwa katika nafasi mbali mbali za uongozi.

“Cha msingi sisi wazazi au hata jamii kwa ujumla tuwafichueni wale wote ambao wana vipaji vya kuongoza na tuwaongoze kwa kuwapa taaluma hiyo ili wawe viongozi bora hapo baadae,”alifahamisha Hafidh.

Nae Khalfan Amour Mohammed kutoka Jumuiya ya wanasheria Pemba alieleza kuwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile Zanzibar imempa fursa mwanamke kuchagua au kuchaguliwa ili awe kiongozi.

Alieleza kuwa katika katiba hakuna sehemu hata moja ambayo imeanisha kuwa mwanamke hana haki ya kuwa kiongozi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali mwanamke ana haki sawa na mwanamme katika uongozi.

“Wakati umefika kwa wanawake kujitokeza kwa wingi katika kugombania nafasi mbali mbali za uongozi kuanzia nafasi Tawi, udiwani, Uwakilishi, Ubunge na hata urais pia,”alieleza Amour.

Alifahamisha kuwa licha ya uchaguzi kuwa kumalizika hapa Tanzania, lakini TAMWA itaendelea kuwashawishi wanawake kujihusisha na uongozi na kila unapofanyika uchaguzi mkuu wajitokeze kuwania nafasi za uongozi.

Mapema akijibu swali lililoulizwa na mwananchi Mohammed Kaimu kuhusiana na mikakati gani ambayo inachukuwa kwa wanawake, Ofisa miradi kutoka TAMWA Asha Mussa Omar alieleza kuwa mikakati ambayo TAMWA wanachukua ni kuihamasisha jamii ili kutoa fursa kwa wanawake katika nafasi za uongozi.

Aidha Ofisa huyo aliendelea kusema kuwa ni kuwawezesha wanawake kuingia katika vikundi vya ujasiriamali ambapo hapo baadae waweze kujilipia na  kuingia katika uongozi wakati wa uchaguzi.

Hata hivyo  TAMWA inamuandaa mwanamke kwa kumsomesha taratibu na misingi yote ambayo itamsaidia hapo baadae na kuweza kuweka heshima katika familia zao.